SERIKALI WILAYANI SONGEA YAWAKUMBUKA WALIOBOMOLEWA NYUMBA ZAO NA MVUA

Na Mwandishi Maalum,Songea




WAATHIRIKA wa maafa yaliyotokana na mvua pamoja na upepo mkali  tarehe
28 Desemba 2024 na Tarehe 2 Januari mwaka huu wilayani Songea mkoa wa
Ruvuma,wameanza kupokea misaada ya kibinadamu kutoka kwa  Serikali ya
wilaya ya Songea na na wadau mbalimbali.


Akizungumza kabla ya kukabidhi msaada huo Mkuu wa wilaya ya Songea
Kapenjama Ndile alisema,maafa hayo yamebomoa  nyumba zaidi ya 155 ambapo
katika Halmashauri ya Madaba nyumba 15 zimebomoka,Songea vijijini
nyumba 7 na katika Manispaa Songea nyumba zilizobomoka ni 133.


“hizi  nyumba zimebomoka kwa maana ya paa zake kuezuliwa na nyingine
kuanguka kabisa,pia kuna shule zetu mbili ambazo ni shule ya Sekondari
ya wavulana(Songea Boys) na shule ya Sekondari Chandarua”alisema Dc
Ndile.


Alisema,baada ya tukio kamati ya maafa ya wilaya ya Songea ilikutana na
kufanya tathimini ya kujua ukubwa wa tatizo na katika hatua ya kwanza
walibaini hasara iliyotokea ni kubwa japo hakuna mwananchi aliyepoteza
maisha.


Ndile alisema,wamepokea fedha taslimu zaidi ya Sh.milioni 4,unga wa
mahindi kilo 2120,sukari kilo 40,mchele kilo 380,maharage zaidi ya kilo
200,mafuta ya kula,maturubai 200,chumvi kilo 200 na sabauni 
yaliyotolewa na wadau mbalimbali.


Amewashukuru wadau kwa kusaidia waaathirika ikiwemo kampuni ya Aviv Ltd
iliyotoa mchele zaidi ya 2,000,maharage na maturubai ambayo yatawasaidia
waathiri kujihifadhi wakati huu ambao utaratibu mwingine unaendelea
kufanyika kwa ajili ya kuwasaidia watu walioathirika.


Dc NdileaAmewaagiza wenyeviti wa mitaa na vijiji waliopokea msaada huo
kwa niaba ya waathirika,kuhakikisha misaada hiyo inawafikia walengwa
bila kupotea na Serikali itawachukulia hatua kali kiongozi
atakayeshindwa kufikisha misaada hiyo kwa walengwa.


Alisema,Serikali imejaribu kufanya kila inaloweza kwa ajili ya kupata
misaada hiyo ili kuwasaidia binadamu wenzetu waliopatwa na janga hilo
ambalo limewarudisha nyuma kimaisha.


Katibu wa umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma Kelvin
Challe,amewaomba wadau wengine walioguswa na tatizo hilo kujitokeza
kuwasaidia wananchi wenzao katika kipindi hiki kigumu ambacho bado
wanahitaji msaada wa hali na mali.


Katibu wa Chama cha Mapinduzi Songea mjini James Mgego,amewataka
wananchi kuchukua tahadhari kubwa kipindi hiki cha mvua zinazoendelea
kunyesha kwa wingi katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Ruvuma.


Diwani wa kata ya Seedfarm Festo Mlelwa,amempongeza Mkuu wa wilaya kwa
kukusanya misaada hiyo na kuwashukuru  wadau wote waliochanga pamoja na
Serikali kwa kuratibu na kusimamia zoezi zima la ukusanyaji na ugawaji
wa misaada.


“naipongeza serikali ya wilaya ya Songea na wadau wote kwa kuwashika
mkono wananchi wa kata yangu na kata nyingine walioathirika na mvua
pamoja na upepo mkali uliopelekeaa baadhi ya mali ikiwemo nyumba
kuharibika”alisema.


Mwenyekiti wa mtaa wa Kuchile  kata ya Seedfarm Manispaa ya Songea Ali
Shafii Kuchile,amehaidi misaada yote itafika kwa walengwa na kusimamia
vizuri ugawaji wa vifaa hivyo kwa waathirika.

Mkuu wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma Kapenjama Ndile
kushoto,akikabidhi misaada mbalimbali  kwa Diwani wa kata ya Seedfarm
Manispaa ya Songea Festo Mlelwa kwa niaba ya wananchi  wa kata hiyo
waliotahirika na maafa ya mvua iliyoambatana na upepo mkali tarehe 28
Desemba 2024 na tarehe 2 Januari mwaka huu,kushoto Katibu wa CCM Songea
mjini James Mgego.

Mwenyekiti wa mtaa wa Kuchile kata ya Seedfarm Manispaa ya Songea mkoani
Ruvuma Ali Kuchile kulia,akipokea baadhi ya vitu kutoka kwa Mkuu wa
wilaya ya Songea Kapenjama Ndile kushoto, kwa niaba ya wananchi wa mtaa
huo walioathirika na maafa ya upepo yaliyotokea tarehe 28 Desemba mwaka
jana na tarehe 2 Januari mwaka huu.

Related Posts