Mnunka akubali yaishe Simba Queens

BAADA ya kukaa nje ya uwanja kwa takribani miezi mitano, hatimaye straika wa Simba Queens, Aisha Mnunka amekubali yaishe na kuingia kambini na wenzake.

Agosti Mosi, mwaka jana Mwanaspoti iliripoti nyota huyo wa timu ya taifa (Twiga Stars) ametoroka kambini ikiwa ni siku chache tangu atoke kwenye majukumu ya taifa.

Hata hivyo, baada ya Simba kutomuona kambini na wenzake walijaribu kumtafuta kupitia simu yake ya mkononi lakini hakupatikana wakisikia amefichwa na timu moja inayoshiriki Ligi Kuu.

Ukimya wake ukawafanya Simba wakimbilie Shirikisho la Soka nchini (TFF) kushtaki juu ya utoro wa mchezaji wao ambaye ana maliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu.

Baada ya shitaka hilo kupokewa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji chini ya Mwenyekiti, Said Soud Desemba 13 likasilikizwa kwa pande zote mbili kwa mchezaji na timu.

Kamati hiyo iliamuru pande zote mbili zikae na kumaliza tofauti zao na Simba ilionyesha imekubali kumpokea nyota wao na kukubali wamalizane na sasa mambo yako freshi.

Mmoja wa viongozi wa mabingwa hao wa Ligi ya Wanawake ambaye hakutaka kutajwa jina alisema mambo yamekwenda vizuri na sasa mchezaji yuko kambini na wenzie.

“Sisi tangu mwanzo hatukuwa na shida na mchezaji kwa sababu bado ni mchezaji mdogo ndio maana tulianza kumtafuta na kumjulia hali kama amepata tatizo,” alisema kiongozi huyo na kuongeza;

“Tunashukuru TFF kwa kuisimamia kesi hii vizuri.”

Related Posts