Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack amekutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Norway Mhe.Andrea Motzfeldt Kravik na ujumbe wake akiwemo Balozi wa Norway Nchini Tanzania Mhe.Toni Tinnes pamoja na Equinor na Shell na wasimamizi wa mradi huo TPDC leo Januari 10,2025.
Telack amemueleza Naibu Waziri huyo wa Mambo ya nje wa Norway Kravik namna ambavyo maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa kuchakata na kusindika Gesi asili (LNG) yalivyofanyika ikiwemo kulipa fidia wananchi wote ambao walikuwa na miliki ya maeneo hayo na uandaaji wa michoro ya utekelezaji wa mradi huo.
Kwa upande wake Naibu waziri wa Mambo ya Nje ya Norway Adreas Kravik amepongeza hatua ambayo Serikali ya Tanzania imefikia katika mradi huo ambapo mbali na kuona na kujiridhisha juu ya eneo utakapotekelezwa amewahakikishia wanakwenda kujiandaa na kushawishi kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo Mkubwa nchini Tanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Telack aliongozana ugeni huo hadi katika eneo la Likong’o Manispaa ya Lindi ambako utekelezaji wa mradi wa uchakataji wa gesi asilia LNG unatarajiwa kufanyika utakaogharimu dola za Marekani Bilioni 42 sawa na Trilioni 90 za Kitanzania .
Baadhi ya manufaa yanayotajwa katika mradi huo ni kuchochea ukuaji wa uchumi, kuiongezea Serikali Mapato, kuongeza ajira na kuongeza uwezo wa Watanzania kitaaluma.
Aidha kati ya miaka minne hadi sita ya ujenzi wa mradi huu unatarajiwa kuwa na ajira wastani wa10,000 na baada ya kukamilika kwa ujenzi, ajira za kudumu zinakadiriwa kuwa 500.