Taoussi aanza hesabu mpya | Mwanaspoti

KIKOSI cha Azam FC kimeanza mazoezi mapema wiki hii, ili kuijiandaa na lala salama ya Ligi Kuu Bara, huku kocha wa timu hiyo, Rachid Taoussi akisisitiza amewarejesha mapema mastaa wa timu hiyo ili kuhakikisha hesabu zake kwa duru la pili la ligi zinakaa sawa kuanzia Machi Mosi.

Azam inayoshika nafasi ya tatu kwa sasa nyuma ya vinara Simba na Yanga iliyo ya pili, imerejea katika kambi ya mazoezi tangu Jumatatu ya wiki hii kwenye Uwanja wa Azam Complex, ili kujiandaa na ngwe ya mwisho ya ligi iliyosimama kwa miezi miwili ambayo itarejea Machi Mosi kusaka bingwa wa msimu huu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Taoussi alisema ameamua kuwarejesha wachezaji hao mapema mazoezini kwa lengo la kuendelea kuboresha uwezo wa kila mmoja, akihofia kuwaacha wakae nje kwa miezi miwili kabla ya kurejea ligi watarudishwa nyuma na kumtibulia hesabu zake kwa msimu huu katika ligi hiyo.

“Wachezaji tayari walikuwa kwenye hali ya ushindani, hivyo kuwapa muda wa miezi miwili bila kucheza mechi za ushindani au kufanya mazoezi ya pamoja ni changamoto kwetu sisi kama benchi la ufundi itatupa kazi kubwa kuwarejesha kwenye ushindani,” alisema Taoussi anayetokea Morocco na kuongeza;

“Mpango wetu ni kuwa timu shindani, tuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha tunarejesha pointi tulizozidondosha na kuweza kufikia malengo, tunawajenga wawe ubora zaidi ya walipo sasa.”

Taoussi alisema atahakikisha anaijenga timu ikiwa ni pamoja na kupata mechi za kirafiki ili kufanya mazoezi kwa vitendo.

“Kwa upande wetu kama makocha kusimama kwa ligi kwa miezi miwili tutatakiwa kuwa na jukumu la kupanga programu za mazoezi upya na kuhakikisha wachezaji wanabaki katika hali ya ubora kimwili na kiakili,” alisema Taoussi aliyeipokea timu kutoka kwa Youssouf Dabo.

“Kuna presha ya matokeo tutakavyorejea ni mzunguko wa mwisho, matarajio makubwa ya viongozi na mashabiki ni matokeo mazuri hivyo endapo ningekubali kuacha wachezaji waendelee kukaa majumbani ningekuwa na wakati mgumu kufuatilia maendeleo yao,” alisema Taoussi.

Alisema anaamini akikaa nao karibu anaweza kuwajenga wachezaji wake kimbinu, kiakili kabla ya kurejea kwa ligi.

Azam iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2023-2024 katika mechi 16 za msimu huu imekusanya pointi 39 kutokana na kushinda michezo 11, sare tatu na vipigo viwili, huku Yanga ikiwa juu yake na pointi 39 kwea mechi 15 kama Simba inayoongoza kwa alama 40 hadi sasa.

Related Posts