TMA watoa hofu wakulima Nyanda za Juu Kusini

Mbeya. Licha ya kuwepo kwa upungufu wa mvua katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi, Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imetoa tahadhari kwa wananchi waishio mabondeni kuhusu kuwepo kwa vipindi vifupi vya mvua kubwa.

Tahadhari hiyo imetolewa leo Ijumaa Januari 10, 2025 na Meneja wa TMA Kanda, Elius Lipiki wakati akizungumza na Mwananchi kuhusiana na kusuasua kwa mvua katika msimu huu hali iliyojenga hofu kwa wakulima.

Lipiki amesema utabiri wa hali ya hewa kwa msimu huu, unaonyesha mvua zilitarajiwa kunyesha wiki ya tatu ya Desemba 2024, lakini kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini zilianza kunyesha mwishoni mwa Desemba na kuendelea hadi Mei 2024 ambazo zitakuwa za wastani na chini ya wastani.

“Kwa mikoa ya kaskazini na magharibi hususani Mbeya kwa Wilaya ya Chunya, Iringa, Rukwa utabiri unaonyesha kutakua na mvua za wastani hadi juu ya wastani na kuwepo kwa vipindi virefu vya jua,” amesema.

Amesema utabiri huo hauzuii kuwepo kwa vipindi vifupi vya mvua kubwa ambazo zinaweza kuleta athari, hivyo tunawataka wafanyabiashara na wananchi wanaoishi mabondeni kuchukua tahadhari mapema kabla ya madhara kujitokeza,” amesema.

Lipiki amesema kwa msimu wa mwaka 2024, utabiri unaonyesha licha ya kuwepo kwa vipindi vifupi vya mvua kubwa, kutakuwa na vipindi vifupi vya jua ambavyo havitaleta athari katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

“Unajua hata uzalishaji wa mazao mara nyingi hayahitaji mvua nyingi wala jua kali sana, tunawataka wakulima kutumia msimu huu vizuri katika uzalishaji na kutokuwa na hofu,” amesema.

Wakati huohuo, Lipiki ametoa wito kwa wadau wa maendeleo kutumia msimu huu kama fursa ya kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi kufuatia kuwepo kwa vipindi vya jua na mvua za wastani.

“Msimu wa mwaka 2023, mvua zilikuwa nyingi na kukwamisha shughuli mbalimbali sambamba na ongezeko la maji katika mwambao mwa Ziwa Nyasa, Wilaya ya Kyela na kufanya uharibifu,” amesema.

Awali, wakulima wa mazao ya chakula na biashara waliingiwa na hofu ya kupungua kwa uzalishaji kufuatia uchache wa mvua maeneo mbalimbali.

Tausi John, mkulima wa Songwe, Wilaya ya Mbeya amesema uchache wa mvua umesababisha majani ya mazao yaliyopandwa hususan maharage na mahindi kukauka.

“Tumeingiwa na hofu katika uzalishaji msimu huu, mvua zinanyesha kwa manati na kusababisha mbolea iliyoungwa kukauka mashambani na mimea kuungua,” amesema.

Naye mkulima wa Kijiji cha Iwindi, Joel Issa amesema kimsingi kwa msimu huu wa kilimo  hawana matumaini ya uzalishaji kufuatia uchache wa mvua na vipindi vya jua kali tofauti na msimu wa mwaka jana.

“Tunaomba wataalamu wa kilimo kutoa elimu kwa wakulima namna ya kukabiliana na hali hiyo ili kutuondoa hofu na kutoa elimu ya mazao yanayo stahimili mvua chache,” amesema.

Related Posts