1,675 watibiwa magonjwa ya ngono Njombe

Njombe. Kaimu Mganga mkuu wa Mkoa wa Njombe Dk David Ntahindwa amesema mwaka 2024 huduma ya uzazi wa mpango ilitolewa kwa vijana balehe wapatao 35,223 (wenye umri kati ya miaka 10 hadi 24) huku zaidi ya 1,600 wakitibiwa magonjwa ya ngono.

Takwimu hizo zimetolewa leo Januari 11, 2025 wakati wa mkutano wa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Ummy Nderiananga na waandishi wa habari mkoani hapo.

“Vijana 2,677 wenye umri kati ya miaka 10 hadi 19 walipata huduma ya matunzo na vijana balehe 1,675 walipatiwa matibabu ya magonjwa ya ngono” amesema Ntahindwa wakati akizungumza katika mkutano huo.

Katika hatua nyingine, Nderiananga amesema juhudi zinapaswa kuchukuliwa ili kupunguza maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi hasa kwa kundi la vijana huko mkoani Njombe.

Amesema pamoja na jitihada za Serikali katika kukabiliana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi wenyewe,  bado kuna maambukizi mapya hasa kwa kundi la vijana.

Amesema kwenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa vijana Serikali inapaswa kuja na fikra mpya ya namna ya kuliendea kundi hilo ili kupunguza athari ya maambukizi kwa kundi hilo.

Amesema Serikali inatakiwa kuja na mawazo ya kuona vitu wanavyotaka vijana katika mapambano dhidi ya Ukimwi kwakua zimeshafanyika afua nyingi lakini bado maambukizi mapya yanatoka kwenye kundi la vijana.

“Kwenye maambukizi ya vijana tunapaswa kuja na fikra mpya ya namna ya kuliendea kundi hili tunaomba mkuu wa mkoa uturuhusu TACAIDS tushirikiane na mkoa wako pengine kuanza jambo hilo kwa hapa Njombe halafu tutalipeleka kwenye mikoa mingine” amesema Nderiananga.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Ukimwi Elibariki Kingu amesema ili kuwalinda vijana na maambukizi ya virusi vya ukimwi,  Serikali ya Mkoa wa Njombe inatakiwa kuhakikisha inatoa elimu katika shule za msingi na sekondari ili kulinda nguvu kazi ya taifa.

“Mheshimiwa RC umezungumza kwa kifupi namna gani mtalinda makundi ya vijana ambayo ni makundi mapya yasiingiliwe  na maambukizi haya tukutie moyo tunaomba uendelee na hayo majukumu kuhakikisha elimu ya kuwalinda vijana na watoto wetu inatolewa” amesema Kingu.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka amesema mkoa huo unafanya juhudi nyingi ili kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa kukutana na kuzungumza na vijana.

“Kwangu mimi ninapoona watoto wa mitaani maana yake ni ngono zembe, ninapoona mtoto wa mtaani maana yake Virusi vya Ukimwi. Ukimuona mwanafunzi ana mimba na uwezekano wa maambukizi pia ni mkubwa kwa sababu pale hakukuwa na kinga” amesema Mtaka.

Related Posts