Aliyepandikizwa figo ya nguruwe afariki dunia

Massachusetts. Richard Slayman kutoka Massachusetts aliyepandikizwa figo ya Nguruwe amefariki dunia hii leo Jumapili Mei 12, 2024.

Kwa mujibu wa BBC Slayman (62) ambaye ni mtu wa kwanza kupandikizwa figo ya mnyama huyo iliyobadilishwa vinasaba amefariki ikiwa ni miezi miwili baada ya kufanyiwa upasuaji huo mnamo Machi 16, 2024.

Slayman aliruhusiwa Aprili 4, 2024 baada ya kuendelea vizuri kwa mujibu wa madaktari wa hospitali kuu ya Massachusetts (MGH) alipofanyiwa upasuaji huo.

Awali, mtu huyo alikuwa akiugua ugonjwa wa figo ingawa katika taarifa ya Hospitali ya MGH imesema hii leo kwamba hakuna dalili kuhusu kifo chake ni matokeo ya upandikizaji huo.

Katika historia ya marehemu mbali na ugonjwa wa figo, pia aliugua kisukari na shinikizo la damu. Mnamo 2018, alipandikizwa figo ya binadamu, lakini ilianza kushindwa kufanya kazi baada ya miaka mitano.

Kufuatia upandikizaji wa figo yake ya nguruwe mnamo Machi 16, madaktari wake walithibitisha kuwa hahitaji tena huduma ya kusafisha damu baada ya kiungo hicho kipya kusemekana kufanya kazi vizuri.

Aidha Hospitali ya MGH imeweka wazi kwamba imehuzunishwa na kifo chake hicho cha ghafla na kutoa rambirambi kwa familia yake.

Hata hivyo awali wakati akifanyiwa upasuaji Mkuu wa Madaktari katika hospitali hiyo David Klassen alisema upasuaji huoi wa kutumia viungo vya wanyama kwenda kwa binadamu ni tumaini kubwa miongoni mwa wagonjwa wanaokabiliwa na ugonjwa huo.

Vilevile taarifa ya hospitali ilisema ataendelea na dawa kadhaa za kinga ya mwili na kufuatiliwa kwa karibu na vipimo vya damu na mkojo mara tatu kwa wiki na pia kuonwa na daktari mara mbili kwa wiki.

Related Posts