Songea. Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma linawashikilia wenza wakazi wa Mjimwema kwa fupi Manispaa ya Songea, kwa tuhuma za kuiba mtoto mwenye umri wa miezi 11.
Jeshi hilo pia linawatafuta wanawake wengine wawili ambao wanadaiwa walishiriki kuiba mtoto huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 10, 2025 ofisini kwake amesema kuwa tukio hilo limetokea Novemba 4, 2024 saa 8 mchana, ambapo Gabriela Hinju (24) mkazi wa Mjimwema Manispaa ya Songea, mfanyabiashara wa saloni alitoa taarifa katika Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Songea kuibiwa kwa mtoto wake aitwae Groly James.
Amesema mwanamke mmoja aliyemtambua kwa sura alifika saluni hapo kwa ajili ya kupata huduma ya kusukwa na kipindi yupo kwenye foleni mtoto wa msusi huyo alikuwa analia ndipo mwanamke huyo akaomba ambebe ili akambembeleze nje. Alipotoka nje kumbembeleza mtoto huyo akatokomea naye kusikojulikana.
Amesema baada ya tukio hilo walianza ufuatiliaji mkali kuhakikisha wanamsaka mtuhumiwa na mtoto huyo na leo wamefanikiwa kumpata mtoto Glory akiwa ndani ya chumba cha fundi cherehani, Janeth Nombo (25) mkazi wa Mjimwema Manispaa ya Songea.
“Mtuhumiwa amehojiwa na amekiri kumuiba mtoto huyo akishirikiana na wenzake wawili ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi na kwamba sababu ya kufanya kitendo hicho ni kuwa wameishi na mume wake kwa miaka saba bila kupata mtoto, ndipo akaamua kutekeleza azima hiyo ili amdanganye mume wake kuwa amejifungua,”amedai Kamanda Chilya
Aidha, Kamanda Chilya ametoa wito kwa wazazi na walezi mkoani hapa kuwalinda na kuwatunza watoto na si kuwakabidhi kwa watu wasiowafahamu, ili kuepuka matukio ya wizi wa watoto.
Kwa upande wake baba wa mtoto huyo, James Nyoni ameshukuru Jeshi la Polisi kwa ushirikiano mkubwa waliompatia pamoja na wananchi na kusaidia kupatikana kwa mwanaye akiwa na afya njema.
Naye mama mzazi wa mtoto huyo Gabriela Hinju ameeleza kufurahishwa na upatikanaji wa mwanaye.
Kwa upande wake Raymond Mbilinyi ambaye mume wa Janeth anayedaiwa kuiba mtoto, amesema alidanganywa na mkewe kuwa amejifungua mtoto njiti hivyo wazazi wanamsaidia kumtunza, kumbe alikuwa ameiba na kumficha hadi alipokamatwa na polisi kwa tuhuma hizo.