Nondo aibua mpya utekaji wake, Polisi yamjibu

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya Chama cha ACT- Wazalendo, Abdul Nondo amesikitishwa na ukimya wa Jeshi la Polisi kushindwa kumpatia mrejesho wa tukio la kutekwa kwake na watu wasiojulikana alilofanyiwa Desemba 1, 2024.

Amesema jambo hilo linazidi kumpatia uchungu na hofu zaidi juu ya mustakabali wa maisha na kesho yake dhidi ya kundi hilo, huku akieleza hata mwaka 2018 alifanyiwa kitendo kama hicho lakini hadi sasa bado hajui na hajawahi kusikia watuhumiwa waliowahi kushikiliwa.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro akijibu kuhusu tukio la kutekwa kwake, amesema anachojua watu wanafanya kazi kubwa ila si kila kinachofanyika lazima kisemwe hadharani.

“Kazi za kiuchunguzi zinafanyika lakini maadili ya kiutendaji hatutaki kutangaza kila kitu unachokifuatilia au mabacho unakifuatilia huwezi kutangaza,” amesema Muliro.

Muliro amesema jeshi haliwezi kumtangaza Nondo kila siku, huku akisema si kweli kwamba uchunguzi haufanywi isipokuwa unafanyika vizuri.

“Uchunguzi unafanyika vizuri kabisa na si kwamba kesi yake imetelekezwa na hata yeye mwenyewe anajua ila anayotaka hatuwezi kuitisha mkutano na vyombo vya habari utakuwa si upelelezi,” amesema.

Katika maelezo yake, Muliro amesema Nondo wakati anaandikiwa jalada lake alipewa ofisa upelelezi wa kuchunguza huku akitaka aulizwe (Nondo), kama anazungumza naye.

Mwananchi ilipomrudia Nondo kwa mara ya pili ajibu kama anawasiliana na ofisi upelelezi wa kesi yake simu yake haikupokelewa.

Leo Alhamisi, Januari 9, 2025, Nondo amekutana na waandishi wa habari, makao makuu ya chama hicho, Magomeni jijini Dar es Salaam na kuelezea tukio hilo na hatua zinazofuata kwenye harakati zake za kisiasa.

Amesimulia hadharani tukio lake la kutekwa na wasiojulika lilotokea Desemba Mosi, 2024 nje ya kituo cha mabasi Magufuli Mbezi Luis, Dar es Salaam na kwenda kutelekezwa maeneo ya ufukwe wa Coco jijini humo.

“Bado nina hofu juu ya usalama wangu, nakumbuka nikiwa hospitali polisi walikuja kunihoji niliwapa ushirikiano wote, lakini hadi sasa nazungumza hakuna mrejesho wowote wa kujua Jeshi la Polisi wamefikia wapi au watuhumiwa wamekamatwa,” amesema.

Nondo amesema jambo hilo linamkosesha amani na chombo hicho, huku akisema siyo tukio hilo kuna kupotea na kutekwa watu lakini hakuna majibu yaliyotolewa na Jeshi la Polisi.

“Matukio ya kutekwa ikiwemo lililonitokea na mengine kuacha yaendelee kutokea na hakuna majibu ya uchunguzi yanayowekwa hadharani hata moja ikiwemo 81 yaliyotolewa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), tafsiri yake ulinzi na  usalama wetu nchini uko hatarini,” amesema.

Nondo ambaye ni mwathirika wa kadhia hiyo mara mbili tofauti ikiwemo lile lilotokea mwaka 2018 alipotekwa Dar es Salaam na kuonekana mkoani Iringa, amesema ni lazima uchunguzi utolewe na Jeshi la Polisi ili wanaofanya hayo mambo wajulikane.

“Nashangaa binafsi polisi walikuja hospitali na niliwapa ushirikiano wote lakini nimeshangaa hadi sasa hakuna ninachojua kinaendelea, Jeshi la Polisi liko kimya nilitekwa watu wanaona na kuna pingu ilikabidhiwa inakuwaje wanakuwa kimya,” amesema Nondo.

Amehoji kwanini polisi wasifanye uchunguzi mahususi na matukio yote yanayojitokeza?

“Kitendo cha tukio langu kuendelea kukaliwa kimya na mengine yanaendelea kutokea wanatufanya tuendelee kuwatilia mashaka wanafanya wao ndiyo maana wanashindwa kujichunguza,” amesema.

Nondo amesema suala la ulinzi na usalama lipo juu ya mipaka ya itikadi ili kukomesha matukio ya utekaji ni muhimu jamii ya Kitanzania kuungana pamoja kupaza sauti na kukemea.

“Matukio ya utekaji ni hatari na Watanzania wasidhani wako salama kwavile yanayotokea baadhi ya watu, tutakuwa tunajidanganya namna matukio haya yalipofikia si ya vyama tena yamevuka mipaka na itikadi,” amesema.

Amesema kuendelee kukaa kimya ni kufanya yaendelee, suala la usalama lazima lipewe kipaumbele na vyombo vya ulinzi lazima viwajibike kuhakikisha ulinzi unatamalaki muda wote.

Nondo katika mkutano huo amependekeza njia za kukomesha matukio ya utekaji nchini yanayofanywa na wanaidaiwa hawajulikani ikiwemo Watanzania kuungana kupaza sauti bila kujali itikadi ya vyama kukomesha wimbi hilo kwa maslahi ya usalama wao.

Pia, amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan aunde Tume huru ya kijaji kuchunguza ili kubaini kiini cha tatizo hilo na mauaji ya utata na kuwabaini wahusika.

Pia, Jeshi la Polisi kuzingatia utaratibu wa ukamatwaji kwa kuvaa sare kujitambulisha na kueleza sababu za kukamata mtuhumiwa na vyombo vya uchunguzi kutoa majibu ili wanaofanya vitendo hivyo wajulikane.

Septemba 8, 2024, Rais Samia alitoa agizo kwa vyombo vya uchunguzi kuchunguza matukio ya utekaji. Ni baada ya tukio la kuuawa kwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema, Ally Kibao lililotokea siku moja baada ya kutekwa akiwa kwenye basi kwenda nyumbani kwao mkoani Tanga.

Tukio hilo lilitokea Septemba 6, 2024 Tegeta, mbele ya Jengo la Kibo Complex, jijini Dar es Salaam na watu waliokuwa na gari mbili zilizozuia basi la Tashrif akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kwenda Tanga.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X, Rais Samia Suluhu Hassan alieleza kusikitishwa na tukio hilo, huku akiviagiza vyombo vya uchunguzi kumpelekea taarifa za kina.

Katika taarifa yake hiyo, alitoa pole kwa viongozi wa Chadema, wanafamilia wa Kibao na marafiki, akisisitiza Serikali anayoiongoza haitavumilia vitendo vya kikatili vya namna hiyo.

“Nimeagiza vyombo vya uchunguzi kuniletea taarifa ya kina kuhusu tukio hili baya kabisa na mengine ya namna hii haraka. Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana Haki ya kuishi.

“Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii,” aliandika katika ukurasa wake wa X.

Related Posts