Wanolewa kuondokana na kilimo cha mazoea Zanzibar

Unguja. Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, imesema itaendelea kuunga mkono jitihada za washirika wa maendeleo kuwasaidia wakulima ili wapate tija.

Mratibu wa Mradi wa Uhimilivu wa Mifumo ya Chakula, Sihaba Haji Vuai amesema hayo leo Januari 10, 2025 alipofungua mafunzo ya mabibi na mabwana shamba, maofisa kilimo na ushirika, Unguja.

Amesema mafunzo hayo yanalenga kuimarisha ujuzi kwa washiriki ili kuimarisha kilimo nchini kutokana na wakulima wengi wanaozalisha mazao kukosa masoko ya uhakika.

“Tutaendelea kuunga mkono jitihada za washirika wa maendeleo, mafunzo haya yataimarisha na kuleta tija katika kilimo cha kisasa,” amesema.

Sihaba amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo katika usimamizi wa kina mama na vijana waliojiunga katika ushirika kwa ajili ya kuzalisha au kuuza mazao ya mbogamboga na kukuza vipato vyao.

Amewataka washiriki  kuyafanyia kazi mafunzo watakayopewa kwa vile yatawaelekeza na kuyawezesha makundi hayo juu ya njia za kutafuta na kupata masoko wakati wa uzalishaji wa mazao yao na waweze kuyafikia masoko kwa urahisi.

Awali, Ofisa Kiungo Elimu kwa wakulima wa mradi huo, Saada Seif Said amesema wakulima wa Zanzibar wamezoea kulima mazao ya mbogamboga bila kufuata taratibu za kilimo, hivyo kutolewa kwa elimu kutasaidia wakulima kuondokana na kilimo cha mazoea.

Ofisa Ushirika kutoka Idara ya Maendeleo ya Ushirika, Abdulmajid Masoud Khalfan, akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake amesema mafunzo hayo yatawawezesha kutambua namna ya kuzalisha bidhaa na utafutaji wa masoko.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanashirikisha mabibi na mabwana shamba 26, yameandaliwa na Mradi wa Uhimilivu wa Mifumo ya Chakula Tanzania Zanzibar unaotekelezwa kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2023 na unatarajiwa kumaliza mwaka 2028 kwa gharama ya Dola za 15 milioni za Marekani.

Mradi huo pamoja na mambo mengine, unalenga kuwajengea uwezo mabibi na mabwana shamba na maofisa ushirika katika kuwasimamia wakulima hasa kina mama na vijana kuzalisha bidhaa bora na kupata masoko ya mazao ya mbogamboga.

Related Posts