KONA YA MAUKI: Jinsi ya kushughulikia migogoro

Katika maisha yetu ya kila siku, iwe kazini, ofisini au nyumbani, migogoro ni asili na sehemu ya maisha yetu. Ukweli ni kwamba maisha yangekosa uhalisi pasipo kuwa na migogoro hii. Hii husababishwa na ukweli kwamba hakuna anayefikiri, au kuwaza au kuwa na mtazamo sawa na mwenzake, kwa sababu vyanzo vya mitazamo hii hutofautiana, kwa hali hii iko migogoro ambayo ni vigumu kuiepuka.

Matatizo hutokea pale misuguano hii inaporuhusiwa kutoka nje ya uwezo wetu na kuzigusa haiba na hisia zetu. Vyanzo vya migogoro vyaweza kuwa vingi, lakini kikubwa ni kwamba kila mmoja anataka ushindi au kupenya kupitia njia yake, na hakuna aliye tayari kuafikiana na kuendana na mtazamo wa mwenzake.

Baadhi ya sababu za kuwepo migogoro ni kama zifuatazo: Tofauti katika malengo, ushindani – hasa unapozidi kipimo, kutokuwa na maelewano au tofauti za kimtazamo, kukosa ushirikiano – (kihalisia au kwa kufikirika) na migogoro ya haiba.

Vyanzo vingine ni matatizo ya mamlaka – mfano misuguano na mabosi, misongo binafsi ya mawazo, uchu wa kutimiza majukumu, kutokuwa tayari kukubali majukumu, kushindwa kuishi au kufanya sawasawa na mipango au maelekezo yaliyowekwa na tofauti katika namna au njia za kufikia malengo.

Tafiti zilishaonesha kuwa wafanyakazi wengi (wasimamizi na wasimamiwa) hutumia zaidi ya asilimia 25 ya muda wao wa kazi katika kusuluhisha migogoro. Jambo hili linaifanya migogoro kuwa ya gharama sana.

Migogoro siyo jambo baya, mara nyingine ina matokeo mabaya na mingine ina matokeo mazuri, ile migogoro inayoleta matokeo mazuri lazima tujue jinsi ya kuichochea na kuiendeleza, ingawa inabidi pia tuwe na ujuzi wa kuvistahimili vyema vile vyanzo vya migogoro hii ili visilete madhara yasiyotarajiwa.

Migogoro ya aina hii yaweza kuwa na faida zifuatazo: Kufunua vitu muhimu na vya msingi vilivyofichika muda mrefu, kuboresha mawasiliano baina ya walengwa waliohusika, huchochea ari ya kazi na uwezo wa kufikiri na humwamsha kila mhusika kutimiza majukumu yake. Huleta kufikiwa kwa suluhisho la tatizo au matatizo fulani, huwawezesha wahusika kupunguza au kutua mzigo wa hisia au hasira zilizorundikana na huwawezesha wahusika kutumia ufanisi wao ili kuonyesha ujuzi walionao.

Kwa kawaida migogoro yenye matokeo mabaya haina budi kuepukwa, ingawa siyo rahisi mara zote. Hata kama kuna ugumu katika kuepuka migogoro, basi jitihada za makusudi zifanywe ili kutafuta njia bora za usuluhishi.

Migogoro inaweza kuwa mibaya na inayoleta athari pale ambapo: Inaondoa akili na mawazo ya watu kutoka kwenye uhalisi wa jambo au mambo, inasababisha mtu au kundi la watu kutoshirikiana na inapowafanya wanaohusika kuchanganyikiwa na kutoridhika.

Wakati migogoro mingine ni ya kuiepuka, iko ambayo inabidi kuishughulikia ili isije kuzidi na kwenda nje ya uwezo wetu. Ili kufanya hili liwezekane zingatia haya yafuatayo:

Jifunze kutambua na kuzikubali tofauti baina ya watu. Mfano haiba zao, mahitaji yao, historia zao, matumaini yao nk.

Jifunze kusikiliza vema kila wengine wanachokisema na siyo tu kukimbilia kutoa hukumu.

Jaribu kuwafahamu vema wale wote ambao umekuwa unakwaruzana nao mara kwa mara, fanya hivi ukisha jielewa kwanza mwenyewe, na uelewe pia kwa nini wanafanya au wanakuwa vile walivyo.

Jaribu kuangalia mambo kwa mtazamo wa wenzako pia, siyo kila wakati kujiona uko sawa na wenzako ndio wanaokosea.

Fahamu na ukubali kuwa haiwezekani kila mtu akubaliane na wewe mara zote, na usiruhusu hii hali ya kupingwa au kukosolewa kukukosesha raha, na kukukasirisha.

Waruhusu na wengine wanaohusika katika mgogoro wapate nafasi ya kujielezea vile wanavyofikiri, waombe wafanye hivyo kwa upole na sio kwa ukali.

Baada ya mgogoro kutulia angalia nini umejifunza kutokana na mgogoro huo, usiruhusu mgogoro ukapita tu bila kujifunza chochote.

Migogoro lazima isuluhishwe kwa njia bora kila mara, hili linawezekana kupitia njia zifuatazo: Kujifanya kama hakuna kinachoendelea wala kilichotokea, hasa pale tatizo linapokuwa halina umuhimu sana.

Lakini pia kutokuzijali sana tofauti za mawazo baina yenu, hasa pale mahusiano yenu yanapokuwa ya maana zaidi na wote mnatamani kuilinda amani iliyopo baina yenu.

Mara nyingine mamlaka yanaweza kutumiwa ili kuunyamazisha mgogoro, hususan mmoja anapokuwa ana nguvu kwenye mamlaka kuliko wengine, hapa mtu anaweza kuahidi kuushughulikia mgogoro taratibu wakati wengine wakiwa kimya na wakiendelea na shughuli za kawaida. Mbinu hii inaweza kufaa kwa kupoza mgogoro kwa muda mfupi na siyo kutengeneza mahusiano baina ya walioko katika mgogoro huo.

Njia nyingine ni ya kutafuta muafaka baina ya pande mbili zilizo kwenye mgogoro, hii hutokea zaidi pale ambapo pande zote mbili zinapotaka kuyatimiza malengo yao na kwa hiyo kuliko wote wakose basi bora hata kila mmoja apate japo nusu ya lengo.

Related Posts