VIDEO: Hatua kwa hatua maendeleo Zanzibar

Unguja. Rais Hussein Mwinyi amesema Zanzibar inapoadhimishwa miaka 61 ya Mapinduzi, inajivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana, ikiwamo kudumisha amani, umoja na mshikamano na kukuza uchumi.

Mbali ya hayo, amesema kumefanyika ujenzi wa miundombinu, uwekezaji na biashara, kuboresha huduma za jamii na kuimarisha demokrasia na utawala bora.


Hatua kwa hatua maendeleo Zanzibar

Dk Mwinyi alisema hayo jana, katika hotuba ya kusherehekea miaka 61 ya Mapinduzi ambayo mwaka huu kitaifa sherehe zinafanyika Gombani, Pemba.

Alisema miaka 61 na mafanikio yake, msingi wake ni Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 na jitihada za wananchi na viongozi wa awamu zote zilizotangulia.

“Serikali ya awamu ya nane ilipoingia madarakani miaka minne iliyopita, imefanya juhudi za kuyaendeleza mafanikio yaliyopatikana na kuhakikisha Zanzibar inazidi kupiga hatua za maendeleo katika sekta zote na kudumisha misingi ya amani, uzalendo na umoja wa kitaifa,” alisema.

Rais Mwinyi alisema uchumi wa Zanzibar umeendelea kuimarika hadi kufikia Septemba 2024, umekua kwa kasi ya asilimia 7.5, huku pato la Taifa kwa bei ya soko nalo limeongezeka kufikia thamani ya Sh6.04 trilioni mwaka 2023 kutoka Sh4.78 trilioni mwaka 2021, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 26.

Alisema kuongezeka kwa pato la Taifa na kasi ya ukuaji wa uchumi kumesababishwa na kuimarika kwa sekta ya huduma iliyokua kwa wastani wa asilimia 9.9 mwaka 2023 kutoka wastani wa asilimia 1.3 mwaka 2021.

“Sekta ndogo ya huduma za watalii imeimarika zaidi, watalii waliotembelea Zanzibar wameongezeka kwa asilimia 145 kwa kipindi hicho. Kadhalika, kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa asilimia 51 kutoka Sh858.2 bilioni mwaka 2020/21 kufikia Sh1.3 bilioni 2022/23,” alisema.

Alisema kasi ya uwekezaji imeongezeka, akieleza miradi 449 yenye thamani ya Dola5.9 bilioni za Marekani imesajiliwa na Mamlaka ya Kukuza Uchumi Zanzibar (Zipa), inayotarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 22,966.

Miradi hiyo inahusisha uwekezaji katika sekta ya hoteli yenye miradi 169, biashara za majengo ambayo ni 99, viwanda (43), kilimo (28), michezo (28) na sekta nyinginezo 82.

Akizungumzia uimarishaji uwekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu, alisema Serikali kupitia Zipa imeruhusu uwekezaji katika visiwa vidogovidogo.

Dk Mwinyi alisema hadi sasa imesajili miradi ya uwekezaji katika visiwa 17, akieleza Dola 377.5 milioni (Sh954.34 bilioni) zinatarajiwa kuwekezwa.

Alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuvutia wawekezaji na kutangaza fursa zilizopo katika maeneo ya Bandari Jumuishi ya Mangapwani, huku ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji na umeme kwa ajili ya maeneo ya uwekezaji ukiendelea.

Ili kuleta mapinduzi ya kiuchumi, alisema wanaendelea na hatua za kuwawezesha wananchi ili kupambana na umasikini, akieleza mikopo yenye thamani ya Sh35.2 bilioni imetolewa kwa wananchi 24,111, wakiwamo watu wenye ulemavu 373.

Katika kuwapatia mazingira bora ya kufanyia shughuli zao wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo, Dk Mwinyi alisema Serikali imekamilisha ujenzi wa masoko makubwa na kuwawezesha 7,000 kufanya shughuli katika mazingira mazuri na ya kudumu.

Kwa sekta ya viwanda, alisema Sh33.122 bilioni zimetumika kwa ujenzi wa miundombinu katika eneo la Dunga Zuze.

Alisema jitihada za kuvutia uwekezaji katika eneo hilo zimefanikiwa, akieleza Serikali imeshatoa hati za ukodishaji wa ardhi kwa wawekezaji saba.

“Wawekezaji hao wataanzisha ujenzi wa viwanda, vikiwamo viwili vya kutengeneza dawa za binadamu, kiwanda cha kuunganisha pikipiki, bajaji na magari zinazotumia umeme,” alisema.

Pia, kiwanda cha kuzalisha bidhaa za plastiki na cha kuzalisha nguo, huku uwekezaji mwingine ni wa kiwanda cha kuzalisha bidhaa za chuma na ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa jua megawati 50 utakaotumika eneo la Dunga na wa ziada utaingizwa kwenye gridi ya Taifa.

Dk Mwinyi alisema baada ya kukamilika miradi hiyo, mchango wa sekta ya viwanda katika pato la Taifa utaongezeka kutoka asilimia 20.8 ya sasa na kufikia asilimia 25 mwaka 2030 na kuchangia upatikanaji wa ajira, bidhaa na kuchochea kuimarika biashara.

Alisema mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta ya utalii kwa kuongezeka idadi ya watalii kutoka 568,312 Novemba 2023 na kufikia 645,144 Novemba 2024 sawa na ongezeko la asilimia 14. Mbali ya hayo, alisema jitihada za Serikali, zimechochea kuongezeka uzalishaji wa samaki wanaovuliwa kwa asilimia 107.2 kutoka tani 38,107 mwaka 2020 zenye thamani ya Sh205.35 bilioni hadi kufikia tani 78,943 mwaka 2024 zenye thamani ya Sh618.18 bilioni.

“Serikali itaendelea kuwasaidia wavuvi ili kuwajengea uwezo wa kufanya shughuli zao kwa tija, ikiwamo kuwapatia vifaa, mikopo na utaalamu ili wavue kisasa na kufika bahari kuu,” alisema.

Dk Mwinyi alisema jitihada kubwa zimefanywa na Serikali kuimarisha huduma za bandari na usafiri wa majini.

Alisema Serikali ilifunga mkataba na Kampuni ya Africa Global Logistic (AGL) ili kusimamia uendeshaji wa Bandari ya Malindi kwa jina la Zanzibar Multipurpose Terminal (ZMT).

Alisema hatua hiyo imeleta mageuzi ya huduma za Bandari ya Malindi kwa kupunguza idadi ya siku za kuegesha meli kutoka saba hadi nne kutokana na uboreshaji uliofanywa na matumizi ya vifaa na teknolojia ya kisasa.

Pia, uwezo wa kuhudumia kontena umeongezeka kufikia makontena 70,768 mwaka 2024, sawa na asilimia 67 ya malengo ya kuhudumia makontena 105,000.

Ili kuimarisha usafiri wa baharini, alisema Serikali imeingia mkataba na Kampuni ya Synergy Ship Builders ya India kwa ajili ya ujenzi wa boti mbili za mwendo kasi zitakazofanya kazi baina ya bandari za Unguja, Pemba, Tanga na Dar es Salaam. Ujenzi wa boti hizo za kisasa unatarajiwa kuanza Februari, 2025.

Kwa upande wa usafiri wa anga, alisema Serikali kwa kushirikisha sekta binafsi, mapato ya mamlaka ya viwanja vya ndege yameongezeka kutoka Sh11.6 bilioni 2019/20 na kufikia Sh40.2 bilioni mwaka 2023/24 na kuimarika kwa huduma za wasafiri.

“Idadi ya abiria wanaotumia viwanja vya ndege wameongezeka kutoka 1,305,222 mwaka 2021 hadi abiria 2,140,986 mwaka 2024 na jumla ya mashirika ya ndege 81 ya kimataifa yanafanya safari za moja kwa moja kuja Zanzibar,” alisema.

Alisema Serikali ilifanya uamuzi wa kupungua bei za kuunganishiwa umeme kutoka Sh464,000 hadi Sh200,000 kwa gharama za uungaji usiozidi mita 30 ambayo ni sawa na wastani wa asilimia 50. Jumla ya wateja wapya wa umeme 115,242 wameunganishiwa huduma kutokana na punguzo hilo, huku Serikali ikipeleka huduma za umeme katika vijiji 222 kati ya Novemba, 2020 hadi Agosti, 2024.

Alisema wameimarisha sekta ya elimu kwa ujenzi wa shule mpya za ghorofa zenye miundombinu ya kisasa ya maabara, maktaba na vyumba vya kompyuta, huku za zamani zikifanyiwa ukarabati.

Alisema madarasa mapya 2,773 yamejengwa kupitia ujenzi wa shule 35 za ghorofa. Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 184.8 ya malengo ya kujenga madarasa 1,500.

Alisema bajeti ya elimu imeongezwa kutoka Sh265.5 bilioni mwaka 2021/22 hadi Sh830 bilioni mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 212.6.

Dk Mwinyi alisema ili kukabiliana na uhaba wa walimu, hasa wa masomo ya sayansi, Serikali imeajiri wapya 3,531. Katika mwaka huu wa fedha 2024/25 imepanga kuajiri walimu 1,867.

Akizungumzia uimarishaji wa huduma za afya, alisema mageuzi yamefanywa katika muundo wa uendeshaji wa huduma. Serikali imeimarisha miundombinu ya afya kwa kujenga hospitali 10 za kisasa za wilaya na moja ya mkoa zenye huduma bora za tiba, zikiwemo za kibingwa na vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa maradhi.

Uwepo wa hospitali hizo alisema umefungua ukurasa mpya wa upatikanaji wa huduma za afya nchini na kuboresha mfumo wa rufaa katika sekta ya afya na pia, wameanza ujenzi wa vituo vya afya 10 na zahanati 35.

Kwa upande wa maji, alisema Serikali imetekeleza miradi miwili mikubwa ya uhuishaji na uimarishaji wa huduma za maji Zanzibar wenye thamani ya Dola 92.18 milioni na mradi wa uimarishaji huduma za maji wa fedha za ahueni ya Uviko-19 wenye thamani ya Sh40.2 bilioni.

Alisema matangi 15 yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 134 yamejengwa na visima 64 vyenye uwezo wa kuzalisha wastani wa lita za maji milioni 177 kwa saa.

Dk Mwinyi alisema katika Muungano mafanikio yamepatikana katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Alisema tangu kuanzishwa utaratibu wa kushughulikia hoja za Muungano mwaka 2006, jumla ya hoja 26 zimejadiliwa na 22 kati ya hizo zimeshapatiwa ufumbuzi.

“Vikao 60 vya ushirikiano baina ya wizara na taasisi za Muungano vimefanyika. Zanzibar inaendelea kunufaika na mgawanyo wa mapato yanayotokana na misaada kutoka nje,” alisema.

Katika hatua nyingine, alisema Serikali zote mbili kupitia tume za uchaguzi zinaendelea na hatua za maandalizi kuhakikisha uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu unafanyika kwa misingi ya haki na sheria.

Alisema ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha inadumishwa amani ya nchi kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Related Posts