Sidibe siku zinahesabika Azam | Mwanaspoti

WAKATI kikosi cha Azam FC kikiendelea kujifua ili kujiweka fiti kwa ngwe ya lalasalama ya Ligi Kuu Bara itakayorejea Machi Mosi, inaelezwa kwamba beki wa kushoto wa kimataifa wa timu hiyo kutoka Senegal, Cheikh Sidibe anahesabiwa siku kabla ya kumtemwa kabla dirisha la usajili halijafungwa.

Mwanaspoti limedokezwa kwamba beki huyo anayeitwa mara kadhaa timu ya taifa ya Senegal, yupo hatua ya mwisho ili kuondoka klabu hapo ikielezwa huenda akaibukia AS Vita ya DR Congo inayompigia hesabu kutokana na kocha Youssouf Dabo aliyewahi kuinoa Azam kuagiza asajiliwe haraka.

Chanzo cha ndani kutoka Azam kimeeleza kwamba viongozi wamefanya kikao na kukubaliana kuachana na Sidibe wakiweka mikakati ya kusajili wachezaji wengine wa kimataifa ili kuongeza nguvu katika kikosi hicho.

Majuzi klabu hiyo ilimtambulisha beki wa kati anayemudu pia eneo la kushoto, Zouzou Lendry.

“Uongozi umefikia hatua ya kuachana na Sidibe kutokana na sababu mbalimbali ambazo siwezi kuziweka wazi, lakini wanaendelea kufanya mazungumzo na wachezaji kutoka nchi mbalimbali,” kilisema chanzo.

“Pia kuna uwezekano wa kumkosa Gibril Sillah ambaye kapata ofa kutoka AS Vita, ingawa bado viongozi wanazungumza naye kuona kama itawezekana kubaki.”

Sidibe ambaye alisajiliwa na Azam kutoka Teungueth ya Senegal, alikuwa mmoja wa wachezaji tegemeo wakati Azam ikiwa chini ya Dabo aliyetimuliwa na kuibuka AS Vita na nafasi yake kuchukuliwa na Mmorocco Rachid Taoussi.

Kwa sasa Taoussi hamtumii mara kwa mara mchezaji huyo katika beki ya kushoto inayochezwa zaidi na Paschal Msindo.

Mwanapoti lilipomtafuta Mkuu wa Idara ya Habari ya Azam, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ ili kupata ufafanuzi juu ya taarifa hizo, alijibu kwa kifupi: “Sifahamu lolote kuhusiana na hilo unajua kuna taarifa ni nyingi mitandaoni ila ndani ya klabu hakuna hilo.”

Related Posts