Moscow. Mfumo wa ulinzi wa anga wa Russia umefanikiwa kudungua ndege zisizo na rubani maarufu kama ‘droni’ 85 za Ukraine kati ya Ijumaa na Jumamosi ya leo.
Tovuti ya Russia Today imeripoti leo Jumamosi Januari 11, 2025, kuwa kati yake droni 31 zimedunguliwa zikijaribu kukatiza Bahari Nyeusi kwa ajili ya kwenda kutekeleza mashambulizi katika maeneo mbalimbali nchini Russia.
Droni 16 zilidunguliwa katika Mkoa wa Voronezh na Krasnodar, 14 katika Bahari ya Azov, nne katika Mkoa wa Belgorod, na mbili katika Mkoa wa Tambov. Droni moja ilidunguliwa katika Mkoa wa Crimea na Kursk.
Mapema asubuhi ya leo, Droni mbili za Ukraine zilifanikiwa kupenya na kulipua majengo mawili ya makazi katika Mji wa Kotovsk mkoani Tambov.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tambov nchini humo, Evgeny Pervyshov, ameandika katika ripoti kuhusiana na tukio hilo katika akaunti yake ya Telegram kuwa watu saba wamejeruhiwa katika shambulizi hilo lililofanyika asubuhi ya leo.
Amesema majeraha ya watu hao yamesababishwa na vioo vilivyopasuka kutokana na mlipuko huo, huku wengine wanne wakipata mshtuko wa moyo.
“Tayari misaada yote inayohitajika imeshatolewa kwa waathiriwa na haikuhitajika kulazwa hospitalini,” amesema Pervyshov.
Wizara ya Ulinzi ya Russia imetoa taarifa kuwa droni nyingine za Ukraine zilizopenya nchini Russia, zililipua maghorofa mawili ya ghorofa tano, kupasua vioo na kuharibu vibaraza vyake.
Tayari mamlaka ya jiji hilo imeshaunda kamati ya kufanya ukarabati wa uharibifu uliofanywa na mashambulizi ya droni hizo, huku wakazi wa maeneo hayo wakitafutiwa makazi ya muda katika eneo hilo.
Tangu mwaka 2024, Ukraine imekuwa ikiendesha mashambulizi katika maeneo yenye miundombinu ya nishati nchini Russia kwa kutumia droni na maeneo ya makazi.
Katika kujibu mashambulizi hayo, Russia ilianzisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati nchini Ukraine, maeneo yenye kambi za kijeshi, na kuharibu sehemu zilizokuwa zinatumiwa na vikosi vya Ukraine kurutubisha silaha za nyuklia.
Kati ya mashambulizi ya Ukraine ambayo hayatosahaulika nchini Russia ni lile la Desemba 2024 lililolenga majengo mawili ya ghorofa katika Mkoa wa Kazan, mashambulizi ambayo yalifananishwa na lile la Septemba 11 (9/11).
Katika hatua nyingine, kombora aina ya Kamikaze la Russia limerushwa na kulipua gari ya Ukraine aina ya ‘Bradley infantry fighting vehicle (IFV)’ iliyotengenezwa nchini Marekani. Shambulizi hilo limefanyika katika Mkoa wa Kursk nchini Russia.
Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema kuwa gari hilo limelipuliwa na kikosi cha Russia kilichopo Kaskazini kwa Kursk ambacho kimekuwa kikipambana na upinzani mkubwa wa uvamizi wa majeshi ya Ukraine katika mkoa huo.
Kipande cha video kinaonyesha droni hiyo aina ya Kamikaze ikilisogelea gari hilo la Ukraine lililokuwa limefunikwa wavu maalumu ya kuzuia droni pembeni mwa barabara.
Ukraine ilianzisha uvamizi dhidi ya Russia katika Mkoa wa Kursk mapema Agosti 2024 hata hivyo vikosi vyake vilirudishwa nyuma baada ya majeshi ya Russia kufanya mashambulizi ya kushtukiza na kuvirudisha nyuma.
Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Russia, Ukraine imeshapoteza wanajeshi wake zaidi ya 50,000 na vifaru zaidi ya 300 tangu wanajeshi wa Volodymyr Zelenskyy waanzishe uvamizi katika mkoa huo wa Kursk nchini Russia.
Rais wa Russia, Vladimir Putin aliuita uvamizi wa vikosi vya Ukraine eneo la Kursk kama ‘usio na tija’ na unaolenga kuipotezea Russia mwelekeo wa kujikita kwenye sekta nyingine za uzalishaji, huku akisema majeshi hayo hayatofanikiwa badala yake yatafutwa yote nchini humo.
Tangu kutangaza operesheni zake za kijeshi nchini Ukraine, Russia imeyatwaa maeneo ya Mkoa wa Donetsk, Luhansk, Kherson, Zaporizhia, Pokrovisk na Crimea iliyotwaliwa na Russia kutoka Ukraine tangu mwaka 2014.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.