Ulega kuwa Waziri wa ‘Site’

Kilwa. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema katika utendaji wake asitarajiwe kuonekana zaidi ofisini bali atajikita kwenye ziara kukagua miradi mbalimbali ikiwemo barabara, ili kuona uhalisia wa utekelezaji wake.

Amesema Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya uboreshaji na ujenzi wa miundombinu hivyo, lazima afuatilie kwa ukaribu kujua utekelezaji wake hasa kwa kuzingatia viwango na ubora uliowekwa.

Ulega ameeleza hayo leo Ijumaa Januari 10, 2025, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Njia Nne wilayani Kilwa mkoani Lindi, muda mfupi baada ya kukagua ujenzi wa daraja la Mikerenge’nde ambalo liliathiriwa na mvua mwaka 2024.

“Niwahakikishie nitakuwa mkaguzi kila mara, siyo wa kusimuliwa na kuandikiwa kwenye madaftari nitakwenda mwenyewe kujua kinachoendelea,” amesema Ulega.

Awali Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Lindi, Emil Zengo alimweleza Ulega kwamba ujenzi wa madaraja mapya baada ya awali kuathiriwa na mvua za mwaka 2024 unakwenda vizuri.

Mvua hizo zilizonyesha Aprili mwaka 2024 zilisababisha uharibifu wa miundombinu hasa madaraja na barabara, hivyo kusababisha kero kutokana na mawasiliano kukatika.

Meneja huyo, amesema ujenzi wa madaraja likiwemo la Mikereng’ende unakwenda vizuri na makandarasi wote wapo eneo la kazi kutekeleza jukumu hilo la kuweka miundombinu ya uhakika katika barabara kuu inayounganisha mikoa ya Lindi, Dar es Salaam na Mtwara.

“Daraja hili la Mikereng’ende litakuwa na mita 40 likiwa na nguzo za chini 16 kwa kila upande, jumla 32. Kinachoendelea sasa hivi kuchimba na kusuka nondo zitakazowekwa chini pamoja na saruji ngumu,” amesema Zengo.

Katika hatua nyingine, Waziri Ulega amepongeza mwenendo wa ujenzi wa madaraja hayo, akisema Serikali imetoa Sh114 bilioni za dharura kwa ajili ya kuboresha mtandao wa miundombinu ya mkoa huo.

“Nimekuja kuangalia je, kasi ikoje ya ujenzi wa miundombinu kwa kuzingatia ubora uliotakiwa. Nimeambiwa ujenzi wa daraja la Mikereng’ende umefikia asimilia 25 za utekelezaji kazi zilizotarajiwa ziwe zimekamilika kati ya Februari au Machi, lakini mmekwenda mbele zaidi , hii ni kuthibitisha makandarasi wazawa wanaweza,” amesema Ulega.

Waziri Ulega amewataka mameneja wa Tanroads nchini kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.

Amesema hatakuwa na huruma kwa watakaobainika kwenda kinyume katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Hawa ni watu wenye weledi na wazalendo kwa Taifa lao, endeleeni kuwapa ushirikiano. Lakini siyo tena mnabweteka na sifa hizi, maana mgema akisifiwa tembo analitia maji,” amesema Ulega.

Katika hatua nyingine, Ulega amegawa mitungi ya gesi zaidi ya 100 kwa wananchi wa Kilwa wakiwemo wa Somanga, Njenga na Njia Nne  kwa ajili kuunga mkono jitihada za Serikali za mkakati wa nishati safi ya kupikia kwa Watanzania.

Waziri Ulega amesema mitungi ya gesi imetolewa na Tanroads kwa ushirikiano na makandarasi wanaotekeleza ujenzi wa madaraja ya Somanga, Njenga na Mikereng’ende ambapo wananchi wanaozunguka watanufaika.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Farida Kikoleka amesema inapoteka changamoto Serikali imekuwa mstari wa mbele ikiwemo kutenga fedha za dharura kuisaidia Kilwa, hali inayowapa faraja wananchi wa wilaya hiyo.

Related Posts