Na Mwandishi wetu, Babati
MAMLAKA ya maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) mkoa wa Manyara, imeitaka jamii ya eneo hilo kutunza vyanzo vya maji ili viweze kuendelea kuhudumia kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
Meneja wa RUWASA mkoa wa Manyara, mhandisi James Kionaumela ameyasema hayo wakati akizungumzia mikakati ya upatikanaji maji kwa jamii ya eneo hilo.
Kionaumela amesema jamii inapaswa kutunza vyanzo vya maji kwa kutofanya shughuli za kiuchumi karibu na vyanzo vya maji ili kuhakikisha miradi ya maji inaendelea vyema.
“Kulima karibu na vyanzo vya maji, kukata miti, kuchunga mifugo au kufanya shughuli nyingine kama hizo haitakiwi kwa jamii,” amesema.
Hata hivyo, amesema Serikali imeweka mikakati ya kila jimbo kwenye mkoa huo kuwa na visima vipya vitano kwa lengo la kuhakikisha maji yanapatikana kwa karibu.
“Kwenye Mkoa wa Manyara kutachimbwa visima 35 japokuwa hadi sasa vimeshachimbwa visima 29 na tunaendelea kuchimba visima vingine vilivyobaki,” amesema Kionaumela.
Amesema RUWASA imejipanga kuhakikisha kuwa huduma ya maji inapatikana kwa kusambazaa kwenye vijiji vyote ambavyo havina maji.
Ameitaka jamii mkoani Manyara ambayo inatumia huduma ya mji kupitia mtandao wa RUWASA, kulipa ankara za maji pindi wanapotumia ili kufanikisha huduma nyingine kuendelea.
“Unapotumia maji na kutolipa ankara za matumizi yake hautakuwa unafanya jambo sahihi hivyo lipenj ili mamlaka iweze kujiendesha kwa mambo mbalimbali ya maendeleo.
“Kuna mafundi ambao wanafanya ukarabati pindi changamoto mbalimbali ya miundombinu ya maji ikiharibika hivyo watu wanapopatiwa huduma na kulipa ankara, pamoja na mengine fedha hizo hutumika kuwezesha mambo hao,” amesema Kionaumela.
Mkazi wa kata ya Magara wilayani Babati, Idd Ntandu ameipongeza RUWASA kwani ni miongoni mwa mamlaka zinazotoa huduma bora na za uhakika kwa jamii kwenye mkoa huo.
”Hata kwenye mbio za mwenge miradi ya RUWASA husifiwa mno kwani inatengenezwa vyema na thamani ya fedha inonekana kwa macho kwenye kila mradi inayofanyika,” amesema Ntandu.
RUWASA Mkoa wa Manyara hutoa huduma zake kwenye Halmashauri za Wilaya za Babati, Kiteto, Simanjiro, Mbulu na Hanang’ .