Dk Kaushik atunukiwa tuzo na Rais wa India

Dar es Salaam. Ofisa Mtendaji Mkuu Hospitali ya Shree Hindu Mandal ya Dar es Salaam, Dk Kaushik Ramaiya, ametunukiwa Tuzo ya Pravas Bharatiya Samman (PBSA) na Rais wa India, Droupadi Murmu, ikiwa ni sehemu ya kuthamini mchango wake katika sekta ya afya nchini Tanzania.

Tuzo ya Pravas Brahatiya Sammanya ya mwaka 2025 ilitolewa Januari Mosi, 2025 na Rais wa India ikiwa ni sehemu ya kuthamini mafanikio makubwa wanayopata watu au taasisi zenye asili ya India na nje ya India katika sekta mbalimbali.

Dk Kaushik ni mtaalamu wa afya,  ametumia muda wake mwingi kufanya tafiti za magonjwa yasiyo ya kuambukiza pamoja na vihatarishi vya magonjwa ya moyo kwa jamii ya watu wa India wanaoishi nchi za Afrika.

Pia, mtaalamu huyo amekuwa akiwasaidia watoto wenye ugonjwa wa kisukari aina ya kwanza, magonjwa ya kurithi, maradhi ya moyo yaliyochochewa na matumizi ya dawa za kufubaza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, kisukari na kifua kikuu.

Mbali na uthubutu huo, kwenye taaluma, Dk Kaushik amefanya kazi na Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais Tamisemi kutekeleza mradi wa kudhibiti kisukari na magonjwa yasiyo ya kuambukiza katika hospitali za wilaya na mikoa kote nchini.

Mbali na majukumu hayo, Dk Kaushik amechapisha machapisho ya kitaaluma zaidi ya 100 na hivi karibuni aliteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Dk Kaushik baada ya kupokea tuzo hiyo anaweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa nne mwenye asili ya India kupokea tuzo hiyo akitanguliwa na Jayantilal Keshavji Chande, mwaka 2005.

Mwingine aliyewahi kupata tuzo hiyo ni Dk Rajni Kanabar, mwaka 2010 na Hajjat Shamim Parkar Khan aliyetunukiwa mwaka 2019.

Utoaji wa tuzo ya Pravasi Bharatiya hufanyika kuimarisha uhusiano baina ya watu jamii ya India waishio nje kuwaunganisha na Serikali ya nchi hiyo pamoja na asili yao.

Katika tukio hilo lililofanyika Bhubaneswar (Odisha) likifanyika kwa siku tatu kuanzia Januari 8 hadi 10, lilitawaliwa na ujumbe mkuu wa “Mchango wa Diaspora katika Visksit Bhafay.”

Related Posts