Unguja. Mapinduzi ya Zanzibar yalifanikishwa na watu wachache waliokuwa mstari wa mbele katika kupigania haki za Wazanzibari. Mmoja wa watu hao ni Kombo Mzee Kombo (89), aliyeongoza vuguvugu la Mapinduzi mwaka 1964. Mapinduzi ya Zanzibar yalitokea Januari 12, 1964, lengo ni kuondoa utawala wa kidhalimu, uliokuwa na ubaguzi wa rangi, ukabila, ubaguzi wa elimu, afya na kuweka usawa kwa wote na kusimika utawala miongoni mwa Waafrika, hususan Wazanzibari wenyewe.
Mwananchi limefanya mahojiano na Mzee Kombo nyumbani kwake Miembeni, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ikiwa ni miaka 61 tangu Mapinduzi hayo yatokee, ambapo anasimulia mambo mbalimbali, ikiwamo mipango ilivyosukwa na ilivyotekelezwa.
Katika simulizi yake, Kombo anaeleza namna walivyovamia vituo vya polisi, watu walivyouawa na kupata vilema vya maisha, familia yake ilivyomkataza kushiriki mapambano hayo lakini akasimamia uzalendo wa kuikomboa nchi yake na alivyokatwa panga la kichwani, akashonwa sindano bila ganzi.
Pia, anasimulia namna Serikali ilivyoanza kusukwa baada ya Mapinduzi, huku akipewa nafasi katika idara ya usalama wa Taifa na aliyekuwa Rais, Hayati Abeid Amani Karume. Kombo, ambaye alizaliwa Aprili 15, 1936, anasema yalipofanyika Mapinduzi, wakati huo akiwa na miaka 28, walikuwa na vikao vingi kuangalia namna ya kuwakabili wakoloni, wao walitumia silaha za jadi, huku wakoloni wakitumia silaha za moto hasa gobole.
Anasema walipotaka kufanya Mapinduzi, yeye alikuwa miongoni mwa viongozi hao, wakati huo alikuwa akifanya kazi katika kinu cha umeme Mtoni akiwa kibarua, hivyo wazee kwa wakati huo, pamoja na ujasiri aliokuwa nao, waliona atasaidia kuzima taa watakapoanza mapambano ya kuwakabili watawala waliokuwapo.
“Alikuja kwangu mtu mmoja anayeitwa Said Bavuai, akaniita nikiwa ndani na mke wangu na wazazi, akaniambia ‘sikiliza brother, nimeambiwa na akina Seif Bakari unatakiwa tukafanye Mapinduzi ya Serikali ya Zanzibar’.
“Nikasema unaniambia kweli wewe, akasema ndiyo nakueleza kweli, nilifurahi sana siku hiyo licha ya kuwa nilikuwa kijana, lakini nikakubaliana nao, tukafanya vikao vyetu, tukapanga namna ya kupindua,” anasimulia mzee huyo.
Anasema moja ya sababu ya kumtaka yeye awe miongoni mwa watu wanaotakiwa kuwa mstari wa mbele kufanya Mapinduzi, ni kwa sababu alikuwa akifanya kazi katika kinu hicho ili ukifika wakati wa kupindua yeye atazima taa zote ili iwe giza na itakuwa rahisi kwani wahusika hawatawaona.
Hata hivyo, “mimi niliwaambia hilo (la kuzima taa) haliwezekani, tutauana sisi wenyewe tukizima taa, itakuwa giza, utamjua mwenzako ni nani? Nikasema tutafute utaratibu mwingine, nikawaambia tutavaa vitambaa kuficha nyuso zetu.”
Mzee Kombo anasema walianza kupanga mipango hiyo licha ya kwamba lilikuwa kundi la watu kadhaa, lakini wao ndio walikuwa viongozi katika kundi. “Mimi nilikuwa mstari wa mbele, tukiwa na Said Bavuai na John Okelo”. Anasema wakati huo alikuwa mwenyekiti wa vijana (Youth League).
“Tulipanga na kuanza kuwatafuta vijana kwenda kuvamia vituo vikuu vya polisi, wengine kwenda Mtoni na Bomani ambapo kwa kipindi hicho ndiyo yalikuwa makao makuu ya polisi,” anasema.
Anasema wakati wanakwenda kuchukua silaha Bomani, kulitokea tofauti baina yao viongozi ambao walikuwa mstari wa mbele, wakibishana, wengine wakitaka waahirishe kukivamia warudi walipotoka.
“Ilipotokea vurugu, tulishauriana nani wa kukata seng’enge, mimi hapo nilijitoa mhanga na kwenda kukata kwa kutumia mkasi, lakini wakati nafanya hayo, nilikuwa kama akili yangu siyo ile ya kawaida kwani nilikuwa nikisema maneno makali sana hata mimi mwenyewe nilijishangaa,” anasimulia.
Anaendelea kueleza kuwa alikata seng’enge kufuata silaha kwa askari na wakati wanafanya hivyo, kuna watu walipigwa risasi na kupoteza maisha, lakini wao walifanikiwa kukiteka kituo hicho, saa 8:00 usiku.
Kwa mujibu wa Kombo, aliondoka nyumbani saa 6:00 usiku kwa ubishani na familia yake, wakati anaondoka nyumbani kwenda kwenye mapinduzi, aliacha familia yake, baba, mama na mke wake ambaye alikuwa hajazaa, wakilia.
“Nilipowaamsha nyumbani nikiwa nimevaa vibayavibaya, niliwaambia leo na kundi letu lote tunakwenda kuipindua Serikali, kwa hiyo mimi nakwenda, nikirudi sawa nisiporudi sawa itakuwa mipango ya Mungu, japo walinikataza lakini niliwaambia kama nikifa basi ila siwezi kuacha kwenda.
“Niliondoka wakiwa wanalia, lakini nikawaambia mimi nakwenda, tumuombe Mwenyezi Mungu, tukifanikiwa kupindua Alhamdulillah, nikirudi sawa, msiponiona mjue nimeuliwa, kwa hiyo, tusameheane, lazima niende.”
Anasema siku ya kufanyika Mapinduzi, walipanga fete (ngoma) maalumu ili watawala wasione kama kuna kitu kinaweza kufanyika siku hiyo, ikiwa ni mbinu ya kuwapoteza maboya.
“Tulipanga hivyo ili wasishtuke, wakiona watu wanacheza fete, watajua wapo kwenye starehe, hivyo isiwe rahisi kufikiria kuwa kuna kitu kibaya kinaweza kutokea siku hiyo.
Anasema baada ya kumaliza kuvamia Bomani, walianza safari ya kwenda kituo cha polisi Malindi, huku akieleza jinsi kituo hicho kilivyowapa taabu kukivamia.
“Kituo cha Malindi kilitupa taabu sana kwa sababu kilikuwa na matundu, kwa hiyo askari walikuwa wanachungulia kupitia matundu, wanaona watu wakija, watu walikufa wengi kwa kupigwa risasi, maana hali ilikuwa imeshachafuka lakini tulifanikiwa,” anaeleza.
Kombo anasema wakati akiwa mstari wa mbele akiongoza moja ya kundi, walipofika Kisima Jongoo akiwa na mawe mkononi, ghafla alivamiwa na mtu, akakatwa panga kichwani kisha akaanguka chini.
Huku akionyesha kwa kidole alama ya panga aliyonayo kichwani, Mzee Kombo anasema: “Baada ya kukatwa panga katikati ya kichwa, nilidondoka na kuvuja damu nyingi, kwa hiyo wenzangu wakaanza kunihudumia na kunibeba kunipeleka hospitali ambayo kwa wakati huo ilikuwa ikiitwa Vee Highland Hospital.”
Anaeleza kuwa kabla ya kupelekwa hospitali, ilibidi apitie nyumbani wakamuona kisha akapelekwa hospitali na alipofika nyumbani waliangua kilio ila aliwatuliza.
Alipofika hospitali, alikuta watu wengi ambao wamejeruhiwa “walikuwa hawatazamiki, kuna watu wengi wamepigwa wakihitaji huduma, wengine walikuwa hawana viungo.”
Kombo anasema kilichomsaidia walipofika hospitali kwa sababu ya umaarufu wake alikuta madaktari wawili ambao walikuwa majirani zake, kwa hiyo wakaacha wagonjwa wote wakaanza kumhudumia yeye.
Uchungu kushonwa bila ganzi
Moja ya vitu anavyokumbuka Kombo ni uchungu na namna alivyopiga kelele, wakati akishonwa nyuzi kichwani bila ganzi.
“Lakini kitu ambacho sitasahau nilishonwa sindano kichwani kavukavu bila ganzi huku ninapiga kelele, lakini nashukuru walimaliza kisha nikarudi nyumbani na kuanza kwenda Rahaleo (Mapinduzi Squre) maarufu Kisonge yalipofanyikia.”
Wakati alipokwenda hospitali, anasema tayari walikuwa wameshakamilisha kupindua na kuitangaza Serikali ya Mapinduzi.
Hata hivyo, licha ya kwamba alikuwa sehemu ya harakati hizo, alipofika katika eneo hilo aliwakuta walinzi ambao hawakumruhusu kuingia ndani, hivyo alilazimika kurudi nyumbani kwake na kwa wakati huo, hakutafutwa na mtu yeyote, ikabidi aendelee na kazi yake katika kinu cha umeme.
“Pale nje (Rahaleo) waliweka askari wa muda, nikafukuzwa kama hawanijui, kwa hiyo nikarudi kwangu, nikatulia kisha nikaenda kazini kwangu Saateni kuendelea na kazi yangu, sikuuliza kitu nikatulia,” anasema.
Anasema baada ya muda mfupi (anakadiria ilikuwa Februari 1964), akiwa anaendelea na kazi zake Saateni, alipokea ujumbe kutoka kwa Ibrahim Makungu (miongoni mwa watu alioshirikiana nao kwenye harakati hizo), akaambiwa anaitwa na Rais Karume, Ikulu.
Alipofika Ikulu, alikuta watu watano, Karume, Seif Bakari na Wajerumani watatu ambao walikuwa wakimshauri Rais kuhusu kuanzishwa Idara ya Usalama wa Taifa, hivyo na yeye (Kombo) akateuliwa kuwa Kiongozi Msaidizi wa Usalama wa Taifa.
Anasema katika kipindi hicho, idara hiyo ilianza na watu wanne na yeye akiwa kiongozi, licha ya kwamba hakuwa na elimu yoyote.
Anasema baada ya muda Wajerumani hao walishauri pia kuanzisha Jeshi la Uanamaji (Navy), kwa sababu ya mazingira ya kisiwa ili wasije kuvamiwa.
Baada ya kuanzisha kitengo hicho, ilibidi aende Ujerumani kusoma kwa ajili ya kuongoza idara, wakiwa watu 18.
Hata hivyo, anasema aliporudi, miezi sita baadaye, alipelekwa Makunduchi, kisha Mkoa wa Kaskazini na baadaye akahamishiwa Pemba mpaka wakati Karume anauawa mwaka 1972, alikuwa Wete, hivyo aliitwa haraka kurudi Unguja Makao Makuu, Idara ya Usalama.
Kombo anasema baada ya kipindi kupita, alihamishiwa Makao Makuu ya Polisi Ziwani ambapo alifanya kazi hadi alipostaafu mwaka 1992 akiwa na cheo cha ASP. Kombo anasema katika utawala wa Rais wa awamu ya pili, Aboud Jumbe alitunukiwa nishani.
Ili kuendeleza Mapinduzi yaliyotokea, anashauri kuwapo kwa umoja na mshikamano ili kujenga nguvu ya pamoja.
“Wosia wangu mkubwa kwa watu wote, vijana na wazee, kwanza umoja wetu uwe na nguvu zaidi, tuijue Serikali yetu, tuiombee dua mambo yote yanayofanyika tufanikiwe na tuzidi kufanikiwa kama ilivyotokea Mapinduzi,” anasema.
Anasema iwapo ukifanyika upuuzi na bila kuwa madhubuti amani ikatoweka au kutelekezwa yaliyofanyika kwa nia ya kuwakomboa Wazanzibari, “kama Taifa hatutakuwa tumeyaenzi Mapinduzi hayo.”