Dar es Salaam. Inaelezwa viongozi wengi wanaoongoza vikundi vya upatu wanakutana na changamoto kubwa ya madeni baada ya washiriki kushindwa kulipa fedha kwa wakati, kuchelewesha, au hata kutoweka bila taarifa.
Hali hii imeathiri hasa upatu unaochezeshwa mtandaoni, ambapo baadhi ya wanufaika huzima simu, kuhama makazi, na hata kutoweka, jambo linalowaweka viongozi wa upatu kwenye matatizo.
Kama sehemu ya mfumo wa upatu, viongozi huwa kiunganishi kati ya washiriki wanaochangiana fedha. Viongozi hao hunufaika kwa kupata jina moja la ziada kama malipo ya kuhifadhi na kusimamia fedha za mpokeaji. Hata hivyo, mara nyingine, wanapokea lawama pale fedha zinapopotea au mpokeaji anaposhindwa kutimiza ahadi.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyorekebishwa mwaka 2022, kifungu cha 171A, kushiriki, kuongoza, au kusimamia upatu ni kinyume cha sheria. Sheria hiyo inasema adhabu ni faini ya hadi Sh5 milioni au kifungo cha hadi miaka mitano.
Ashura Rashid, mkazi wa Buguruni ambaye ana uzoefu wa zaidi ya miaka mitano katika michezo ya upatu, anasema anachezesha upatu kwa viwango tofauti vya fedha kuanzia Sh1,000 hadi Sh20,000 kwa siku.
Anasema changamoto kubwa anayoikumbana nayo ni watu kuchukua fedha za washiriki na kutokomea huku wengine wakihama makazi yao.
Ashura anasema wapo wanaodai wana dharura na kupewa fedha kwa dhamana ya kijumbe, lakini baadaye kutoweka.
“Nilishawahi kulipia watu sita baada ya mmoja kutoroka na pesa za washiriki, hali iliyoniacha katika deni kubwa,” amesema.
Hali hii pia inasababisha migogoro ikiwemo kuuza mali za watu waliokwepa madeni au kupelekana polisi na ofisi za serikali za mitaa. Aidha, wengine huingia majina mengi kwenye upatu bila kujua chanzo cha fedha za kulipia.
Kwa upande wake, Abdallah Salum, mfanyabiashara wa ndizi eneo la Mabibo, anasema wakati mwingine vijumbe ndio wanaoharibu mfumo wa upatu kwa kuwaweka watu wasiokuwa waaminifu na kuchukua majina mengi yasiyolipwa.
“Unakuta kijumbe ana majina matatu au manne, anakula pesa mwenyewe kisha anadai mpokeaji hapokei simu,” anadai Salum.
Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Wenyeviti Wilaya ya Kigamboni, Juma Mwingamno, anasema changamoto kubwa katika michezo ya upatu ni ukosefu wa elimu kuhusu masuala ya fedha, hali inayorahisisha udanganyifu na kuibua migogoro.
“Nimekutana na kesi mbili za upatu na nimewaeleza wanachokifanya ni kinyume cha sheria. Ili kuepuka migogoro hii, wanapaswa kujiunga na vikundi vinavyotambulika na vilivyopewa leseni ya ukopeshaji, badala ya kupeleka pesa moja kwa moja kwa mtu, hali inayoongeza uwezekano wa kudhurumiana,” anasema Mwingamno.
Anabainisha kuwa baadhi ya watu wanajikuta wakidhalilika kwa kudaiwa fedha ndogo, kama Sh300,000, huku familia zao zikiwa hazifahamu kuwa wamejiunga na upatu.
“Wakati wa kudaiwa, wapo wanaojikuta wakifuatwa na watu wanne au zaidi wakiwa na kelele, jambo linalosababisha aibu kwa familia, hasa ikiwa tayari wamekula fedha za majina mengine,” anasema.
Mwingamno anasema vijumbe wa upatu wanajikuta katika matatizo makubwa, ikiwemo kulipa madeni ya washiriki wao au hata kulazimika kuhama makazi yao. Hii ni kwa sababu wanashirikiana na watu wasiofanya uchunguzi wa kina kuhusu kipato na shughuli zao.
Aidha, anasema michezo ya upatu imechangia kuvunjika kwa ndoa, hasa pale wanawake wanaposhiriki bila kuwafahamisha waume zao.
“Michezo hii inachezwa sana na wanawake, sasa inapotokea mnufaika anashindwa kulipa na kufuatwa nyumbani kwake huku mumewe akiwa yupo, hali hiyo huleta udhalilishaji mkubwa kwa familia,” anasema.
Mwingamno anaongeza kuwa kwa sasa, katika maeneo ya Kivukoni, amechukua hatua madhubuti kwa kuweka watu maalumu wanaofuatilia wachezesha upatu.
“Mtu akipatikana, namkamata na kumpeleka kwa kila mtu aliyempa pesa. Nimepiga marufuku michezo hiyo na ikiwa itashindikana, tunafikisha suala hilo katika vyombo vya sheria,” anasema.
Anawahimiza wananchi kuzingatia uaminifu na kujiunga na vikundi rasmi vya kifedha, ili kuepuka changamoto zinazotokana na upatu usio na udhibiti wa kisheria.
Ukosefu wa nidhamu ya kifedha na athari za upatu kwa wanachama wake hilo nalo ni janga lingine.
Mtaalamu wa Uchumi, John Mlay, anasema tatizo kubwa linalowakumba wacheza upatu ni ukosefu wa nidhamu ya kifedha.
“Wanachama wengi wa upatu hawana mipango thabiti ya kifedha na wengine hujiunga bila kuzingatia uwezo wao wa kuchangia. Hali hii husababisha migogoro wanaposhindwa kutimiza ahadi zao,” anasema Mlay.
Mlay anaongeza kuwa upatu unapaswa kuwa njia ya kusaidiana ili washiriki wafanikishe malengo yao kifedha. Anatoa wito wa kuwepo kwa sheria za ndani zitakazowabana wanufaika, ikiwemo kuhakikisha viongozi wanafahamu mahali wanachama wanaishi na kuwa na mawasiliano na ndugu wa karibu wa kila mshiriki.
“Kiongozi wa upatu anapaswa kuwa na mfumo wa maandishi unaosimamia shughuli zote, jambo ambalo litasaidia kupunguza visa vya wanachama kuchukua pesa na kutoweka. Pia, kila mnufaika awe na mdhamini anayefahamika ili kuwapa haki wanachama wengine,” anasisitiza.
Rehema Omega, mwanasaikolojia wa kijamii, anaangazia athari za kisaikolojia zinazotokana na migogoro ya upatu, akisema hali hiyo huathiri wanachama na viongozi kwa njia mbalimbali.
“Wanachama wanaoshindwa kulipa mara nyingi wanakumbwa na wasiwasi mkubwa, wakihofia aibu au hatua za kisheria. Kwa viongozi, mzigo wa kulipa madeni ya wanachama wengine husababisha msongo mkubwa wa mawazo, unaoweza kuvuruga hata maisha yao ya kifamilia,” anasema Rehema.
Anatoa wito kwa wanachama na viongozi wa upatu kuwa waangalifu na kuweka mikakati madhubuti ya kifedha ili kuepuka migogoro na athari za kisaikolojia zinazoweza kuathiri maisha yao ya kijamii na kifamilia.
Ofisa Maendeleo ya Jamii, Rose Mgema, anasema changamoto zinazotokana na upatu zinaweza kupunguzwa kwa kuimarisha usimamizi wa vikundi vya kusaidiana na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kujiunga na vikundi vilivyosajiliwa rasmi.
“Taasisi za kijamii zinapaswa kutoa mafunzo kuhusu faida za kujiunga na vikundi vya vikoba vilivyosajiliwa, ambavyo vina mifumo bora ya ufuatiliaji wa fedha. Hii ni tofauti kabisa na upatu wa jadi ambao mara nyingi hukosa uwazi na usimamizi mzuri,” anasema Rose.
Rose anatoa wito kwa jamii kushirikiana na taasisi zinazotoa mafunzo ya kifedha ili kujenga mifumo thabiti ya usimamizi wa vikundi na kupunguza migogoro inayoweza kusababisha madhara ya kifamilia na kijamii.