Dar es Salaam. Asasi za kiraia (Azaki) zimeitaka Serikali kuingiza mpango wa bima ya afya kwa wote kuwa sehemu ya matarajio katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Siyo kuingiza mpango huo pekee, zimetaka iwekwe wazi kuwa, bima ya afya kwa wote itakuwa nafuu, yenye tija na ufanisi kwa makundi ya watoto, wazee, wanawake, wanaume na watu wenye ulemavu.
Akizungumza katika mkutano wa Azaki kuhakiki rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Deus Kibamba ambaye ni mmoja wa wajumbe wa kikosi kazi kupitia Azaki amesema utekelezaji wa hilo utaiweka nchi katika orodha ya nchi zilizofanikiwa katika utoaji wa huduma hiyo duniani.
“Serikali ipo katika mkakati wa kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi wote kwa ufanisi zaidi, hivyo suala hili halitakiwi kusahaulika katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” amesema.
Novemba 2, 2023, Bunge lilipitisha muswada wa bima ya afya kwa wote, baada ya mkwamo uliokuwepo kwa takribani miaka mitano tangu ulipofufuliwa upya 2018. Desemba 4, 2023, Rais Samia Suluhu Hassan alitia saini muswada huo na kuufanya kuwa sheria kamili.
Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, Septemba 11, 2024 alipotembelea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili aliahidi kukamilisha mchakato wa bima ya afya kwa wote ambao sasa upo katika hatua ya kuandaa kanuni.
Alisema gharama kubwa za matibabu zinawakabili wananchi na bima ya afya kwa wote ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya.
Pamoja na suala la bima ya afya, uboreshaji wa huduma za uzazi, maisha bora kwa wananchi, elimu, ukuaji wa uchumi ni miongoni mwa vitu vilivyotawala katika mkutano wa utoaji wa maoni kwa upande wa Azaki.
Nuru Marwa, mjumbe wa kikosi kazi cha mapitio ya dira hiyo amesema miongoni mwa mapendekezo wanayotoa katika kamati hiyo ni pamoja na kutoshabihiana kwa maudhui na data kwenye chapisho la Kiswahili na Kiingereza.
Akitoa mfano katika aya 2.1 unaoeleza uchumi imara, jumuishi na shindani, aya ya kwanza kwenye utangulizi upo tofauti na chapisho la Kiingereza ambalo kasi ya kukua kwa uchumi ni asilimia 6.4 wakati ya Kiingereza ni asilimia 5-6.7.
Amesema Azaki zimependekeza kamati itumie taarifa na takwimu sahihi na za aina moja kwenye nyaraka zote mbili.
“Katika utawala na uongozi bora haujawekwa kama moja ya sekta za kimageuzi, hivyo tunapendekeza, liwe moja ya sekta za kimkakati, kwani ukitaka maendeleo unahitaji watu, ardhi, uongozi bora na siasa safi ili kufikia maendeleo tunayotarajia,” amesema.
Marwa amesema katika sekta ya elimu haijawekwa kama moja ya sekta za kimageuzi wakati dira hiyo inatarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha mapinduzi ya nne ya viwanda ambayo teknolojia inakua kwa kasi na ndiyo nyenzo kuu ya uzalishaji na tija katika nchi ambayo idadi kubwa ya watu wako chini ya umri wa miaka 15. Matumizi na uzalishaji wao wa kidijitali vinapaswa kuzingatiwa kupita makuzi yao ya kielimu.
Azaki inapendekeza sekta ya elimu kuwa ni moja ya sekta za kimapinduzi, ili utekelezaji wa dira uendane na wakati.
Akizungumzia makadirio ya idadi ya watu ifikapo 2050 kufikia milioni 140 haiendani na takwimu rasmi za Ofisi za Takwimu Taifa (NBS) ambayo inaelezea malengo ya maendeleo endelevu ya dunia, dira ya Afrika Mashariki 2050 na Dira ya SADC ambapo imetajwa ifikapo 2050 idadi ya watu Tanzania itakua imefikia milioni 151.3.
Amesema wanapendekeza takwimu hiyo ya makadirio ya idadi ya watu kufikia 151.3 itumiwe na dira. Pamoja na makadirio haya, ipo haja ya dira kuzingatia hali ya uzazi na ongezeko la watu ambayo imekua ikishuka kwa kasi kwa baadhi ya mikoa.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo amesema baada ya mchakato wa ukusanyaji wa maoni kukamilishwa, kinachofuata ni uchambuzi na utekelezaji wa maoni mbalimbali yaliyotolewa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Foundation For Civil Society (FCS), Justice Rutenge amesema dira hiyo ni nyenzo muhimu kwa upangaji wa pamoja wa ndoto za Watanzania kama Taifa.