MAAFANDE wa Tanzania Prisons wamekamilisha taratibu za kumsajili beki wa kati Athuman Sufian Mwemfua (23) kwa mkataba wa miaka miwili kutoka Junguni United ya Ligi Kuu Zanzibar.
Athuman kwa sasa anaripotiwa kuwa Mbeya tayari kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho ambacho kimeruhusu mabao 17 katika michezo 16 ya Ligi Kuu Bara, na kina wastani wa kuruhusu bao kwenye kila mchezo.
Ukuta wa Prisons umekuwa ukionekana kuwa kati ya changamoto kubwa katika ligi msimu huu, ambapo timu hiyo imeshindwa kuzuia ipasavyo mashambulizi ya wapinzani, hali inayochangia kushuka kwa kiwango cha timu katika msimamo wa ligi.
Viongozi wa Prisons wanaamini kuwa beki huyo anaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha safu ya ulinzi ya timu hiyo, ambayo ina kazi kubwa ya kuwa mbali na hatari ya kushuka daraja.
Wakati hivi sasa, Prisons ipo katika nafasi ya 13 kwa pointi 14, kocha mpya wa kikosi hicho, Aman Josiah ni kama ameona ni vigumu kupiga hatua bila kuiboresha timu.
Mchezaji huyo pia anatarajiwa kuongeza ushindani katika kikosi cha Prisons, hasa kutokana na ufanisi aliouonyesha akiwa na Junguani United, ambako alikuwa mchezaji tegemeo katika safu ya ulinzi ya timu hiyo.
Akiongelea uwezo wa beki huyo, kocha wa zamani wa Gwambina na Mtibwa Sugar, Mohamed Badru, ambaye amemshuhudia akicheza ligi ya Zanzibar, alisema; “Beki wa kati kama Athuman ni aina ya wachezaji wanaohitajika kwenye timu kama Prisons, ambao wanahitaji kuimarisha safu yao ya ulinzi.”
Aliongeza kwa kusema; “Ana nguvu, kasi na uwezo wa kusoma mchezo, na nadhani atasaidia kwa kiasi kikubwa. Ligi Kuu Bara ni ngumu, lakini sidhani kama atapata shida.”