Kizungumkuti magari ya shule | Mwananchi

Dar/mikoani. Wakati shule nyingi zikifunguliwa Jumatatu ya Januari 13, 2025, Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani linaendelea na ukaguzi wa mabasi ya wanafunzi huku likionya kuchukua hatua kali za kisheria kwa wote watakaokiuka sheria na miongozo.

Mamia ya watoto, hasa wanaosoma shule za mijini, wamekuwa wakitumia usafiri wa mabasi ya shule wakati wanakwenda shule ama kurudi nyumbani. Hata hivyo, mabasi hayo yamekuwa yakilalamikiwa kuwa mabovu huku yakijaza wanafunzi kuliko uwezo wake.

Huko nyuma, yametokea matukio kadhaa ya mabasi ya wanafunzi kukamatwa yakiwa yamejaza kupita kiasi, jambo lililohatarisha usalama wa wanafunzi hao endapo itatokea ajali kutokana na uzembe.

Mkuu wa kitengo cha usalama barabarani Jiji la Tanga, Rajabu Ngumbi akikagua moja ya magari yanayotumiwa kubeba wanafunzi wa shule jijini humo, siku chache kabla ya shule kufunguliwa. Picha na Rajabu Athumani

Vilevile, zimetokea ajali kadhaa zilizohusisha mabasi ya wanafunzi na kusababisha vifo vyao. Mbali na hayo, vitendo vya ukatili kwa wanafunzi viliripotiwa kufanywa ndani ya magari hayo.

Kutokana na matukio hayo, Jeshi la Polisi nchini limekuwa likifanya ukaguzi wa magari yanayowasafirisha wanafunzi ili kuhakikisha wanafunzi wanatumia usafiri ambao ni salama wanapokwenda na kurudi shuleni.

Katika ukaguzi wa mabasi hayo, Jeshi la Polisi limebaini kasoro kadhaa, ikiwemo ubovu kwenye mfumo wa breki, umeme, sakafu, kutokuwa na mikanda ya usalama, ubovu wa siti, na uchakavu wa bodi la gari.

Baadhi ya adhabu zitakazochukuliwa kwa watakaokiuka Sheria ya Usalama Barabarani ni pamoja na madereva kufutiwa leseni zao na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Mmoja wa madereva wa mabasi ya shule moja mjini Morogoro (jina limehifadhiwa) amesema mabasi mengi ni mabovu kwa sababu hayanunuliwi yakiwa mapya.

“Hawa wenye shule huwa wananunua mabasi yakiwa yamechakaa na mengi yalikuwa ni daladala; kinachofanyika ni kupigwa rangi tu,” amesema dereva huyo.

Naye Hossein Mdoe, dereva wa Raskazone English Medium School, amesema suala la kuwa na gari ambalo limekaguliwa ni muhimu kwani ni kwa ajili ya usalama wao na wanafunzi.

“Wamiliki wa shule washiriki kuhakiki magari yao kwa kuyapeleka yakaguliwe na Jeshi la Polisi kwa kuwa kwenye ukaguzi huo unakupa nafasi ya kujiamini kazini,” amesema Mdoe.

Licha ya ukaguzi huo kufanyika, bado kunashuhudiwa magari ambayo hayajapakwa rangi ya njano, magari madogo kama Noah, Hiace maarufu kama vipanya, Probox maarufu kama michomoko, na hata bajaji yakionekana kupita maeneo ya makazi na barabarani yakiwa yanabeba wanafunzi. Magari mengine ni chakavu.

Alipoulizwa Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga amesema suala hilo linashughulikiwa na Jeshi la Polisi la Usalama Barabarani.

Februari 28, 2023, Kamishna wa Elimu, Dk. Lyabwene Mtahabwa, alitoa waraka wa elimu Na. 1 wa mwaka 2023 kuhusu uboreshaji wa huduma ya magari/mabasi yanayotumika kusafirisha wanafunzi.

Waraka huo uliotumwa kwa wadau mbalimbali wa elimu, sehemu ya maelezo yake ulieleza: “Thamani ya rasilimali watoto ni kubwa kuliko thamani ya rasilimali yoyote ambayo tumejaliwa kuwa nayo katika nchi yetu.”

Dk Mtahabwa alisema pamoja na ukweli huo, imebainika baadhi ya watoa huduma kwa watoto wamekuwa na tabia zenye mwelekeo wa kuleta mmomonyoko wa maadili, kuathiri ukuaji, ujifunzaji, na kuhatarisha ustawi wa watoto kwa ujumla.

Katika waraka huo, alieleza kuwa unalenga kuboresha utoaji wa huduma ya usafiri wa magari/mabasi kwa wanafunzi kwenda na kurudi kutoka shuleni kufuatia matukio ya ukatili dhidi ya wanafunzi yanayofanywa na baadhi ya watoa huduma, ikiwemo ubakaji na ulawiti.

Aidha, baadhi ya tabia za watoa huduma zina viashiria vya kuleta mmomonyoko wa maadili, kuathiri ukuaji, ujifunzaji, na kuhatarisha ustawi wa watoto kwa ujumla.

Miongoni mwa kasoro ni ratiba ya safari inayoanza alfajiri (mfano: saa 11:00) na kuwalazimu watoto wadogo kukatisha usingizi usiku wa manane na hivyo kuathiri ukuaji na ujifunzaji wao; na au ratiba za safari za kutoka shule zinazowafanya baadhi ya wanafunzi kufikishwa nyumbani usiku, ilhali vipindi vya masomo vimeisha mapema alasiri.

Kamishna huyo wa elimu alimtaka kila mmiliki wa shule kuhakikisha kuna mhudumu wa kike na wa kiume katika kila gari/basi linalosafirisha wanafunzi kuanzia mwanzo hadi mwisho wa safari.

“Kuwa na magari/mabasi yenye vioo angavu (visivyokuwa tinted) yanayotumika kusafirisha wanafunzi na kuwa na ratiba rafiki za safari ili wanafunzi, hususan watoto wadogo, wapate muda wa kutosha kupumzika kwa ajili ya ukuaji wao,” unaeleza waraka huo.

Ukaguzi na hatua za kisheria

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, maofisa wa Kikosi cha Usalama Barabarani wamesema wanaendelea na ukaguzi wa magari ya wanafunzi na watachukua hatua kwa madereva watukutu wasiofuata sheria.

Kamanda wa Trafiki Mkoa wa Songwe, Joseph Bukombe, amesema tangu shule zilipofungwa, walianza ukaguzi wa magari ya shule na yaliyobainika kuwa na upungufu yalipelekwa kufanyiwa marekebisho.

“Tumekagua zaidi ya magari 20 kwa Mkoa wa Songwe, tumejipanga kuendelea na ukaguzi baada ya shule kufunguliwa. Tutatoa elimu ya vitendo kwa wanafunzi namna ya kuvuka barabara, na madereva wa bajaji na pikipiki watashiriki,” amesema Bukombe.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Tanga, Willy Mwamasika, amesema watawachukulia hatua wamiliki na madereva wa magari ya shule ambayo yatabeba wanafunzi bila kufanyiwa ukaguzi wa kitaalamu.

Amesema mpaka sasa zaidi ya mabasi 30 ambayo yanakwenda kutumiwa na wanafunzi kwa shule mbalimbali Mkoa wa Tanga yamekaguliwa katika ukaguzi uliofanywa na ofisi yake, na zoezi linaendelea.

“Mpaka sasa tumekagua magari zaidi ya 30, tunataka wamiliki wa magari, wakuu wa shule, na wamiliki wajitokeze kwa ukaguzi kufanyika kabla ya hatua kuchukuliwa ili kulinda usalama wa watoto.

“Maeneo yanayofanyiwa ukaguzi ni matairi, milango, taa, siti, bodi, na maeneo mengine muhimu. Lengo ni kuhakikisha vifaa vyote vinakuwa vizuri wakati wote,” amesema Mwamasika.

Mkuu wa Operesheni Mkoa wa Mwanza, Aloyce Nyantora, kwa niaba ya Kamanda wa Polisi mkoani humo, Wilbrod Mutafungwa amewataka wamiliki na madereva wa magari ya shule kuyapeleka magari yao yakakaguliwe na kupewa hati ya utambulisho.

Amesema operesheni ya Juni 2024 ilikagua magari 252, ambapo 35 yalikuwa mabovu na hivyo kutoruhusiwa kubeba wanafunzi hadi yalipofanyiwa ukarabati.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza, Sunday Ibrahim, amesema ukaguzi wa magari ya shule ulianza Desemba 14 – 31, 2024, ukiambatana na utoaji wa elimu na kukabidhi hati ya kutambua endapo gari limekaguliwa.

Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Martin Nkwabi, amepiga marufuku magari ya shule yenye vioo vyeusi (tinted) akisema ni hatari kwa wanafunzi kwani sababu anayekuwemo ndani haonekani.

Amewataka madereva kuzingatia kanuni na taratibu za kuwafuata wanafunzi majumbani, akieleza kuwa baadhi huwafuata saa 10 alfajiri na kuwarudisha kati ya saa 3 hadi saa 4 usiku kutokana na umbali wanafunzi wanapoishi.

“Gari la wanafunzi haliruhusiwi kutembea likiwa limebeba wanafunzi zaidi ya saa 11 jioni… miongozo inaelekeza kila gari la shule linatakiwa kuwa na mhudumu wa jinsia ya kike ama wahudumu wa kike wawili, au mmoja kati ya wahudumu wawili,” amesema.

Amewaonya wamiliki wa magari ya shule wanaonunua magari mabovu, akiwakumbusha wanafunzi wanatakiwa kubebwa kwenye magari bora na salama.

Magari Mabovu Morogoro    

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, amesema jumla ya mabasi 24 ya wanafunzi yamekaguliwa, ambapo 16 yalikutwa na makosa mbalimbali na kusitishiwa safari hadi yatakaporekebishwa.

Ameeleza ubovu uliokutwa kwenye mabasi hayo kuwa ni ubovu kwenye mfumo wa breki, umeme, sakafu, kutokuwa na mikanda ya usalama, ubovu wa siti, na uchakavu wa bodi.

“Mabasi tuliyoyakuta na ubovu, tumeyazuia kuendelea na kazi. Wakikiuka agizo hilo, tukiyakamata tutachukua hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani,” amesema Mkama.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Katavi, Leopold Fungu, amesema pamoja na ukaguzi walioufanya, mkakati wao ni kufanya msako wa kukamata magari ambayo hayakukaguliwa baada ya shule kufunguliwa.

Amesema katika ukaguzi wa awali, magari ya wanafunzi 20 yalikaguliwa, ambapo matano yalikutwa na matatizo na mawili yalifungiwa moja kwa moja na kutakiwa kubadilishwa mfumo.

“Baada ya shule kufunguliwa, tutakuwa na operesheni ya kukamata magari ambayo hayakukaguliwa. Ukaguzi wa kwanza ulienda vizuri na tulitoa hati ya ukaguzi kwa yaliyokaguliwa,” amesema Fungu.

Akizungumzia ukaguzi huo, Jumatano Januari 8, 2025, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema mabasi yanayobeba wanafunzi yamekaguliwa kama ilivyo utaratibu waliojiwekea miaka yote.

“Mabasi yanayobeba wanafunzi yamekaguliwa kama ilivyo miaka yote,” amesema.

Katika maelezo yake, Kamanda Muliro hakufafanua ni lini ukaguzi huo ulifanyika kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Wamiliki wa Shule Tanzania (Tamongsco), Yusto Ntungi, amesema ubora wa usafiri kwa wanafunzi ni kipaumbele chao, lakini changamoto ni ubovu wa barabara za mitaani.

“Nchi nzima tunaelekea kwenye ukaguzi wa magari na shule nyingi zinajitahidi kununua magari mapya, lakini tatizo ni ruti za hayo magari; hali ya barabara ni mbaya mno,” amesema.

Amesema wamekuwa wakiwasilisha kero hiyo kwenye vikao vyao na mamlaka za Serikali, lakini utatuzi wake umekuwa kitendawili.

“Wajibu wa mmiliki wa shule ni kuboresha shule na vifaa vya kufundishia. Wakati huu shule zinafunguliwa, wengi wamenunua magari mapya, lakini yape mwezi mmoja tu, utaona jinsi yalivyochakaa, kwa sababu barabara ni mbovu.

“Ni tofauti na daladala zinazopita kwenye barabara za lami; huku mitaani barabara ni mbovu, zinatosha kupata magari madogo. Sasa ukipeleka gari kubwa kama Toyota Coaster, lazima liharibike mapema,” amesema.

Mmoja wa wamiliki wa shule, Selestine Mbilinyi, mkazi wa Manispaa ya Morogoro, amepongeza hatua hiyo akisema utaratibu wa kukagua mabasi ya shule ni mzuri na yeye anaunga mkono kwa kupeleka mabasi ya shule yake ili yakakaguliwe.

“Mabasi yangu bado hayajakaguliwa, lakini nitawaambia madereva wangu wapeleke yakakaguliwe na yale,” amesema.

Related Posts