600,000 watumia majina feki kuomba vitambulisho Nida

Dar es Salaam. Ikiwa zimepita siku 25 tangu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa kuipa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), siku 60 za kusambaza vitambulisho milioni 1.2 vilivyotengenezwa, mamlaka hiyo imebainisha kukumbana na changamoto ya majina feki.

Akizungumza na waandishi wa habari, baada ya ziara fupi ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo, Mkurugenzi Mkuu wa Nida, James Kaji amesema mpaka sasa watu 600,000 wamebainika kufanya udanganyifu huo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Daniel Sillo (kulia) akiambatana na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa James Kaji (kushoto) akisalimiana na baadhi ya wafanyakazi wa mamlaka hyo wakati wa ukaguzi wa kituo cha uchakataji vitambulisho vya taifa. Jijini Dar es Salaam

Hayo ameyasema leo Ijumaa Januari 10,2025 baada ya ziara fupi ya kukitembelea kituo cha uchakataji wa taarifa za Nida, jijini Dar es Salaam.

“Tunapaswa kufuata utaratibu kwa kuhakiki majina yako, wapo waliosoma kwa majina tofauti na wanayo tumia sasa, na wale walioachishwa kazi kwa kutumia majina feki na sasa wanatamani kutumia majina yao halisi, changamoto iliyopo ni kuwa alama za vidole zinasoma jina alilotumia mwanzo na hivyo kuongeza idadi ya majina feki,”ameeleza

Hata hivyo, Kaji amesema tangu waanze kutumia mfumo mpya wa kutuma ujumbe mfupi kwa ambao vitambulisho vyao viko tayari, mpaka juzi Januari 8,2025, wamewafikia  watu 400,000 ndani ya wilaya 87 kati ya wilaya 153.

“Baada ya kuona malalamiko kuhusu upatikanaji wa vitambulisho, tumeweka mfumo wa kukusanya vitambulisho vyote vilivyokuwa kwenye ofisi za kata, na tumeandika ujumbe mfupi kwa kila mwenye namba za Nida, na tuna uhakika mpaka kufikia Januari 31,2025 tutakua tumesambaza vitambulisho vyote kama tulivyo agizwa,”amesema

Kadhalika, Kaji amewaasa Watanzania kufika kwenye vituo vya kujiandikisha ili kupata kitambulisho cha Taifa wanapotimiza miaka 18, ili kupunguza msongamano pale uhitaji unapokuwa wa haraka.

“Tumekuwa na tatizo la msongamano hasa ajira zinapotoka, na wanafunzi wanapotakiwa vyuoni,”ameeleza

Sambamba na hilo, Kaji ameendelea kuwaasa Watanzania kutoa taarifa kwa wakati pale changamoto inapotokea, ili itatuliwe kwa haraka.

“Wote ambao vitambulisho vyao vimewekewa tarehe ya ukomo wa matumizi wafike kwenye ofisi za Nida zilizo karibu ili wapatiwe ufafanuzi bila gharama yoyote.”

 Aidha, Naibu Waziri Sillo ameonyesha kuridhishwa na utendaji kazi wa mamlaka hiyo, na kuwa uzalishaji wa namba na vitambulisho unafanyika kwa kasi inayotakiwa.

“Miaka miwili iliyopita kulikuwa na changamoto kwenye utoaji vitambulisho, lakini Serikali imetoa Sh42.5 bilioni ili kuhakikisha wote waliojiandikisha na kupata namba wanapata vitambulisho pia,”amesema

Sillo amesema mpaka kufikia Septemba, 2024 uzalishaji umeongezeka kwa kiasi kikubwa.

“Kutoka Septemba, 2024 mpaka leo Januari 10,2025 vitambulisho takribani milioni 20 vimesambazwa kwa baadhi ya Watanzania ,”ameeleza

Sambamba na hilo, amesema ni vyema Watanzania wakafuata vitambulisho vyao mara watakapopokea ujumbe mfupi.

Pia, Sillo ameendelea kuwaasa Watanzania kujiandikisha bila kuchanganya majina.

Related Posts