SERIKALI imewataka mapromota kuhakikisha wanakuwa na ripoti ya afya kwa mabondia kabla ya kuingia makubaliano ya kusaini mikataba ya kucheza mapambano.
Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma ‘Mwana FA’ wakati akifanya kikao na mapromota wa ngumi za kulipwa jijini Dar es Salaam.
Mwana FA amesema mapromota wanatakiwa kuhakikisha wanakuwa na taarifa za afya za mabondia hao kabla ya kusainia mikataba ya mapambano ili kujua hali zao kiafya.
“Mapromota mnapaswa kufahamu taarifa za afya za mabondia kwa sababu mchezo huu ni hatari hivyo unatakiwa kufahamu afya yao kabla kusaini, ” amesema.
Naibu Waziri huyo amesema kupima kwa mabondia kabla ya kusaini mikataba itawasaidia kufahamu hali ya afya na namna ya kujilinda kuelekea katika mapambano yao.
“Jambo lingine ni bima za afya. Mabondia wanatakiwa kuwa nazo ili kupima afya kabla ya pambano na baada ya pambano ili kufahamu maendeleo yake,” amesema Mwana FA.
“Utaratibu wa vibali vya Uwanja wa ndege hivi sasa vimefutwa, hivyo mapromota wanatakiwa kufuata utaratibu nzuri ili kuepuka usumbufu kipindi mabondia wanapoenda nje ya nchi.”
Pia amewataka Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) kuhakikisha mabondia wanapitia ngumi za ridhaa kabla ya kuingia zile za kulipwa.
Amesema anataka uwekwe utaratibu wa mabondia kucheza mapambano kadhaa ya ngumi za ridhaa ndipo wacheze za kulipwa.
“Hivi sasa mabondia wengi wanaingia moja kwa moja kulipwa bila kupitia amater (ridhaa), hivyo TPBRC nahitaji kupata majibu Januari 15, mwaka huu ni mapambano mangapi wanatakiwa kupitia,” amesema Mwana FA.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Benson Chacha amesema changamoto kubwa wanayopitia kutoka kwa mapromota ni ucheleweshaji wa vibali vya mapambano.
“Mapromota wengi wamekuwa na changamoto ya kuchelewesha vibali vya pambano vya nje ya nchi. Pia kuhusu suala la ‘groves’ tumepokea kama BMT,” amesema Chacha, huku Mwenyekiti wa Kamati ya Mpito wa TPBRC, Emmanuel Saleh akiongeza kuwa wakati wanaingia uongozini waligundua makocha wengi hawana elimu ya mchezo huo.
Amesema wanao mkakati wa kumuita mkufunzi kutoka Kenya kuwapa elimu makocha ili kuendeleza mchezo huo.
“Tumeshafanya mazungumzo na mkufunzi huyo, hivi sasa tunasubiri gharama zake ili kutafuta mdhamini ambaye atamleta hapa ndani ya mwezi moja ili kuwapatia makocha wetu (elimu). Pia kila kocha anatakiwa kuwa na leseni ambayo itamtambulisha kuwa amepitia darasani na anatambua sheria na kanuni za mchezo huo,” amesema Saleh.
Kikao hicho kimefanyika wiki kadhaa tangu mashabiki wa ngumu washuhudie mmoja wa mabondia waliokuwa wanakuja kasi nchini, Hassan Mgaya akifariki dunia baada ya kupigwa TKO katika pambano la raundi sita lililofanyika Dar es Salaam, Desemba 28, mwaka jana.
Mgaya alicheza pambano hilo lisilokuwa la ubingwa lililofanyika usiku wa Desemba 28 na kupigwa katika raundi ya sita na aliyekuwa mpinzani wake ulingoni, Paulo Elias.