MSHAMBULIAJI wa Yanga, Clement Mzize ameendelea kuwa gumzo kwa mashabiki na wadau wa soka kutuokana na kiwango kizuri alichokionyesha hadi sasa katika mechi za mashindano zote za timu hiyo.
Akiwa ndiye kinara wa mabao wa Yanga katika Ligi Kuu Bara akifunga mabao sita na kuasisti mara tatu, mbali na mabao matano aliyoyafunga kwenye michuano ya CAF kwa msimu huu yakiwamo mawili ya wikiendi iliyopita dhidi ya TP Mazembe na kufufua tumaini la timu hiyo ya Jangwani kuitafuta tiketi ya robo fainali.
Kiwango hicho cha mshambuliaji huyo chipukizi, kimemshtua na kumuibua straika wa zamani wa Stand United, Mbeya City na Pamba, Mnaigeria Abasirim Chidiebere aliyempongeza, huku akimtaka kutobweteka ili aaendelee kuandika historia itakayodumu klabuni.
Mzize amekuwa na kiwango bora msimu huu ambapo wikiendi iliyopita alifunga mara mbili wakati Yanga ikiifumua TP Mazembe ya DR Congo kwa mabao 3-1 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa iliyopigwa Kwa Mkapa. Mabao hayo yamemfanya Mzize kufikisha jumla ya mabao 12 katika mechi 25 za michuano yote msimu huu hadi sasa, kwani alifunga mengine matatu katika mechi za awali za CAF, ametupia sita ya Ligi Kuu na jingine la Ngao ya Jamii.
Nyota huyo aliyeibuka kutoka timu ya vijana, anashika nafasi ya tatu ya wachezaji waliohusika na mabao mengi katika Ligi Kuu hadi sasa akiwa nyuma ya Feisal Salum wa Azam mwenye 13, Jean Ahoua wa Simba (12) na yeye mwenye 9 zikiwamo asisti tatu alizonazo hadi sasa.
Akimzungumzia mchezaji huyo, Chidiebere alisema Mzize ameonyesha amekomaa na yuko tayari kuandika historia baada ya kupata uzoefu chini ya mkali, Fiston Mayele aliyetimkia Pyramids ya Misri.
“Namfuatilia vizuri Mzize, amepambana kutafuta nafasi na kutoa ushindani kwa wachezaji wanaomzidi, tayari ameshakomaa na ni mchezaji mzuri. Juzi nilimuona dhidi ya Mazembe amecheza vizuri na kwa daraja la juu mno,” alisema Chidiebere na kuongeza;
“Ni mchezaji ambaye Watanzania wanatakiwa wajue tayari wanaye mtu wa kumtegemea waache mambo ya zamani ya kutoamini vijana, Mzize ameshakomaa kubeba majukumu na ni mchezaji mzuri kwa sababu ana nguvu, kasi, kupiga mashuti na anaweza kucheza winga na mshambuliaji wa kati.”
Chidiebere alitoa tahadhari kwa wachezaji wazawa kutoridhika mapema wanapoanza kupata mafanikio na kuaminiwa, wanapaswa kupambana dhidi ya wageni wanaokuja na uchu wa kufanikiwa, kujitafuta na kutaka kutoka kwenda hatua nyingine.
“Wakijituma na kufanya mazuri watafanikiwa. Waache kujiona tayari nimeshafika wajue kwamba bado kabisa wawe na uchu wa mafanikio,” alisema.