Gavana wa Benki Kuu aipongeza Benki ya DCB kwa kuongeza mtaji wake.

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba ameipongeza Benki ya Biashara ya DCB kwa kuongeza mtaji wake kutoka shs bilioni 15 hadi shs bilioni 25.74 kwa kupitia zoezi ya uuzaji wa Hisa Stahiki lililofanyika hivi karibuni.

 

Pongezi hizo alizitoa jijini Dar es Salaam leo, katika hafla ya kuorodheshwa hisa hizo katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), ambapo alisema mafanikio ya zoezi hilo sio tu kwa manufaa ya Benki ya DCB pekee bali pia ni kwa sekta nzima ya fedha ikionesha maono, uvumilivu, na nia thabiti ya uongozi wa benki, masoko ya mitaji, wanahisa, na wadau wake, ambao wameendelea kuamini katika uwezo wa benki hii na mchango wake katika mageuzi ya uchumi wa taifa.

 

“Umuhimu wa masoko ya mitaji katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi hauwezi kupuuzwa, kwa kutoa jukwaa la kukusanya mtaji wa muda mrefu, masoko haya huwezesha biashara kupanuka, kuleta ubunifu, na kuchangia katika uundaji wa ajira, mafanikio ya DCB yanadhihirisha nguvu ya masoko haya katika kukuza na kuimarisha uchumi wa nchi yetu.

 

“Utoaji wa Hisa Stahiki za Benki ya DCB uliofanikiwa na kupata mwitikio mkubwa kutoka kwa wanahisa umeonyesha imani ambayo wawekezaji wanayo kwa maono ya benki hii na safari yake ya mabadiliko, ninafurahi kuona kwamba kupitia zoezi hili la mauzo ya Hisa Stahiki, DCB imefanikiwa kuongeza mtaji wake kutoka TZS bilioni 15 hadi kufikia TZS bilioni 25.7”, alisema Gavana Tutuba.

 

Pamoja na hayo alitoa kongole kwa hatua ambazo DCB imechukua akisema zinaendana na vipaumbele vya maendeleo ya kitaifa, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono wanawake wajasiriamali, wafanyabiashara wa masokoni, na makundi maalum kupitia bidhaa bunifu za mikopo kama huduma ya mkopo wa wanawake “Tausi,” mikopo ya Bodaboda na Bajaji, na Mikopo ya Sokoni.

 

“Naipongeza Bodi, Menejimenti, wanahisa, na wadau wa Benki ya DCB kwa kujitolea kwao bila kuchoka katika jitihada hizi, pia natambua mchango wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), na iTrust Finance Ltd kwa mwongozo na usimamizi wao uliowezesha mafanikio ya zoezi hili.

 

“Benki Kuu ya Tanzania imejitolea kuunda mazingira wezeshi kwa taasisi za kifedha kustawi huku ikihakikisha uthabiti na uadilifu wa mfumo wa fedha ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi dhabiti wa Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan, mafanikio ya leo ya DCB ni ushahidi wa kile kinachoweza kufikiwa wakati vyombo vya udhibiti, taasisi za kifedha, na wadau wanaposhirikiana kufanikisha malengo ya pamoja”, aliongeza gavana huyo.

 

Awali akizungumza mahali hapo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya DCB, Bi. Zawadia Nanyaro alisema suala la kuongeza mtaji wa benki yao linatokana na sheria na kanuni za Benki Kuu zinazotaka mabenki ya kibiashara kuwa na mtaji wa angalau shs bilioni 15, hivyo ili kuweza kufanya biashara kwa ufanisi zaidi, Bodi

na Menejimenti ya benki iliweka mpango mkakati wa miaka mitano (2024-2028) ambao ulitoa

kipaumbele kwenye suala zima la mtaji ikiwa na lengo la kukuza mtaji kutoka bilioni Tsh 15

(2024) hadi kufikia shilingi bilioni 61 ifikapo mwaka 2028.

 

 

“Tunatambua ili taasisi ya kifedha iweze kusimama imara, suala la

ongezeko la mtaji ni jambo muhimu hivyo kwa muktadha huo tulizindua zoezi la uuzaji wa Hisa

Stahiki mnamo Novemba 11, 2024, tukiwa na malengo ya kuongeza mtaji wa kiasi cha

shs bilioni 10.74, ninayo furaha kubwa leo hii kutangaza kuwa zoezi hili lilifungwa

rasmi Disemba 6, 2024 na limefanyika kwa mafanikio makubwa na kukamilisha malengo yetu

kwa asilimia 100, hivyo kutimiza azma yetu ya kukuza mtaji wetu kutoka shs Bilioni 15 tuliokuwa

nao hadi shs bilioni 25.7 kwa sasa.

 

“Benki ya DCB tutaendelea kufanya biashara kwa kuzingatia vigezo, kanuni na miongozo yote inayotolewa na mamlaka za serikali ili kuendeleza uchumi wa nchi yetu kwa masilahi mapana ya wanahisa wetu, wadau, wateja na watanzania kwa ujumla”, alisema Bi. Zawadia.

 

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Sabasaba Moshingi alisema, ongezeko la mtaji linatarajia kuleta matokeo mazuri zaidi yatayoleta tija kwa wanahisa wake, wadau na watanzania kwa ujumla, mtaji ukitumika kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo wadogo, kutoa mikopo kwa makundi maalumu

kama wanawake, bodaboda, masokoni, walimu na wafanyakazi, kuboresha pia huduma za kibenki kwa njia ya kidigitali ili ziendane na wakati hivyo kukidhi mahitaji ya watanzania wenye kiu ya kupata huduma bora, za kifedha kwa urahisi na kwa gharama nafuu.

 

“Historia yetu inaonesha kwamba, mtaji wa kwanza wa benki wa shs bilioni 1.7 ulipatikana kutoka Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kuhimizwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2001 hayati Mhe.

Benjamin Mkapa, ambapo benki yetu ilipata kibali cha kuendesha benki ya jamii (community bank)

kutoka Benki Kuu mwaka 2002, ikifahamika kama benki ya wananchi. Mtaji wa benki

uliendelea kuongezeka kupitia wanahisa waanzilishi na baadae wanahisa wengine waliwekeza

katika benki kupitia masoko ya mitaji na hatimaye kuorodheshwa katika soko la hisa ikiwa ni benki ya kwanza  kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es

Salaam (DSE), mnamo mwaka 2008.

 

 

“Kama sehemu ya mkakati wetu wa kuiandika upya historia ya benki yetu kupitia uongozi bora wa bodi na menejimenti na wafanyakazi mahiri, benki imeweza kutoka katika hasara na kupata faida ya shs milioni 317 kabla ya kodi mwaka 2024. Mikopo tuliyotoa imekua kutoka shs milioni 126 katika robo ya kwanza hadi shs milioni 136 katika robo ya nne. Amana za wateja zimeongezeka kutoka shs

bilioni 142 katika robo ya kwanza hadi shs bilioni 152 katika robo ya nne ya mwaka na kwa upande wa mikopo chechefu tumeweza kupunguza kasi kutoka shs bilioni 6.9 katika robo ya kwanza hadi shs bilioni 4.7 katika robo ya nne ya mwaka.

 

 

Hata hivyo alisema changamoto moja waliyonayo ni kuwa na dhamana nyingi zenye riba

Kubwa hivyo kusababisha benki kushindwa kupata faida kubwa ambapo awali baada ya kuanzishwa

benki, msaada mkubwa wa biashara na dhamana ulipatikana kutoka kwa wanahisa

waanzilishi kwa kufungua na kupitisha fedha kwenye akaunti za makusanyo, mikopo ya asilimia

kumi na akaunti za maendeleo, huku wanahisa wengine waliisaidia benki kwa kufanya biashara

na benki.

 

“Natoa shukurani kubwa kwa wanahisa wetu walioshiriki katika mauzo ya Hisa Stahiki, niwaombe sana muendelee kuisaidia benki yetu katika kufanya biashara na

benki na kuleta dhamana katika benki yetu, tunaamini tukifanya hivyo benki itapata faida

kubwa, mtaji wa benki utaongezeka, pato la wanahisa litaongezeka,  hivyo kuendelea kusukuma mbele ajenda ya Rais wetu shupavu, Mhe. Mama Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea wananchi maendeleo kupitia huduma za kifedha huku tukihakikisha huduma hizi zinawafikia watu wengi na kwa urahisi.

 

 

“Pia nitoe shukurani za pekee kwa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kwa miongozo ambayo imewezesha kupata mafanikio katika mauzo ya Hisa Stahiki na kuwezesha kuorodhesha hisa hizi leo katika Soko la Hisa, aidha, napenda kutoa shukrani za

dhati kwa kampuni ya iTrust Finance Limited ambao ni washauri kiongozi katika zoezi zima la

uuzaji wa hisa wakiwa na timu ya wanasheria kutoka Endoxa na wahasibu kutoka Auditax, na kwa wanahisa wetu wote wakiwemo Halmashauri ya Jiji la  Dar es Salaam, Halmashauri za Manispaa za Ilala, Ubungo, Kinondoni, Temeke na Kigamoni, UTT, NHIF na wengineo”, alisema Bw. Moshingi.

 

Akizungumza katika hafla hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Bw. Peter Nalitolela alitoa rai kwa watanzania kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana katika masoko ya mitaji huku Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bwana Nicodemus Mukama akisema mazingira wezeshi na shirikishi yaliyowekwa  na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ndio yaliyosababisha asilimia 100 ya waliojitokeza kununua hisa za DCB kuwa  watanzania binafsi na taasisi za kitanzania.Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba akizungumza wakati wa hafla ya kuorodheshwa Hisa Stahiki za Benki ya Biashara ya DCB kwenye soko Hisa la Dar es Salaam (DSE) leo.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba ( wa tatu kushoto) akigonga kengele kuashiria  kuorodheshwa kwa Hisa Stahiki za Benki ya Biashara ya DCB kwenye soko Hisa la Dar es Salaam (DSE) jijini Dar es Salaam leo. Zoezi la uuzwaji wa Hisa Stahiki 97,646,913 zenye thamani ya shilingi 10,741,160,430 lilizinduliwa Novemba 11, 2024 na kukamilika Disemba 6 mwaka huo kwa mafanikio ya asilimia 100. Wengine Kutoka kushoto ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Itrust Finance, Bw. Faiz Arab, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa DCB, Bi. Zawadia Nanyaro, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Sabasaba Moshingi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE , Bw. Peter Nalitolela.

Related Posts