Wakulima Njombe walia uhaba mbegu za viazi mviringo

Njombe. Wakulima wa viazi mviringo mkoani hapa, wameiomba Serikali kuongeza wigo wa upatikanaji wa mbegu za zao hilo ili kukabiliana na uhaba wa mbegu hizo unaowafanya washindwe kuzalisha viazi kwa wingi.

Wakulima wametoa ombi hilo leo Januari 10, 2025 mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka ambaye alitembelea shamba la mkulima mmoja wa viazi, lililopo Mtwango, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe mkoani hapa.

Wamesema licha ya kuwa mbegu za viazi zinauzwa gharama kubwa lakini bado upatikanaji wake ni mgumu kwani kiwango kinachozalishwa kiwandani, bado hakikidhi mahitaji ya wakulima waliopo kwenye vikundi na hata mmojammoja.

Wamesema wapo wakulima ambao wamekuwa na utaratibu wa kulima zaidi ya ekari moja ya viazi mviringo, lakini kutokana na uhaba wa mbegu mwaka huu wamelazimika kupanda ekari moja pekee.

Wamesema mbegu wanayotumia wakulima wengi mkoani humo ni aina ya Sagita ambayo mzalishaji wake ni mmoja, Silverland na anahudumia nchi zaidi ya moja, hivyo wanapata wakati mgumu pindi wanapohitaji kiasi kikubwa cha mbegu na kupata kidogo.

Mkulima wa viazi Njombe, Lenard Kadali amesema msimu wa mwaka jana katika ekari moja ya viazi alipata gunia 136 na kuuza Sh65,000 kwa gunia moja.

“Changamoto kwa sisi bado inabaki ni mbegu uhitaji wa sisi wanachama pamoja na wakulima wetu ni kulima zaidi ya hapa, sasa ili kila mtu apate wanagawana zinazopatikana,” amesema Kadali.

Naye Gladness Charles amesema hii ni mara yake ya pili kulima viazi mviringo ambapo msimu wake wa kwanza alipata gunia  148 kwa ekari moja na kuuza Sh75,000 kwa gunia.

“Mwaka jana nililima ekari mbili, mwaka huu imebidi nilime ekari moja kutokana na changamoto ya mbegu, ni chache na wakulima wapo wengi,” amesema Charles.

Mwenyekiti wa chama cha msingi cha Ushirika cha Isowelo Amcos, Elia Mhonjwa amesema chama hicho kina wanachama 630 wanaojishughulisha na kilimo cha viazi mviringo ambapo eneo waliloomba mwaka huu kwa mahitaji ya wanachama ni ekari 1,279, ambapo waliomba mbegu tani 700 lakini walijibiwa kuwa watapata tani 400.

“Mbegu ya viazi kwa ekari moja bila ya gharama ya usafiri ni Sh1.3 milioni lakini mpaka inafika chamani kuwagawia wakulima inafika Sh1.37 milioni. Chama kinachukua asilimia kidogo ya ushuru kama Sh30,000, hivyo inafanya ifike Sh1.4 milioni,” amesema Mhonjwa.

Ofisa Kilimo Mkoa wa Njombe, Wilson Joel amesema mahitaji ya mbegu za viazi mviringo mkoani humo ni tani 130,000 lakini kiasi kinachopatikana ni tani 400.

“Idadi hiyo ni zile mbegu bora lakini wapo wakulima wanatumia hizi mbegu za shambani zinazotokana na viazi walivyolima hasa wa huko Makete,” amesema Joel.

Mrajisi wa Mkoa wa Njombe, Edmund Massawe amesema uhaba wa mbegu unatokana na aina ya mbegu ya Sagita kuwa na mwamko mkubwa kwa wakulima hao, kwa kuwa imekuwa ikiwapatia faida kubwa pindi wanapoitumia.

“Ukifuatilia hawa Silverland walianza na Isowelo kama mteja wake mkubwa na alikuwa amewalenga wao na msimu huu wameomba tani 700, lakini msambazaji huyo kwa sasa anapeleka mbegu maeneo mengine kama Moshi, Arusha, Iringa Mbeya kwa hiyo yeye anaangalia kutanua soko lake,” amesema Massawe.

Mtaka amesema ipo haja ya kuhamasisha watu wengi kuja kuzalisha mbegu ya viazi mviringo kwa kuwa nchi ina wataalamu wa kilimo wa kutosha.

“Nchi nzima mzalishaji wa mbegu ya viazi mviringo ni mmoja kwa hiyo siku akiamka akakwambia amepoteza hamasa ya kuzalisha mbegu Tanzania maana yake tumekufa,” amesema Mtaka.

Related Posts