LILE dili la mshambuliaji wa Azam FC, Adam Adam la kwenda kwa mkopo wa miezi sita Kagera Sugar limeyeyuka na sasa anatajwa yupo hatua ya mwisho kujiunga na chama lake la zamani la Tanzania Prisons.
Mwanaspoti limepata taarifa za ndani kilichokwamisha Adam asijiunge na Kagera ambayo ilishakubaliwa na Azam, sababu ni viongozi wa timu hiyo kutozungumza chochote na mchezaji wala kumpa programu za nini akifanye, hivyo akawa amebakia njia panda.
“Kagera ilishajibiwa na uongozi wa Azam kumchukua Adam aliyeomba kutolewa kwa mkopo ili akapate nafasi ya kucheza, lakini baada ya hapo viongozi wa timu hiyo hawakuzungumza chochote na mchezaji, kwani walipaswa kumpigia simu na kumpa programu zao,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Mchezaji akaomba dili hilo lisitishwe na anaweza akajiunga na Prisons ambayo inaendelea kukamilisha baadhi ya taratibu na imezungumza na mchezaji wamekubaliana na yupo tayari kujiunga nao.”
Alipoulizwa Adam kuhusiana na sakata hilo alijibu kwa kifupi; “Ni kweli naweza nikajiunga na Prisons kama mambo yatakwenda vizuri, kuhusiana na Kagera naomba nisiliongelee.”
Adam alijiunga na Azam kwa mkataba wa mwaka mmoja msimu huu akitokea Mashujaa ambako alifunga mabao saba katika mechi za Ligi Kuu (2023/24) kabla ya hapo alishawahi kukipiga JKT Stars, Polisi Dodoma, Mtibwa Sugar, Ihefu (sasa Singida BS) na KMC.