Majeruhi ajali ya Msoga waruhusiwa

Bagamoyo. Majeruhi wote 21 waliokuwa wamelazwa kwenye Hospitali ya Msoga Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani kufuatia ajali iliyohusisha Coaster na lori wameruhusiwa baada ya afya zao kutengamaa.

Ajali hiyo iliyotokea Januari 10, 2025 Kijiji cha Mazizi Mkoani Pwani inadaiwa kusababishwa na uzembe wa dereva wa Coaster aliyekuwa anaendesha gari huku akitumia simu.

Akizungumza kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Salim Morcase, amesema ajali hiyo ilitokea jana saa tatu asubuhi Coaster ilikuwa inatokea Dar es Salaam kuelekea mikoa ya kaskazini na kwamba dereva wake,  aliligonga lori kwa nyuma na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi hao.

Amesema kuwa kufuatia ajali hiyo majeruhi walikimbizwa kwenye hospitali ya Msata ili kupatiwa matibabu,  huku mwili wa marehemu ukisubiri kufanyiwa uchunguzi kabla ya kukabidhiwa kwa ndugu  kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Leo Januari 11, 2025 Mganga mfawidhi wa Kituo cha afya Msata Dk Jamali Nankalava amesema kuwa baada ya kuwapokea majeruhi hao, waliwapatia matibabu na baada ya hali zao kutengamaa wamewaruhusu.

“Tulipokea majeruhi 21 kati ya hao wanaume walikuwa saba na wanawake 14 tunashukuru wote wamepata nafuu na kuruhusiwa” amesema.

Wakizungumza kwa masharti ya kutotaja majina, baadhi ya mawakala wa mabasi yaendayo mikoani kutoka kituo cha Mailimoja Kibaha,  wamesema kuwa gari hiyo ilipita mapema jana Ijumaa kwenye kituo hicho ikiwa na abiria mmoja na ikawa inatafuta wasafiri wengine.

“Ilifika asubuhi hapa stendi Mailimoja ikiwa na abiria mmoja ikawa inatafuta wasafiri wengine ikawapata ikaendelea na safari baadae tukasikia ajali imetokea ikihusisha gari hilo,” amesema mmoja wa mawakala hao.

Related Posts