Hayo yamefichuliwa licha ya kauli za serikali ya Zanzibar za kukemea ubadhirifu na matumzi mabaya ya fedha za umma
Akisoma ripoti hiyo leo Jumatatu ikulu mjini Unguja, ,kaguzi mkuu wa hesabu za serikali ya Zanzibar, Dk Othman Abbas Ali, ametoa mfano wa miradi ya ujenzi wa hospitali 10 za wilaya na moja ya mkoa, kwamba malipo yake kwa wakandarasi yamekiuka taratibu, ambapo fedha nyingi zimelipwa kama matumizi ya ziada bila idhini.
“Ukaguzi wangu ilipitia ripoti ya thamini katika ujenzi wa hospitali moja ya mkoa na kubaini kuwa wizara ya afya uliwaalika wazabuni watano kwa zabuni isiyo ya wazi ambapo katika hatua za awali mzabuni aliyewasilisha zabuni ya bei ya chini iliokidhi vigezo na viwango vinavyotakiwa yenye thamani Sh bilioni 17.13 aliondolewa kwenye mchakato huo na kupendekezwa mzabuni mwengine mwenye thamani mkubwa zaidi kwa zaidi ya bilioni 24.25,” amesema mkaguzi mkuu.
Eneo jengine lililotajwa kuhusika na matumizi hewa, ni ukarabati wa kiwanja cha michezo gombani kisiwani Pemba, ambapo katibu mkuu wa wizara ya habari, vijana, utamaduni na michezo amedaiwa kuruhusu nyongeza ya fedha kwa mkandarasi bila hata kupata baraka za bodi ya wizara.
CAG: Mfumo wa malipo kwa mtandao haujamaliza ubadhirifu
Dkt Abbas amefafanua kuwa nia njema ya serikali kutaka malipo yafanywe kwa njia ya mtandao, haitekelezwi ipasavyo, na bado mifumo hakidhi haja au inachezewa kwani fedha nyingi hutumiwa na kulipwa lakini hakuna pahala zinaposomeka.
“Dosari nilioibaini katika upekuzi wangu wa mifumo ni malipo yasiokuwa na tija kwenye utekelezaji wa miradi ya tehama yenye thamani ya bilioni 23.76”
Kwa upande mwengine, mkaguzi huyo amedai kuingiliwa katika kazi zake kinyume na katiba, kwa baadhi ya watendaji wakuu wa wizara kufanya urasimu kwa nia ya kumzuia kutekeleza majukumu yake ambayo yapo kisheria.
Akizungumza baada ya kupokea ripoti ya mkaguzi, Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi, amesisitiza mifumo iheshimiwe, na pale penye kasoro hatua za kurekebisha zichukukliwe.