Wataalamu: Kipindupindu kidhibitiwe kama Uviko-19

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya mikoa nchini ikiripotiwa kukumbwa na kipindupindu, wataalamu wa afya wameshauri juhudi zilizotumika kudhibiti Uviko-19 zitumike kukomesha ugonjwa huo.

Wakati wa mapambano ya Uviko-19, jamii ilihamasishwa kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kuepuka kugusana, matumizi ya maji safi na salama na kuzingatia usafi wa mazingira.

Mbali ya hayo, wataalamu wa afya wameshauri taarifa za mlipuko wa kipindupindu zitolewe kwa umma ili jamii ichukue tahadhari kwani upo utamaduni wa kupuuza maradhi hadi pale madhara yanapobainika kuwa makubwa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, kipindupindu kilianza Januari 2023 na mikoa 23 iliripoti wagonjwa ambayo ni Mara, Kigoma, Kagera, Singida, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Ruvuma, Mwanza, Geita, Rukwa, Dodoma, Manyara, Morogoro, Katavi, Pwani, Mtwara, Tanga, Arusha, Songwe, Lindi, Mbeya na Dar es Salaam.

Taarifa ya wizara ilisema hadi Desemba 2024, wagonjwa 11,703 na vifo 145 vimerekodiwa kutokana na kipindupindu, Mkoa wa Simiyu ukitajwa kuongoza kwa wagonjwa 4,246.

Hata hivyo, katika baadhi ya maeneo nchini yakiwamo yanayotajwa kuwa na ugonjwa huo, bado wananchi wanapanga bidhaa chini sokoni na kanuni za afya bado hazizingatiwi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Watoa huduma za afya Tanzania (Aphtha), Dk Samwel Ogillo amesema ili kudhibiti ugonjwa huo ni muhimu hatua zilizochuliwa wakati wa ugonjwa wa Uviko-19 zichukuliwe sasa.

“Mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu unapaswa kutolewa taarifa kama ulivyokuwa ugonjwa wa Uviko-19 na hatua zinazochukuliwa kuudhibiti zinapaswa kuendana ili kutokomeza mapema tatizo,” amesema.

Amesema watu wakitumia vyoo kwa njia sahihi na kunywa maji salama, ugonjwa hauwezi kuonekana kwani kipindupindu kinatokana na uchafu.

Dk Ogillo amesema wananchi wakielimishwa kuhusu ugonjwa huo na Serikali ikaweka miundombinu ya kuondoa majitaka utaisha.

Kwa upande wake, rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema wakati wa Uviko-19 watu walizingatia afua za kunawa mikono na hakukuwa na shida ya kipindupindu.

“Kinachotakiwa ni kuelimisha umma wa Tanzania kuzingatia kanuni za usafi, kuwekeza nguvu kwenye udhibiti na tiba ya wagonjwa waliopo sasa kwa haraka, na kisha kuwa na ufuatiliaji wa viashiria vya ugonjwa,” amesema.

Dk Nkoronko amesema wananchi na wadau wote washirikishwe kikamilifu, akieleza kipindupindu kinatokana na jamii kutozingatia kanuni za afya ambazo ni kunawa mikono kwa maji tiririka kila mara baada ya kutoka chooni na kabla ya kula.

Mtaalamu mshauri wa masuala ya afya, Festo Ngadaya amesema: “Unamkuta mtu anasema huu ni ugonjwa tu mbona tunaishi nao na ulikuwepo tangu mwanzo, kama ugonjwa wa kipindupindu haukuwahi kutokea kwenye familia yako na kusababisha madhara makubwa kama ilivyokuwa kwa Uviko-19 watu wana tabia ya kupuuza mambo.”

Amesema hofu ya ugonjwa kwenye jamii huanza kuonekana vifo vinaporipotiwa, akisisitiza jamii inapaswa kuzingatia kanuni bora za afya.

Amesema ushauri unaotolewa na wataalamu kuhusu kunawa mikono kwa maji tiririka na kunywa maji safi na salama, jamii haizingatii ndiyo maana kipindupindu hakiishi.

Dk Kuduishe Kisowile amesema jamii ndiyo inapaswa kutokemeza ugonjwa huo kwa kuzingatia kanuni za afya.

Amesema wakati wa Uviko-19 juhudi za kunawa mikono zilisaidia kudhibiti magonjwa ya kuhara na magonjwa ya upumuaji yalipungua kutokana na usafi kuwa mkubwa.

Zikiwa zimepita siku 26 tangu Desemba 17, 2024 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi alipotoa maelekezo kudhibiti kipindupindu, wagonjwa wamepungua kwa asilimia 85.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Januari 11, 2025, Kaimu Mganga Mkuu (RMO) wa Mkoa wa Simiyu, Dk Khamis Ramadhan amesema wagonjwa wamepungua kutoka 128, Desemba 17, 2024 hadi 19, Januari 10, 2025.

Amesema kupungua kwa maambukizi ni matokeo ya ushirikiano wa idara mbalimbali mkoani humo, hususani za maji, afya, elimu na utawala ambazo ziliingia mtaani kutoa elimu kuhusu mlipuko huo.

Amesema halmashauri ambazo bado zina wagonjwa ni Itilima yenye wagonjwa 12, Mji wa Bariadi (4) na ya Wilaya ya Bariadi (3).

“Ugonjwa wa kipindupindu kitaalamu unasababishwa na mtu kula kinyesi kibichi kwa hiyo anayeugua ugonjwa huo anapaswa kutambua kuwa ni mchafu au amekula chakula kichafu, kwa hiyo tunahimiza kufuatwa kwa kanuni za usafi katika jamii,” amesema.

Amesema baada ya ufuatiliaji, wataalamu wa tiba na magonjwa ya mlipuko, wamebaini ukosefu wa vyoo vya kisasa kumechangia ugonjwa huo.

Pia amesema mila potofu katika jamii ya Wasukuma kwamba mkwe hawezi kutumia choo kimoja na mkamwana wake huwalazimu baadhi kujisaidia porini.

Amesema uhaba wa maji hususani maeneo yenye mikusanyiko ya watu ikiwemo kwenye minada kunachangia kusambaa kwa ugonjwa huo.

“Choo bora ni kile ambacho kina pembe nne, kuna sakafu ambayo inasafishika kwa urahisi, kina tangi la kuhifadhia kinyesi lenye mfuniko. Asilimia zaidi ya 70 ya kaya zake hazikuwa na vyoo bora lakini tumeshatoa elimu na ujenzi wa vyoo bora umeanza,” amesema.

Amesema watu zaidi ya 12 waliokaidi maelekezo yaliyotolewa na RC Kihongosi kupitia kwa Katibu Tawala wa Mkoa huo, Prisca Kayombo hasa waliogoma kujenga vyoo bora wamefikishwa mahakamani.

Dk Ramadhan amesema kuna maagizo sita ya kutekelezwa na jamii ili kukomesha kipindupindu ambayo ni kuzuia wanafunzi kula na kwenda na kiporo shuleni, walimu wakuu kuhakikisha shule zinakuwa na vyoo safi vyenye huduma zote hususani maji tiririka na sabuni ya kunawa.

Mkoa umepiga marufuku unywaji wa maji ya kwenye majagi katika migahawa, badala yake mama na baba lishe waweke maji ya kwenye chupa kipindi chote cha mlipuko wa ugonjwa hadi itakapotangazwa vinginevyo.

“Pamoja na RC Kihongosi kufanya ziara kata zote zaidi ya 134 kuhamasisha ujenzi wa vyoo, tutapita tena kwenye shule zote wiki hii kukagua hali ya usafi lengo letu ni kuondoa kabisa ugonjwa huu kabla ya Februari,” amesema.

Amesema maofisa afya wamesambazwa maeneo yote yenye minada na magulio kusimamia usafi wa watoa huduma ya chakula na kuhamasisha utamaduni wa kunawa mikono mara kwa mara.

Mama lishe katika Kijiji cha Mwamapalala, wilayani Itilima, Leah Makindi amekiri kupokea maelekezo, akisema awali hakuwa na choo katika mgahawa wake lakini amejenga kwa ajili ya wateja.

Mfanyabiashara wa Nyamachoma wilayani Maswa, Maduhu Sarige amesema kutokana na tishio la ugonjwa huo amelazimika kuweka maji ya moto wakati wote kwenye genge lake ili kutohatarisha afya za wateja.

Mkazi wa Mwandoya wilayani Meatu, James John ameitupia lawama Serikali akidai taarifa sahihi za uwepo wa kipindupindu zilichelewa badala yake wataalamu waliuita ugonjwa wa kuharisha na kutapika.

“Katika jamii zetu Watanzania tumezoea kuhofia endapo tutasikia kuna kipindupindu tunachukua tahadhari mapema lakini mtu wa huko kijijini ukimwambia sijui ugonjwa kwa kuharisha na kutapika hata hashtuki kwa hiyo wahusika wasiwe wanaficha taarifa kutusaidia,” amesema.

Wakati mtaa wa Ilolo ukifungia vilabu vya pombe na wengine kufunga biashara kwa hiari kutokana na mlipuko wa kipindupindu, baadhi ya wafanyabiashara katika stendi ya Kabwe jijini Mbeya wameendelea kupanga bidhaa chini bila kuchukua tahadhari.

Mkoani Mbeya kipindupindu kimetajwa kuwapo katika halmashauri za wilaya za Chunya, Mbeya Jiji na Mbeya DC.

Mbeya Jiji imetajwa kuwa na wagonjwa 261, Mbeya DC watano, huku Chunya ikiwa haijaweka wazi takwimu zake.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera aliliambia Mwananchi wamechukua hatua za haraka kudhibiti ugonjwa huo ikiwamo kupiga marufuku bidhaa kupangwa chini.

“Tutafunga migahawa ambayo haina viwango, usitishaji vyakula maeneo ya mikusanyiko, kuwatenga wagonjwa maeneo maalumu na kamati za afya zijipange kudhibiti ugonjwa huo,” aliagiza Homera.

Akizungumza na Mwananchi Januari 10, Mwenyekiti wa Mtaa wa Ilolo, Ezekiel Mwasandube alisema vilabu viwili vya pombe vimefungwa kwa muda.

“Kwa kushirikiana na viongozi wengine akiwamo mtendaji ambaye amepewa kibali tumefunga vilabu viwili vya pombe, mwingine amefunga mwenyewe kwa hiari. Wananchi wamekuwa na mwitikio mzuri katika mapambano haya, wamekuwa watekelezaji wa maelekezo ya viongozi na wataalamu wao ili kukabiliana na ugonjwa huu,” amesema.

Kwa upande wa stendi ya daladala Kabwe, baadhi ya wafanyabiashara wamepanga bidhaa chini.

Mmoja wa wafanyabiashara aliyekataa kutajwa jina amesema hawajapata maelekezo kutoka kwa viongozi kuhusu upangaji huo wa bidhaa.

“Sina cha kuongea, nani aliyesema tusipange chini, mimi sijapewa taarifa yoyote na siwezi kusimamisha biashara zangu kwa kuwa ndiyo nategemea na familia yangu,” amesema.

Hata hivyo, gari la matangazo wiki hii lilipita mitaa ya jiji kuelekeza wananchi kuchukua tahadhari kwa kuzingatia usafi na kutopanga bidhaa chini ili kukabiliana na kipindupindu.

Imeandikwa na Baraka Loshilaa, Mgongo Kaitira na Saddam Sadick

Related Posts