Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitangaza zaidi ya mifumo 300 kufanya kazi kwa kusomana, wajumbe wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) wametaka mchakato wa utoaji namba jamii kwa Watanzania kuharakishwa.
Hiyo imetajwa kuwa moja ya njia itakayosaidia kusomana kwa mifumo hiyo kuwa na faida katika ukuaji wa uchumi na kuongeza uwazi zaidi.
Jamii namba ni namba ya utambulisho wa mtu kwenye mitandao yote ya kidijitali, huku ndani yake ikiwa na mfumo wa kumwezesha mtu kuunganishwa na huduma mbalimbali ikiwemo akaunti za kibenki zitakazomuwezesha kufanya shughuli mbalimbali.
Hii inakwenda hadi kwa kampuni za kibiashara ambazo zitawezesha watu kufikia taarifa za kampuni.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo Ijumaa, Januari 10, 2025 baada ya mkutano wa sekretarieti ya TNBC, wajumbe wamesema jamii namba ni moja ya njia itakayoongeza utendaji si ndani ya Serikali pekee bali hadi sekta binafsi.
Rais wa Chemba ya Biashara, Kilimo na Viwanda Tanzania (TCCIA), Vincent Minja amesema kuunganishaji wa mifumo ni vyema kwenda sambamba na uwepo wa namba moja kwa kila Mtanzania ambayo itasaidia pia sekta binafsi kupata urahisi wa kuwatambua watu wote.
“Hii itasaidia hata kama mtu amefanya kazi hapa ameharibu, akienda sehemu nyingine unaweza kujua huyu mtu alikuwa anafanya kazi sehemu fulani. Sasa hivi ni ngumu, mtu anafanya kazi mlango huu, anakwenda sehemu nyingine anasema hajawahi kufanya kazi sehemu yoyote na hawajui kama huyu mtu ni mwizi,” amesema.
Amesema kitambulisho cha Taifa, ambacho kina taarifa nyingi za mtu, bado kinaacha kundi kubwa la watu bila utambuzi, kwani hutolewa kwa watu wenye miaka 18 na kuendelea.
Amesema mfumo wa NIDA huwafanya watu wanaojishughulisha na vitu mbalimbali vya kujiingizia kipato kuwa ngumu kutambuliwa.
Amesema kupitia namba jamii, wigo wa walipakodi utaongezeka na kupunguza mzigo wa kodi kwa watu wachache kama ilivyo sasa.
Kwa mara ya kwanza, Aprili 2024, Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza kuwapo kwa namba moja ya utambulisho kwa kila mtu badala ya kuwa na utitiri wa kadi.
“Watanzania wote, kila mtu awe na namba yake mwenyewe, (Wizara ya Habari) wameipa jina Jamii Namba. Haiwezekani mtu mmoja una identity (utambulisho) tatu, lazima uwe na identity moja, akiitwa Samia Suluhu rekodi ni hizo kila mahali,” alisema.
Kuhusu ulipaji kodi, Oktoba 4, 2024, akizindua Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi ambayo itafanya kazi ya kutathmini mfumo wa kodi nchini, Rais Samia alisema kila anayestahili kulipa kodi nchini anapaswa kufanya hivyo, kwani sasa walipakodi ni wachache na makusanyo hayaendani na viashiria vingine vya ukuaji wa nchi.
“Ni watu kama milioni mbili kati ya milioni 65 wanaolipa kodi, ukitoa watoto na wengine ambao hawapaswi kukatwa kodi hatupungui milioni 37… ina maana watu kidogo wanalipa kuwajenga watu wengi, hatuwezi kufika. Lazima wote tuchangie kwa kila mtu na kiasi chake,” alisema.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara Tanzania (TNBC), Dk Godwill Wanga amesema jamii namba ni muhimu ili kuweka urahisi wa utumiaji wa mifumo iliyounganishwa.
Amesema wakati hayo yakifanyika ni vyema taasisi za umma na binafsi zianze kupimwa kwa kuangalia namna zinavyotumia mifumo hiyo ili kuleta tija kwa wananchi.
Akijibu hoja kuhusu jamii namba, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehema, Dk Nkundwe Mwasaga amesema mchakato wa utekelezaji wa jamii namba umeanza na siku za hivi karibuni zitaanza kutolewa taratibu kwa ajili ya kuwaandaa watu ili watumie mifumo mipya.
Kuhusu kuunganishwa mifumo, Dk Mwasaga amesema zaidi ya 300 ya Serikali imeshaunganishwa, huku mifumo ya sekta binafsi ikiendelea kuunganishwa.