BAADA ya dili la kutua Yanga kukwama, kiungo mkabaji Kelvin Nashoni aliyekuwa akitajwa kutua Pamba Jiji sasa ataendelea kusalia Singida Black Stars, huku kiungo Amade Momade akitolewa kwa mkopo wa miezi sita kwenda Tanzania Prisons.
Nashon alikuwa anahusishwa na Yanga pamoja na Pamba Jiji kwa mkopo, lakini mambo yameenda tofauti sasa anaendelea kubaki katika timu hiyo ya Singida BS.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Singida BS, Hussein Masanza alisema baada ya dili la Yanga kukwama, Nashon anabaki kuwa mchezaji wa timu hiyo yenye maskani yake mjini Singida, japo kwa sasa ipo kambini jijini Arusha na kiungo huyo wa zamani wa Geita tayari anaendelea kujiweka fiti kwa ajili ya kumaliza msimu.
“Wachezaji wote ambao hatujatoa taarifa zao kama tumewatoa kwa mkopo wataendelea kubaki ndani ya timu kama ambavyo wengine wamerejeshwa kutoka timu mbalimbali walizokuwa wanazitumikia kwa mkopo,” alisema Masanza na kuongeza;
“Dirisha hili tumetoa taarifa ya Israel Mwenda pekee kutolewa kwa mkopo na tumemrejesha kikosini Hussein Masalanga kutoka Tabora United, Shiga Jackson na wengine ambao bado taarifa zitaendelea kutoka.”
Wakati huo huo, Mwanaspoti limezinasa taarifa za kiungo mkabaji raia wa Msumbiji, Momade, kutolewa kwa mkopo kwenda Tanzania Prisons kwa mkataba wa miezi sita.
Hata hivyo, Masanza alipoulizwa juu ya taarifa za kiungo huyo wa kimataifa wa timu ya taifa ya Msumbiji aliyewahi kukipiga pia UD Songo na Namungo, alisema mambo yakiwa tayari wataweka wazi.