Serikali yaanza kumwaga fedha miradi ya barabara

Lindi. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema Serikali imeanza kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi ya ujenzi wa barabara, hivyo hakutakuwa na kisingizio kwa makandarasi kutoikamilisha kwa wakati miradi hiyo.

Waziri Ulega ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Januari 11, 2025 wakati akikagua ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya Nachingwea – Ruangwa – Nanganga, yenye urefu wa kilomita 106. Pia, amekagua sehemu ya pili ya ujenzi huo inayohusisha kilomita 53.2 kutoka Ruangwa hadi Nanganga.

Mwonekano wa daraja la Mto Lukuredi wilayani Ruangwa mkoani Lindi

Ulega amesema awali malipo yalikuwa yanakwenda taratibu, lakini haikufanyika kwa makusudi bali Taifa lilikuwa na mambo mengi ikiwemo kuimalizia miradi ya kimkakati ya Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR na daraja la Kigongo Busisi mkoani Mwanza.

Amesema hivi sasa  Serikali imeanza kutoa fedha hizo katika miradi inayoendelea nchi nzima, kama ambavyo Ruangwa – Nanganga hadi Nachingwea inavyofanyika.

Jumatatu Januari 6, 2025, akizungumza katika kikao cha ushauri wa bodi ya barabara mkoa wa Arusha, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alisema mtiririko wa fedha kwenda kwenye miradi ikiwemo barabara ulipungua ili kumaliza miradi ya mkakati, lakini hivi sasa kasi ya utoaji fedha itaongezeka zaidi.

“Tunatambua kazi yenu (ujenzi wa barabara) ni kiungo muhimu katika uchumi, hakuna nchi iliyowahi kuendelea pasipo kuwa na miundombinu,” alisema Dk Mwigulu.

Leo akizungumza na wananchi wa Ruangwa kwa nyakati tofauti Ulega amesema; ‘’ Niwahakikishie Serikali imeanza kuweka mzigo (fedha), ambazo zimeanza kuingia, juzi imetolewa Sh64 bilioni kwa ajili ya malipo ya maeneo mbalimbali meneja huyu (Emily Zengo wa Tanroads mkoa wa Lindi) anafahamu, hakikisheni hii barabara inakamilika sasa.

“Simamieni haya malipo yake, fedha zinazokuja, tunaendelea kulipa na hawa wanaofanya kazi katika hii barabara wapewe kipaumbele ili walipwe na kukamilisha kazi kwa wakati. Nimeona wananchi wa Ruangwa wanahitaji sana barabara na siyo maneno mengine.”

Waziri huyo, ameiagiza Tanroads mkoa wa Lindi kuwa, gawio likifika wahakikishe wanapeleka fedha kwenye miradi ili ikamilike kwa wakati ikiwemo ujenzi wa daraja la Mto Lukuredi.

Kaimu Msimamizi wa mradi huo kutoka Kampuni ya China Railway 15th Bureau Group, Jianhang Yan amemwambia Waziri Ulega kulingana na maendeleo yanavyokwenda, ujenzi wa daraja hilo utakamilika baada ya miezi mitano ikiwemo barabara unganishi za daraja hilo.

Alipoulizwa na Waziri Ulega endapo wakipewa fedha watamaliza kwa muda gani alijibu: ” Kama fedha zipo tutamaliza kujenga daraja ndani ya miezi mitatu,”

Kutokana na hilo, Waziri Ulega alimtaka mkandarasi huyo, kufanya kazi kwa bidii ili kukamilisha ujenzi huo na Serikali inakwenda kumlipa malipo yake.

Related Posts