Dar es Salaam. Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amesema tayari wameshaandaa miongozo itakayotoa elimu ya fedha kwa Watanzania itakayofundishwa kuanzia shuleni.
Amesema hatua hiyo inalenga kumpa Mtanzania elimu ya kumwongoza kwenye matumizi ya fedha ili kuepuka utumiaji usiofaa unaosababisha umasikini.
Tutuba ametoa kauli hiyo kwenye hafla ya kuorodheshwa kwa Hisa Stahiki za Benki ya DCB kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), leo Ijumaa Januari 10, 2025 makao makuu ya DSE jijini Dar es Salaam.
“Mtu akipata fedha anawaza atazitumiaje na kuna wakati anakosa hadi usingizi hadi pale atakapozitumia ziishe. Umasikini mwingine unatokana na namna isiyofaa ya matumizi ya fedha kwa baadhi yetu,” amesema.
Katika hilo amesema wananchi wanapaswa kuwa na tabia ya kujiwekea akiba zitakazowasaidia katika kipindi kigumu.
“Changamoto ya elimu ya fedha imefanya tumetengeneza miongozo miwili. Wa kwanza, unahusu shule na umeshachukuliwa na Wizara ya Elimu wanaitafsiri tayari kufundishwa kuanzia ngazi ya shule za msingi,” amesema.
Mwongozo wa pili, amesema ni wa nje ya mitalaa ya shule na yote ipo kwenye tovuti ya BoT. Amesema mtu akipata pesa anaweza kuitumia kama mtaji kwa ajili ya manufaa yake.
Akizungumzia hatua ya kuuzwa hisa za DCB amesema ni habari njema kwani utoaji wa hisa stahiki uliofanikiwa na kupata mwitikio kutoka kwa wanahisa umeonyesha imani ambayo wawekezaji wanayo.
“Ninafurahi kuona kwamba kupitia mauzo ya Hisa Stahiki, DCB imefanikiwa kuongeza mtaji wake kutoka Sh15 bilioni hadi kufikia Sh25.7 bilioni.”
“Mnapoanza kutekeleza mpango mkakati wenu wa miaka mitano (2024-2028), nawahimiza kuendelea kushikilia misingi ya ubunifu, kujali wateja na kuzingatia sheria. Kanuni hizi ni msingi wa ukuaji endelevu na zitawawezesha kuendelea kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Taifa letu,” ameagiza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DCB, Sabasaba Moshingi amesema uuzaji wa Hisa Stahiki za benki ulifikia tamati Desemba 6, 2024 kwa mafanikio ya asilimia 100.
“Benki yetu imefanikiwa kuuza Hisa Stahiki zenye thamani ya Sh10.74 bilioni kwa wanahisa wa benki yetu,” amesema.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Tanzania (CMSA), Nicodemus Mkama amesema masoko ya mitaji na dhamana yanatoa fursa katika kuchochea maendeleo ya nchi.
“Natoa wito kwa benki zingine kutumia fursa zilizopo kwenye masoko ya mitaji kwa kuwa yanatoa mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya sekta ya uchumi na fedha.
“Natoa rai kwa benki ya DCB watambue walionunua hisa hizo wamewapatia jukumu kuhakikisha kunakuwa na ongezeko la thamani la uwekezaji wao ili wanufaike kiuchumi, ikiwemo kupatiwa gawio,” amesema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi DCB, Zawadia Nanyaro amesema matokeo baada ya uuzaji wa Hisa Stahiki yanaenda kuwaletea wanahisa na Watanzania kwa ujumla tija za kiuchumi.
“Baada ya kuongeza mtaji, benki yetu inalenga kukuza biashara na kuwapatia wafanyabiashara wadogo na wa kati mitaji ya kukuza biashara zao. Pia, tutaimarisha uwezo wa kutoa mikopo hiyo hususani kwa makundi maalumu, wakiwemo wanawake,” amesema.