SERIKALI YAWAONYA WAANDISHI WASAIDIZI NA WAENDESHA VIFAA JIMBO LA MBINGA VIJIJINI KUEPUKA ULEVI WAKATI WA ZOEZI LA UANDIKISHAJI KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA

Na Mwandishi Wetu,Mbinga

WAANDISHI wasaidizi na waendesha vifaa vya Bayometriki katika Jimbo la Mbinga vijijini mkoani Ruvuma,wameonywa kutokwenda kwenye vituo vya Uandikishaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura wakiwa wamelewa bali kufanya kazi kwa kujituma, weledi na uadilifu ili waweze kufanikisha kazi hiyo.

Wito huo umetolewa jana na Afisa Mwandikishaji wa Jimbo hilo Pascal Ndunguru,alipokuwa akifungua mafunzo kwa watendaji ngazi ya kata katika jimbo la Mbinga vijijini kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Alisema,mafunzo hayo yanalenga kuwaongezea waledi na ufahamu kuhusu zoezi zima la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na kwenda kuwa waadilifu ili waweze kufanikisha zoezi hilo ambalo Serikali imetumia gharama kubwa kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ujao.

“Pia nawaomba mhakikishe mnawahi kwenye vituo vyenu vya kazi,mkuwe,mkajitume na kujiepusha na ulevi ambao unaweza kuharibu zoezi zima kwenye vituo vyenu,Serikali haitasita kuchukua hatua kwa mwandikishaji yoyote atakayekiuka kiapo cha Tume huru ya uchaguzi”alisema.

Afisa uchaguzi wa Jimbo la Mbinga vijijini Andrew Mbunda,amewataka kwenda kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za Tume huru ya uchaguzi na kufuata maelekezo watakayopewa na Tume ili kufanikisha zoezi hilo muhimu kwa maslahi makubwa ya nchini yetu.

Amewataka kujituma,na kuwa makini kwa kuhakikisha hakuna mwananchi mwenye sifa anayeachwa bila kuandikishwa katika Daftari la kudumu la wapiga kura kwani kufanya hivyo ni kosa,kwa sababu Serikali inatumia fedha nyingi kufanikisha zoezi hilo.

“katika jimbo letu tuna vituo 189 lakini katika uboreshaji huu tutakuwa na vituo 188 kwa sababu tuna kituo kimoja ambacho kitafanya kazi kwenye hatua nyingine”alisema Mbunda.

Pia alisema,watakapokwenda kwenye vituo vya uandikishaji suala la muda ni jambo muhimu kwani kwa mujibu wa maelekezo ya Tume Huru ya uchaguzi kazi ya uandikishaji inatakiwa kuanza saa mbili kamili asubuhi na kufungwa saa 12 jioni.

Mbunda,amewasisitiza maafisa hao kwenda kuwa makini wakati wa zoezi launadikishaji na kuhakikisha wanatunza vifaa watakavyopewa na Tume kwani ikitokea wamepoteza watalazimika kulipa vifaa hivyo.

Afisa kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi(INEC) Nicholaus Natay,amewataka maafisa hao kuzingatia mafunzo yatakayotolewa ili kurahisisha kazi iliyopo mbele yao na kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa muda uliopangwa.

Afisa mwandikishaji kutoka kata ya Mkumbi Halmashauri ya wilaya Mbinga Christina Mapunda,ameipongeza Serikali kwa kuendesha mafunzo hayo kwani yatawasaidia maafisa uandikishaji kufanya kazi kwa weledi mkubwa.

Mwalimu Kidana Shilingi alisema,baada ya mafunzo hayo wananchi na Serikali wategemee mafanikio makubwa kwa kutoa idadi sahihi ya wananchi watakaojitokeza kwenye vituo vya kujiandisha.

 

Related Posts