Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda ameagiza mkandarasi anayejenga ofisi na makao makuu ya Halmashauri ya Jiji la Arusha kukamilisha awamu ya pili ya ujenzi Mei badala ya Julai, 2025 kama ilivyokuwa imepangwa awali.
Ametoa agizo hilo leo Alhamisi Januari 9, 2025 alipokagua ujenzi unaoendelea.
Katika ukaguzi huo alielezwa mradi ulisuasua kutokana na changamoto kadhaa.
Makonda amemtaka mkandarasi kuhakikisha wanakamilisha mradi kwa kufanya kazi usiku na mchana.
“Tunataka hili jengo likamilike hatutaki tena hadithi, kumbukeni hili jengo siyo mali ya sisi viongozi ni mali ya wananchi,” amesema.
Akizungumzia elimu, Makonda amewaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayeshindwa kwenda shule kwa sababu ya changamoto, ikiwemo ukosefu wa madarasa.
“Hakikisheni asiwepo mwanafunzi atakayekosa kwenda shule kwa sababu ya kutokuwa na madarasa, fedha zipo. Nafahamu kuna changamoto pale Arusha DC, Karatu, mkoa mzima wanafunzi wasikose nafasi eti kwa sababu hakuna dawati, sijui madarasa.
“Kule ambako kuna changamoto za kimanunuzi na mnaona hamtaweza kwenda na kasi hakikisheni mnatafuta njia mbadala hao watoto waende shule,” ameagiza.
Makonda ameagiza Halmashauri ya Jiji la Arusha kutafuta na kusimamia wakandarasi watakaojenga vivuko 21 katika kata mbalimbali kabla msimu wa mvua haujaanza ili wananchi wasikwame kufanya shughuli zao.
“Jifungieni mtafute wakandarasi watakaoweza kufanya kazi hiyo, isije kunyesha mvua hapa wananchi wakashindwa kuvuka, pesa iko kwenye akaunti tutakuwa hatujawatendea haki wananchi,” amesema.
Kuhusu ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi jijini Arusha, amesema mwaka huu lazima wananchi waone matokeo ya ujenzi wa kituo hicho.
“Lazima Jiji la Arusha tuwe na stendi na siyo maneno ya stendi, mwaka huu lazima wananchi waone matokeo. Mtakapokwama sisi mkoa tuko tayari kuwasaidia kuhakikisha tuna stendi ya kisasa. Arusha tunakosaje soko na stendi? Ni maneno matupu. Mwaka huu siyo wa maneno, tuwaheshimishe viongozi wetu waliotupa nafasi kwa kuweka alama,” amesema.
Makonda amesema: “Tujipange kwenye kuleta matokeo badala ya kujipanga kujibishana kwa maneno, wa maneno waacheni tu waseme maneno hayakosekani, aidha ni sisi wenyewe ndani ya chama tawala maneno yapo tu hata kwenye familia maneno yapo wanajadiliana na wanatofautiana.”
Msimamizi wa mradi huo, Rashid Kapwani amesema awamu ya pili ya mradi huo inayogharimu Sh6.2 bilioni ilipangwa kukamilika Julai, 2025.
Amesema kipindi cha Septemba hadi Novemba, 2024 kulikuwa na changamoto ya upatikanaji wa nondo ila limeshatatuliwa na ujenzi unaendelea.
Meya wa Jiji la Arusha, Maxmillian Iranghe, amesema awamu hiyo ya pili iliyokuwa imepangwa kukamilika Julai, 2025 watahakikisha kabla ya muda huo wanakaa na kamati ya fedha, wataalamu na baraza la madiwa waangalie namna nzuri ya kuhakikisha mkataba unasainiwa ili kazi ya awamu ya tatu ianze haraka.
Amesema wiki hii jiji limepokea magari mawili mapya na wanatarajia kupokea greda moja, akieleza watakwenda kata zote 25 kuboresha barabara zipitike wakati wote.