Wakulima wa parachichi Njombe sasa kucheka

Njombe. Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema ujenzi wa kiwanda cha kuchakata parachichi mkoani mwake,  ni mkombozi mkubwa kwa wakulima kwani tofauti na ilivyokuwa awali mkulima alikuwa anauza kwa bei ndogo kutokana na hofu ya tunda kuharibika lakini sasa atakuwa na maamuzi ya bei.

Akizungumza katika ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa kiwanda hicho kilichopo Halmashauri ya Makambako, Mtaka amesema:

“Tunapokwenda kwenye msimu wa kununua parachichi wanunuaji wanakuja wengi sana lakini namna ya kumuonea mkulima ni kumwambia hizi ni ‘reject’ (zisizofaa) maana yake anajua huna pa kupeleka lakini anakuja mlango wa nyuma anakwambia nazinunua  kilo  kwa Sh150 hadi 180 kwa hiyo mkulima anaona kuliko zioze ni bora apate kiasi hicho kidogo cha fedha” amesema.

Amempongeza Mkurugenzi wa kiwanda hicho, kwa kuitikia kauli mbiu ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwatoa hofu wawekezaji ambao wana nia ya kuwekeza hapa nchini kuwataka kufanya hivyo na Serikali itawaunga mkono.

Ofisa Kilimo Mkoa wa Njombe Wilson Joel amesema makadirio ya parachichi ambazo zilikuwa zinakataliwa kutokana na kukosa ubora kwa mkoa wote ni tani 20,000 hivyo kama kiwandani kitaweza kuchukua zaidi ya tani 10,000 maana yake zaidi ya asilimia sabini ya parachichi hizo zitachukuliwa na kiwanda hicho.

“Nafikiri itakuwa mchango mkubwa sana kwenye sekta sisi tutaendelea kushirikiana na wewe ili kuweza kuwafikia wakulima ili hizo parachichi zikufikie,” amesema Joel.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Avo Africa Najib Kamal, amesema  kiwanda hicho mpaka kukamilika kwake kinatarajia kugharimu Sh20 bilioni, ambazo ni  gharama  kwa ajili ya mashine na vifaa vingine vitakavyokuwepo katika kiwanda hicho cha kuchakata mafuta.

Amesema kiwanda hicho kina mashine mbili na kitakuwa na uwezo wa kuchakata tani 600 za parachichi kwa siku na  Juni mwaka huu,  wataongeza mashine zingine mbili hivyo kuwa na uwezo wa kuzalisha tani 1,200 kwa siku.

Amesema kiwanda hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuajiri wafanyakazi  wasiopungua 400.

“Huu ni mradi wetu wa pili, wa kwanza ni ule wa kupaki parachichi na kusafirisha nje ya nchi lakini wa pili ni huu wa kuzalisha mafuta yanayotokana na parachichi na tunatarajia kuwa wazalishaji wakubwa wa mafuta hapa nchini” amesema Kamal.

Mkulima wa parachichi, Steven Mlimbila ameiomba Serikali kuwasogezea miundombinu ya umeme katika maeneo ya uzalishaji,  ili waweze kuvuta maji kutoka kwenye vyanzo kupeleka mashambani ili kuzalisha parachichi kwa wingi.

“Kilimo cha kutegemea mvua hakiwezi kumsaidia mkulima kuzalisha kwa wingi. Njia pekee inayoweza kumtoa mkulima hatua moja kwenda nyingine ni kilimo cha umwagiliaji, ” amesema Mlimbila.

Related Posts