Mwanza. Wanaume wawili wanaosadikiwa kuwa majambazi wenye silaha wameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, baada ya kudaiwa kujaribu kutekeleza tukio la ujambazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Januari 10, 2025 amesema wanaume hao ambao walivaa magauni na vilemba kuficha utambulisho wao, wameuawa usiku wa kuamkia leo.
Amesema wakiwa wanne walifika yalipo makazi ya mfanyabiashara, Flora Abdallah (42) yaliyopo Mtaa wa Kabambo, Kata ya Kiseke wilayani Ilemela, mkoani Mwanza kisha kujaribu kuingia ndani kwa ajili ya kupora fedha.
“Wanaume hao walikuwa wamevaa magauni na vilemba ili wasibainike kwa urahisi. Kwa hiyo, alipofunguliwa geti tu akiwa ndani ya gari lake, ghafla waliingia getini ndipo mfanyabiashara huyo alipokimbilia ndani,” amesema.
Mutafungwa amesema msako wa kuwakamata wawili waliotoroka unaendelea, akisema anaamini makachero waliosambazwa mtaani watawatia mbaroni.
“Wengine waliokuwa nje (majina hayajatambulika) walipobaini kuwa maofisa wetu wameshafika eneo la tukio waliwasha pikipiki yao na kutokomea kusikojulikana,” amesema.
Akizungumza nyumbani kwake Mtaa wa Kabambo, mfanyabiashara Flora amesema watu hao walianza kumfuatilia tangu usiku wa kuamkia Jumapili Januari 5, 2025.
Amesema wanaume hao walianza kufuatilia mwenendo wake kuanzia alipotoka kwenda dukani kwake na kurudi nyumbani usiku jambo analodai alilibaini kupitia kioo cha gari lake.
“Jumapili (Januari 5,2025) niliwapita hapo nje ya nyumba wakiwa wamekaa kwenye msingi wa nyumba ya jirani yangu, walipoona nimeingia wakajaribu kuja hapa nyumbani kwangu wakashindwa lakini niliwaona kwenye kamera za CCTV,” amesema.
Flora anasema baada ya kubaini dalili za kufanyika uhalifu huo, alitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambao waliahidi kulishughulikia bila kumweleza hatua gani zitachukuliwa.
“Jumapili sikwenda dukani kwangu kwa sababu nilikuwa nimeshaogopa. Jumatatu nilikwenda, lakini wakati narudi kwenye kona nikawakuta tena wamekaa kwenye msingi hapo nje.
“Nilipowaona wapo hapo sikufungua geti badala yake nikanyoosha gari hadi kwa jirani yangu ambaye alinisindikiza mpaka ndani. Baada ya hapo nikaanza kuwa na wasiwasi,” amesema.
Kuhusu kuingia ndani, Flora amesema akiwa ndani ya gari akitoka mjini jana (Alhamisi Januari 9) alipofika Mtaa wa Kemondo alibaini kufuatiliwa na pikipiki mbili ndipo alipompigia Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) kumtaarifu kuhusu suala hilo.
“Nilipompigia RCO aliniambia nibadilishe uelekeo, basi nikageuza badala ya kwenda Kiseke nikarudi kama naenda Nyakato, nilipogeuza gari bado waliendelea kunifuatilia nikampigia kuwa wanaendelea kunifuatilia.
“Nilipompigia akaniambia basi wewe nenda polepole tunatuma askari wetu, sasa waliponifuatilia hadi nilipokaribia nyumbani bado naona watu wako nyuma yangu. Sasa ule muda askari kumbe walikuwa wameshaingia ndani,” amesema.
Amesema baada ya kukaribia nyumbani kwake, alimpigia msaidizi wa kazi za ndani amfungulie geti haraka kisha akaendesha gari kwa kasi hadi ndani ya uzio wa nyumba yake.
Huku akiwa na hofu, Flora anasema alipofanikiwa kuingia ndani ya geti alichomoka mbio kutoka kwenye gari hadi ndani ya nyumba, huku wengine wawili (washukiwa wa ujambazi) wakiingia ndani kwa kuruka uzio ndipo walipokabiliana na maofisa wa polisi.
“Nilikuwa siamini kama kuna askari, kwa hiyo mmoja alinikimbiza mpaka ndani ndipo nikasikia milio ya risasi baadaye nikabaini kuwa waliokuwa wameingia ndani wamepigwa risasi wote,” amesema.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Getruda Kaolela amesema alisikia milio ya risasi saa 2:30 usiku (Januari 9) ndipo aliposogea na kukuta tayari maofisa wa polisi wameshawaua watu hao ndani ya nyumba hiyo.
“Nilisikia vitu kama vinalipuka baadaye nikasikia tena milio nikatoka nje kutembea kwa mguu kidogo sikuona chochote, baadaye askari polisi wakatanda hadi huku kwetu wakirusha risasi, wakiuliza nani amepita eneo letu kwa wakati huo,” ameeleza.
Kamanda Mutafungwa, amewataka wananchi kufunga teknolojia ya kamera za CCTV kwenye makazi na maeneo ya biashara zao kukabiliana na vitendo vya uhalifu, akidai jitihada zinazofanywa na jeshi hilo huenda zisifanikiwe kwa asilimia 100 kukomesha vitendo hivyo.
Amesema hata CCTV zisipofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa wa uhalifu jijini humo, zitawasaidia maofisa wa uchunguzi kuwabaini watekelezaji wa vitendo vya kihalifu.
“Tumekuwa tukihimiza wananchi kufunga kamera za CCTV kwenye biashara na makazi yao japo mwitikio siyo mkubwa (bila kutaja idadi), kwa sababu wengi wanasingizia gharama,” amesema.
Katika hatua nyingine, Kamanda Mutafungwa amewataka wananchi kutoa taarifa Polisi wanapobaini dalili za uwepo wa tukio la kihalifu katika maeneo yao, ili kuokoa kabla halijaleta madhara.