Wadau watoa angalizo, sera ya elimu ikizinduliwa Januari 31

Dodoma. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua rasmi Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya 2014 toleo la 2023, Januari 31, 2025. Kabla ya uzinduzi huo, wadau wa elimu wametoa angalizo kwenye mambo matano yanayopaswa kuzingatiwa ili kufanikisha utekelezaji wa sera hiyo.

Mambo hayo ni pamoja na dhamira ya watekelezaji, hamasa kwa walimu, miundombinu, utengaji wa rasilimali fedha, matumizi ya teknolojia, na upatikanaji wa wataalamu wa kutosha.

Akizungumza na Mwananchi jana jijini Dododma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Adolf Mkenda, amesema sera hiyo iliyopitishwa na Rais Samia kupitia Baraza la Mawaziri, inatekelezwa sambamba na mtalaa mpya ulioanza mwaka 2024.

“Mageuzi yaliyoko katika sera ni makubwa na yanatekelezwa kwa awamu. Tutashuhudia kila mwaka hatua zinazochukuliwa katika kuimarisha sekta ya elimu. Haya ni mabadiliko makubwa yatakayogusa vizazi vijavyo,” amesema Profesa Mkenda, aliyekuwa ameambatana na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga.

“Tunasikia watu bado wanatoa michango mbalimbali kuhusu masuala ya elimu. Kuna hoja mbalimbali zinazungumzwa na sisi tunafuatilia, yako majibu karibu ya hoja zote katika sera na mitaala mipya,” amesema.

Profesa Mkenda ametoa mfano wa mjadala mkubwa unaoendelea nchini wa lugha ya Kingereza, somo la hisabati na akili mnemba ambayo yote yameelezewa kwenye sera na mtalaa mpya jinsi ya kushughulikiwa.

“Leo napenda kuwaeleza kuwa kutakuwa na uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya 2014 toleo la 2023. Uzinduzi huo utafanyika Januari 31, 2025 na utafanywa na Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.

Waziri Mkenda amehimiza jamii kushirikiana na Serikali kuhakikisha mabadiliko haya yanafanikiwa. “Kila mmoja wetu anapaswa kuchangia kwa nafasi yake ili kufanikisha utekelezaji wa sera hii,” amesema.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, uzinduzi wa Sera ya Elimu toleo la 2023 ni hatua muhimu kuelekea mageuzi ya kweli katika sekta ya elimu nchini.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie, amesema mabadiliko haya yanahitaji kujitolea kwa hali ya juu ili kufanikisha utekelezaji.

Dk Paul Loisilie amesema mabadiliko yaliyofanyika katika sekta ya elimu ni makubwa na hivyo yanahitaji watu kujitolea kwa hali ya juu kuliko hivi sasa katika kufanikisha utekelezaji wake.

Amesema jambo la kwanza linalotakiwa kufanyika ni wadau kuwa na nia, kwa sababu hiyo ndiyo itakayowawezesha kushinda changamoto zilizopo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.

“Jambo la pili ni hamasa, Serikali ilete hamasa kwa walimu hasa shuleni na sio vitisho, walimu waonyeshwe wana uwezo na wanaungwa mkono na Serikali katika kutekeleza mtalaa mpya. Bila hamasa yatakuwa ni mambo ya kawaida,” amesema.

Dk Loisulie amesema jambo jingine linalotakiwa kufanyika ni kutenga rasilimali za kutosha katika utekelezaji wa sera na mtalaa kwa kuwa kuna baadhi ya maeneo yanahitaji vifaa.

“Jamii nzima pia ione kuwa jambo hili lina faida, isionekane kuwa ni kitu kilicholetwa tu bali iwe tayari kukikopokea na kukitumia kwa mtazamo chanya,” amesema.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St. John, Dk Shadidu Ndossa, ameongeza kuwa miundombinu na wataalamu ni sehemu muhimu ya mabadiliko hayo.

“Matumizi ya teknolojia yanapaswa kupewa kipaumbele. Hata kama hatuna walimu wa kutosha, teknolojia inaweza kusaidia kufikisha maarifa kwa wanafunzi wengi kwa wakati mmoja. Tunaweza kutumia intaneti na umeme ili mwalimu mmoja afundishe shule nyingi kwa wakati mmoja,” amesema Dk Ndossa.

jumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Bakari Mtembo, amesema mabadiliko hayo yanaweza kufanikiwa endapo watekelezaji watakuwa na nia thabiti kama ilivyokuwa kwa waasisi wa taifa.

Amesema walimu wanahitaji mafunzo ya kina ili kuongeza uwezo wao wa kufundisha kwa vitendo. “Kwa sasa, walimu wengi wanafundisha kwa nadharia, jambo linalosababisha changamoto katika kufundisha masomo yanayohitaji vitendo,” amesema.

Mtembo pia ameipongeza Serikali kwa juhudi zake katika kuboresha miundombinu ya shule, lakini akashauri kuwa uwepo wa nyumba za walimu uwe miongoni mwa vigezo vya usajili wa shule mpya.

Wadau wameendelea kusisitiza umuhimu wa teknolojia katika kusaidia kutatua changamoto za upungufu wa walimu na vifaa vya kufundishia.

Wamependekeza Serikali kuhakikisha shule nyingi zinaunganishwa na umeme na intaneti ili kuboresha mfumo wa elimu kwa ujumla.

Related Posts