Madiwani Mlimba wapunguza ushuru mchele kutoka elfu 4000 Hadi elfu 3000 kwa gunia

Baraza la madiwani Halmashauri ya wilaya ya Mlimba Mkoani Morogoro imeadhimia kupunguza ushuru wa Mchele kwa wafanyabiashara kutoka shilingi 4000 hadi shilingi 3000 Kwa gunia moja kutokana na kushuka kwa bei ya zao hilo

Akizungunza wakati wa baraza la madiwani Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Innocent Mwangasa kwa sasa zao la Mchele limeporomoka kwa kiasi kikubwa katika wilaya nzima ya Kilombero tokana na kipindi Cha masika kwani uchumi wa wananchi katika bonde Hilo kushuka tokana na kujielekeza katika shughuli za Kilimo.

Mwangasa amesema tokana na hali hiyo wameona wapunguze bei ya ushuru kwani wakiendelea na bei ya mwanzo wataumiza wakulima ama kuwakimbiza kabisa hivyo jambo la kuwasaidia ni kuwapunguzia bei ya ushuru.

Amesema baraza lilipokea maelekezo toka menejimenti na kuahidi kuyafanyia kazi kulingana na Sheria Ndogo za halmashauri pamoja na Sheria ya mapato ambayo inataka ushuru utozwe sio zaidi ya asilimia tatu ya bei ya soko.

Aidha baraza hilo limempongeza na kumshukuru Dk Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwajali na kuwapatia mahitaji wananchi waliopata maafa kutokana na mafuriko hususani katika kata ya Masagati na Utengule.

Amesema serikali kupitia Rais waliharakisha kuwapatia huduma za msingi na haraka pale waliopata taarifa ya mafuriko katika kata hizo ikiwemo uokozi na vyakula na kusema kuwa wananchi wa kata hizo wanamshukuru Rais na serikali yao kwa kuwajali na hivi sasa wapo salama wanaendelea na shughuli zao za kawaida ikiwemo Kilimo.

Katika hatua nyingine baraza hilo limeelekeza Menejimenti kuhakikisha wanakamilisha kazi ya kuzungumza na wawekezaji juu ya mashamba ya Halmashauri yaliyoko kata ya Masagati na Utengule ili kuwekeza na Halmashauri ipate mapato.

Pia mwenyekiti huyo ameelekeza mpango wa Halmashauri kuendeleza vipaji vya Wananchi wa Halmashauri kwa kuhakikisha kila Diwani ahakikishe Michezo, Sanaa na Utamaduni inafanyika kwa kila kata na vile vipaji vinavyofanya vizuri viwekewe Mpango mkakati wa kuviendeleza katika tasnia zao ili kuwezesha Vijana kuweza kujiajiri na kuajiriwa.

Awali baraza hilo lilishuhudia diwani mteule wa kata ya Kamwene Zugumbwa G. Mbaruku akiapishwa na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Mngeta na kuanza rasmi majukumu yake baada kuchaguliwa kufuatia kifo Cha aliyekuwa Diwani wa kata hiyo ambapo Baraza limempokea na kumpongeza Diwani huyo.

Related Posts