Arusha. Familia ya watu sita wilayani Monduli, mkoani Arusha kwa siku nne imelala nje, baada ya nyumba zao kuchomwa moto na wanaodaiwa kuwa maofisa maliasili.
Watu hao wanaoishi Kata ya Monduli Juu wanadaiwa kuishi ndani ya hifadhi ya msitu wa jamii katika Kijiji cha Emairete.
Akizungumza na Mwananchi jana Januari 10, 2025 katika kijiji hicho, baba wa familia hiyo, Faraja Mephoroo amesema Januari 7, saa 12:00 asubuhi walifika watu aliodai aliwatambua kuwa wanafanya kazi kitengo cha maliasili walioambatana na mgambo na viongozi wa kijiji waliochoma nyumba zake tatu walizokuwa wakiishi na wake zake.
“Asubuhi hiyo mimi nilikuwa nimeamka nikitoa mifugo nje kuelekea shambani kuchunga, kwa mbali niliona gari la maliasili linakuja kwa kasi likiwa limewasha taa na kusimama barabarani. Walishuka watu waliokimbia kuelekea nyumbani kwangu,” amedai Faraja mwenye wake wawili na watoto watatu.
“Baada ya kuona hivyo nilijificha nione nini kinatokea, nikaona mke wangu mkubwa anashurutishwa kutoa vitu nje ya nyumba yake na mke wangu mdogo naye vivyo hivyo,” amedai.
Baada ya vitu na watoto kutoka nje, anadai watu hao kwa usimamizi wa mwenyekiti wa kijiji walimwaga petroli na kuchoma moto nyumba zake mbili walizokuwa wanaishi na nyingine ya pembeni iliyokuwa stoo ya chakula.
“Mambo hayo yalifanyika mbele ya macho yangu lakini sikuweza kufanya chochote kwa hofu ya wingi wao. Niliendelea kujificha hadi walipokamilisha kazi yao na kuondoka na ng’ombe wangu sita na punda watatu,” amedai.
Neyesu, mke mkubwa wa Faraja amesema asubuhi akijiandaa kwenda kukamua ng’ombe, aliona watu wengi wakikimbilia nyumbani kwake akaingiwa hofu akaingia ndani.
“Walipofika walianza kuuliza alipo mume wangu nikajibu sijui, wakatutaka kutoa vitu vyote nje wakisema wanachoma moto nyumba kwa sababu iko eneo la hifadhi.
“Tulilia mimi na mwenzangu tukiomba watupe muda wa kujiandaa kuhama wakakataa wakaanza kutoa vitu vyetu nje, vikiwamo vitanda na vyakula, wakachoma nyumba zetu na stoo ya mahindi,” amedai.
Amedai siyo mara ya kwanza kwa hali hiyo kutokea akieleza walishabomolewa nyumba ya awali mwaka 2018, wakahama ambako pia walibomolewa tena mwaka 2021.
Akizungumza na Mwananchi ofisa maliasili Wilaya ya Monduli, Adili Mwanga amesema suala hilo liko ofisi ya kijiji ndio wanaoweza kutoa maelezo.
“Ukitaka taarifa nzuri wasiliana na wahusika wakuu ofisi ya kijiji ambao hifadhi hiyo iko chini yao,” amesema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Emairete, Mboyo Kaiyai amesema wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya juhudi za mawasiliano ya kawaida ya kumhamisha mwananchi huyo kugonga mwamba.
“Huyu mtu tulishaongea naye kipindi cha nyuma mara nyingi na kumpa muda wa kuhama bila utekelezaji kwani eneo alilojenga nyumba liko ndani ya hifadhi ya msitu ambao umekuwa msaada kwetu hasa msimu wa ukame.
“Mbaya zaidi amekuwa akiharibu asili ya msitu kwa kukata miti na kulisha mifugo kwenye nyasi za asili kitendo kinachotishia uhai wa msitu kwa vizazi vijavyo,” amesema.
Ameongeza: “Hata siku moja kabla ya tukio tulifika nyumbani kwake kumjulisha anatakiwa kuhama la sivyo tutabomoa nyumba lakini hakutaka kutusikiliza, zaidi alikimbia na siku ya tukio tuliwahi ili kumpa taarifa ahame kwa hiari, lakini pia alikimbia ndiyo tukaamua kuteketeza nyumba ili isivutie watu wengine kuhamia,” amesema.
Akizungumzia suala hilo leo Januari 11, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Festo Kiswaga amesema hana taarifa za ofisi yake kutekeleza ubomoaji huo, akitaka apatiwe muda wa kuwasiliana na wahusika na kufuatilia kwa undani kujua kiini chake.
“Sina taarifa ya mtu kuchomewa nyumba kwa sababu niko safarini lakini naomba nikirudi nitafuatilia kujua ukweli wa mambo hayo na kama kosa limefanyika wahusika watachukuliwa hatua za kisheria, kwani kuchoma nyumba ya mtu ni kujichukulia sheria mkononi na ni kosa, lakini pia kama kweli mtu anaishi ndani ya hifadhi nayo ni kosa vilevile,” amesema.