Dar es Salaam. Mama mwenye umri wa miaka 52 (jina limehifadhiwa), mkazi wa Bagamoyo mkoani Pwani, amepitia changamoto kubwa ya kiafya baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe wa kilo 5.5 uliokuwa kwenye mfuko wake wa mayai.
Mama huyo akizungumza na Mwananchi, ameeleza namna alivyogundua tatizo hilo, ambalo anasema lilimuanza Agosti, 2024 na kumsababishia maumivu makali ya tumbo, kiasi cha kushindwa kufanya kazi za nyumbani na kulazimika kutumia muda mwingi akiwa amelala.
“Mwezi wa nane mwaka jana nilianza kuhisi maumivu makali tumboni. Tumbo lilikuwa limejaa kama la mama mjamzito na sikuweza kukaa wala kusimama. Pia nilikuwa nashindwa kula na nikila ni chakula kidogo sana na hata kulala usingizi kwangu ilikuwa shida kutokana na maumivu niliyokuwa nayapitia,” alisema mama huyo.
Alisema hali hiyo ilimtesa sana: “Nilikuwa silali, nikilala ni ule usingizi wa mang’amung’amu, na kilichokuwa kinanishangaza zaidi, ni tumbo langu lilikuwa linaongezeka kila kukicha kwa kasi kama nina mimba.”
Hata hivyo, anasema alienda Hospitali ya Serikali iliyopo eneo la Bunju kwa ajili ya matibabu, kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Mwananyamala.
Akizungumzia ugonjwa wa mama yake, mtoto wa pekee aliyejitambulisha kwa jina la Yahaya Miraji alisema walipoona hali ya mama yake hali inazidi kuwa mbaya, waliamua kumpeleka hospitalini kwa vipimo.
“Tulianza na kipimo cha ultrasound hospitalini na baadaye tukapata uhamisho kwenda Mwananyamala, ambako walifanya kipimo cha CT Scan. Ndipo wakagundua kuwepo kwa uvimbe kwenye mfuko wa mayai,” alisema Yahaya.
Alisema baada ya matokeo ya vipimo, madaktari walimuanzishia mama yake kliniki, lakini alikumbana na changamoto za shinikizo la damu kushuka na kupanda.
Hata hivyo, kwa juhudi na msaada wa madaktari, Januari 7, 2025 upasuaji wa saa saba ulifanikiwa na uvimbe huo ukaondolewa.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Taiba Haidar kutoka Hospitali ya Rufaa ya mkoa Mwananyamala anasema uvimbe uliotolewa kwa mwanamke huyo una kilo 5.5 na ulikuwa kwenye mfuko wake wa mayai upande wa kushoto.
Akizungumzia kisababishi cha changamoto hiyo kwa wanawake, Dk Haidar anasema ni pamoja na uzito kupitiliza na kwa wasichana kuvunja ungo mapema ni miongoni mwa sababu zinazoweza kusababisha uvimbe kwenye mfuko wa mayai.
“Na hata uvutaji wa sigara au historia ya familia sambamba na vinasaba ni moja ya vyanzo vya uvimbe huo,” anasema Dk Haidar.
Anasema kitaalamu, hakuna sababu inayosababisha moja kwa moja hali hiyo, bali kuna visababishi vinavyoweza kufanya hali hiyo ikatokea, mfano uvutaji wa sigara kwa sababu kwenye sigara kuna visababishi vya saratani, hivyo huweza kuchangia.
Akizungumzia kuvunja ungo mapema, anasema huchangia yai kufanya kazi kwa muda mwingi ukilinganisha na anayechelewa kuvunja, hali inayoweza kuchochea uwapo wa uvimbe kwenye mfuko huo wa mayai.
Daktari huyo bingwa anashauri wanawake wawe na desturi ya kupima afya zao angalau mara moja kwa mwaka au miezi sita kwa sababu uvimbe huanza kukua taratibu.
“Watu walioko vijijini wanaweza kwenda hospitali kupima afya. Kutokana na maisha kuna jambo, mfano mtu aliye hatarini ni wale ambao wana watoto wachache au hawana kabisa watoto ndio wanaoweza kupata tatizo hili,” ameainisha Dk Haidar.
Anasema jambo la kuzingatia ni kuepuka kuvuta sigara, kuzingatia lishe, kufanya mazoezi na kupima afya mara kwa mara.
“Matatizo kama haya yanawapata wenye umri kuanzia miaka 40 na kuendelea na kwa wale waliochini ya umri huo mara nyingi siku za hedhi hubadilika,” anabainisha daktari huyo. Anasema dalili za mwanzo mara nyingi ni pamoja na tumbo kuuma kila mara na baadaye mgonjwa hushindwa kula chakula kutokana na mgandamizo ulioko tumboni, ukiwamo mfuko wa mkojo na utumbo.
Naye Elias Kweyamba, Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama kutoka Hospitali ya Misheni Ifakara, mkoani Morogoro anasema uvimbe kwenye mfuko wa mayai mara nyingi huanza na vivimbe vidogo vinavyojaa maji na hivyo huweza kumtokea mwanamke yeyote na vinaweza kupata maambukizi ya bakteria vikaathirika.
“Watu waliohatarini kupata uvimbe wa namna hii mara nyingi ni wale wenye umri mkubwa, mtu ambaye amezaa mara nyingi au amezaa mara chache,” anasema.
Na wakati mwingine anasema vinaweza kumsababishia mtu kupata saratani kwenye mfuko wa mayai.
“Uvimbe kwenye mfuko wa mayai unaweza kukua kwa kasi na ukubwa wowote kuanzia mdogo hadi mkubwa mfano wa kichwa cha mtoto,” anasema.