Jamii yahimizwa kuomba mikopo kukuza biashara

Unguja. Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Shaib Hassan Kaduara amewataka wajasiriamali wa Soko la Kinyasini, Mkoa wa Kaskazini Unguja kujiunga na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kuomba mikopo ili kuendeleza biashara zao.

Amesema hayo katika ufunguzi wa tawi la PBZ leo Ijumaa Januari 10, 2025, Kinyasini, Kaskazini Unguja.

“Biashara yoyote inahitaji mtaji, hivyo wajasiriamali wa soko hili waitumie fursa hii kwa kuomba mikopo ili kukuza biashara,” amesema.

Amesema uwepo wa tawi hilo katika soko itawarahisishia wananchi kufanya huduma za Serikali bila kwenda mjini kama ilivyokuwa awali.

“Tawi hili la PBZ lipo kwa ajili ya wafanyabiashara wa soko hili na wananchi ambao wanahitaji kufanya malipo ya Serikali, kulipia umeme na kufanya miamala, hili litawarahisishia wao kupata huduma hizo,” amesema.

Hata hivyo, amewataka wananchi wa eneo hilo kulitumia vizuri tawi hilo kwani lengo lake ni kupatiwa suluhisho la kifedha kwa kufungua akaunti, kuweka na kutoa pesa na malipo ya Serikali.

Ametoa wito kwa wamiliki wa hoteli, wafanyabiashara na wajasiriamali kuiunga mkono benki hiyo na ikitokea changamoto wasisite kuziwasilisha ili zitafutiwe ufumbuzi.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Juma Makungu Juma amesema mambo ya kuhifadhi pesa katika vibubu yalishapitwa na wakati, hivyo sasa watumie fursa hiyo kuweka akiba benki.

“Wananchi tunapaswa kuondoa dhana ya kuwa watu wenye pesa nyingi ndio ambao wanaweka fedha hizo benki ila kwa wale ambao wana fedha kidogo waweke katika vibubu hilo siyo jambo zuri, ikitokea ajali ya moto akiba yote inateketea,” amesema.

Amewaasa wananchi kuwa makini na mitandao ya simu na wasiwe tayari kutoa namba za siri kiholela.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa PBZ, Arafat Haji amesema benki hiyo inakua kwa kasi hadi kufikia sasa ina matawi 44, ambayo 29 yapo Zanzibar na Tanzania Bara yapo 17 na mawakala 1,500.

Amesema benki hiyo inafanya vizuri na kufikia rasilimali ya jumla Sh2.4 trilioni akieleza ni ya sita inayofanya vizuri kwa upande wa faida.

Related Posts

en English sw Swahili