Siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Slovakia, Robert Fico kutishia kukatisha misaada kwa Ukraine, Rais wa Marekani, Joe Biden amekiri kujutia uamuzi wa kuiwekea vikwazo Russia.
Marekani na mataifa ya Umoja wa Ulaya (EU) yameiwekea vikwazo Russia ikiwemo kuishawishi Ukraine kutoridhia ombi la kufufua mkataba wa bomba usafirishaji wa gesi asilia linalotoka Russia kwenda Ulaya kupitia Ukraine.
Kwanza mujibu wa Rais Zelenskyy wa Ukraine, kuridhia ufufuaji wa mkataba huo uliokoma Desemba 31, 2024, kungeiwezesha Russia kupata fedha za gesi, ambazo inadai ni sawa na kufadhili uvamizi wa vikosi vya Vladimir Putin katika ardhi ya Ukraine.
Tovuti ya Russia Today imeripoti kuwa Biden amesema vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya nishati ya mafuta na gesi ya Russia, inaweza kuathiri maisha ya Mmarekani mmoja mmoja hususan kuchangia ongezeko la bei ya bidhaa hiyo.
“Vikwazo vilivyowekwa hivi karibuni dhidi ya viwanda vya gesi na mafuta vya Russia vinaweza kuwaathiri Wamarekani hususan wa hali ya chini na inaweza kusababisha bei ya gesi kuongezeka,” amesema Biden.
Jana Ijumaa, Idara ya Hazina nchini Marekani iliweka vikwazo dhidi ya Russia, vikwazo ambavyo vinaungana na vilivyowekwa na Uingereza.
Vikwazo hivyo vinazilenga kampuni kubwa mbili za uzalishaji wa gesi za Russia ambazo ni Gazprom Neft na Surgutneftegaz na matawi yake yanayojihusisha na usafirishaji wa nishati hizo.
Zaidi ya meli 180 za Russia zilizokuwa zimezuiwa kusafirisha mafuta kwenda Ulaya nazo zimezuiwa kusafirisha nishati hizo kwenda Marekani.
Alipoulizwa iwapo uamuzi huo unaweza kuwa na madhara kwa raia wa Marekani, Biden alisema ni jambo ambalo liko wazi kuwa kuiwekea vikwazo Russia kutasababisha kupanda kwa bei ya gesi na mafuta kwa raia wake.
“Ni wazi kwamba bei ya mafuta na gesi itaongezeka kwa zaidi ya senti tatu ama nne kwa kila lita, ila vikwazo vyetu vitakuwa na madhara makubwa zaidi kwa Russia hususan kuikwamisha kuendeleza vita yake dhidi ya Ukraine,” alisema Biden.
“Vikwazo hivi pia vitakuwa na athari kwenye ukuaji wa uchumi wa Russia moja kwa moja,” Biden alisisitiza huku akisema Marekani inafanya hivyo ili kuikwamisha Russia kupata fedha za kupeleka mahitaji kwenye vikosi vyake vinavyoivamia Ukraine.
Utawala wa Biden umeanzisha vikwazo hivyo zikiwa zimebaki wiki mbili tangu kuondoka kwake madarakani na kumpisha Rais mteule wa taifa hilo, Donald Trump.
Trump amekuwa akiuokosoa utawala wa Biden huku akisema kuwa unachochea mizozo na kufadhili vita ambayo anaamini endapo angekuwa rais isingetokea.
Pia, alitishia kuwa atakapoapishwa kuingia Ikulu ya Washington DC, atasitisha misaada ya silaha, fedha na wanajeshi wanaopelekwa Ukraine kwenda kupigania taifa hilo jambo alilodai ni kuwaweka watoto wa Marekani katika hatari ya maisha ambayo haiwahusu.
Hata hivyo, Russia imevipinga vikwazo hivyo na kudai kuwa vinakinzana na utaratibu wa kisheria.
Rais Vladimir Putin amesema haviiumizi Russia kwa sababu itavitumia kuimarisha ustawi wa viwanda vyake vya ndani.
Alizungumzia vikwazo vipya vilivyowekwa na Marekani wiki hii, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Russia, Maria Zakharova amesema utawala wa Biden nchini Marekani utatafsiriwa kwa mateso aliyowaachia wananchi wake.
Bei ya mafuta nchini Marekani imeongezeka kwa asilimia tatu jana Ijumaa na kufanya ongezeko kuwa maradufu nchini humo katika kipindi cha wiki mbili, jambo ambalo huenda likaanza kuleta madhara kwa wananchi wanaoishi nchini humo.
Wakati Biden akikiri kuwepo ongezeko la bei ya mafuta na gesi kutokana na vikwazo hivyo, hali imeanza kubadilika nchini Uingereza baada ya kiwango cha hifadhi ya gesi kupungua kwa kasi.
Kwa mujibu wa Shirika la Uzalishaji Nishati nchini Uingereza la Centrica, hifadhi ya gesi nchini humo imeshuka kuliko kiwango cha kawaida katika hifadhi ya taifa hilo.
Centrica imetoa taarifa hiyo jana Ijumaa katika mkutano na vyombo vya habari, na kusema baada ya kufanya ukaguzi katika ghala za kuhifadhia gesi nchini humo lililopo Rough, wamebaini kupungua kwa kesi kwa asilimia 20 ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka 2024.
Hifadhi hiyo inadaiwa kuwa ilikuwa imejaa kabla ya kuanza kwa msimu wa baridi kali.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hifadhi ya gesi asilia nchi Uingereza iko katika msongo wa hali ya juu na tayari imesababisha ongezeko la bei ya nishati hiyo kwa watumiaji.
Kuongezeka kwa hali ya baridi kali na uamuzi wa Ukraine kugomea ufufuaji was mkataba wa bomba la usafirishaji wa gesi ya bei nafuu kutokea Russia kwenda Ulaya kupitia Ukraine ukitajwa kuchangia ongezeko hilo.
“Hifadhi ya gesi ilikuwa imeshaanza kushuka kuliko kiwango cha kawaida kwa mwezi Desemba ikilinganishwa na kiwango cha gesi kilichokuwepo katika kipindi kama hicho mwaka 2023.
Kupungua kwa gesi hiyo kumechangiwa na ongezeko la matumizi kutokana na baridi kali ya msimu huu sambamba na ongezeko la bei ya ununuzi wa gesi baada ya Ukraine kugomea mkataba wa bomba la gesi la Russia,” iliandika Centrica.
Kwa ujumla, kufikia Januari 9, 2025 hifadhi ya gesi katika vituo vya kuhifadhia nchini Uingereza imeshuka kwa asilimia 26.
“Hali kama hiyo imesikika katika mataifa mengine barani Ulaya,” ilisema Centrica huku ikidokeza kuwa hadi sasa hali ya uhifadhi wa nishati ya gesi nchini Uingereza ni asilimia 69 pekee ikilinganishwa na asilimia 84 mwaka jana katika kipindi kama hiki.
“Sisi ndiyo tuko vizuri kwa mataifa ya Ulaya kwenye suala la uhifadhi wa gesi lakini tumeshaanza kuona uwepo wa changamoto na uhaba wa nishati hii. Tutajitahidi kuhifadha kadri inavyowezekana ili madhara yasiwe makubwa zaidi,” alisema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Centrica, Chris O’Shea.
Tofauti na mataifa mengine wanachama wa EU, Uingereza haina ukomo wa kiwango cha uhifadhi wa gesi, badala yake imekuwa ikichukua tahadhari tangu mtikisiko wa nishati ulioyakumba mataifa hayo mwaka 2022.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.