Mradi wa LNG Lindi wanukia, mazungumzo karibu kukamilika

Dar es Salaam. Mazungumzo ya utekelezaji wa mradi wa kusindika gesi asili kwenda kwenye kimiminika (LNG) mkoani Lindi huenda yakafika tamati mapema mwaka huu, huku kila upande ukiwa na matumaini ya kupata ‘dili’ lililo bora.

Mradi huo wenye thamani ya Dola bilioni 42 za Marekani (Sh106.1 trilioni) unatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 1,000, zikiwemo 500 za kudumu, lakini utekelezaji wake umekuwa ukisuasua, sababu kubwa ikitajwa ni kutokamilika kwa majadiliano baina ya Serikali na wawekezaji.

Wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Andrreas Kravik, aliyetembelea miradi mbalimbali inayofadhiliwa na nchi yake pamoja na ile ya uwekezaji kutoka katika taifa hilo la Nordic, kampuni zinazotekeleza mradi huo zilieleza huenda majadiliano yao na Serikali sasa yakafika mwisho.

Baada ya kutembelea eneo ambalo mradi huo, Januari 10, 2025, Kravik amesema Serikali ya Taifa lake inatamani kuona mradi huo ukitekelezwa mapema kwa kuwa una faida kubwa kwa Tanzania, watu wake, na wawekezaji.

Amesema mradi huo ni muhimu si tu kwa Lindi, bali Tanzania nzima kwa upande wa nishati, kazi, na kodi, na kuongeza kwamba utekelezaji wa mradi huu ni sehemu ya uhusiano wa muda mrefu wa biashara kati ya Norway na Tanzania.

“Serikali yangu ipo hapa kuhakikisha kila linalowezekana linahakikisha mradi huu unafanikiwa. Kuna mapendekezo yapo mezani, tunamini kila upande utaweza kuyaridhia. Kwa upande wa wanaotekeleza mradi, nimezungumza nao na wameniambia wako tayari,” amesema.

Mkurugenzi Mkazi wa Equinor Tanzania (kampuni yenye hisa kubwa katika mradi huo) Hilde Nafstad amesema ana imani majadiliano ya mradi huo yatafikia tamati hivi karibuni, akisema inaweza kuwa mwanzoni mwa mwaka huu.

“Kilichokuwepo ni kila upande kupigania haki yake (we need to find a balance). Katika mapendekezo yetu yaliyopo mezani sasa, tunaamini kila upande utanufaika, hivyo tutafikia mwafaka,” amesema Nafstad.

Amesema suala la huduma za bima na za kifedha limewekewa mpango ambao utazifanya taasisi za ndani nazo zinafaike na utekelezaji wa mradi huu.

Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya Shell Tanzania, ambayo ni ya pili kwa ukubwa katika mradi huo, Menno Bax, amesema kutokana na ukubwa wa mradi huo ndiyo maana majadiliano yanakuwa marefu, kwa kuwa kila upande unaangalia namna ya kulinda maslahi yake.

“Nina imani kubwa, kwa kuwa soko la LNG ni kubwa duniani, hivyo tumekuwa tukifanya jitihada za muda mrefu na Serikali. Tunatarajia kumaliza jambo hili. Kwa ushirikiano tunaoupata Serikalini, tuna imani kuwa mradi huu utaanza hivi karibuni,” amesema Bax.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Januari 12, 2025, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk. Felchesmi Mramba, amesema kwa upande wa Serikali, iko tayari na ina matumaini zaidi ya kuanza kwa mradi huu, pengine kuliko hata wawekezaji wenyewe.

“Kama unavyofahamu, tumegundua gesi nyingi, zaidi ya mita za ujazo trilioni 57, na kati ya hizo trilioni 47 ziko mikononi mwa makampuni hayo yanayotaka kutekeleza mradi wa LNG Lindi. Hivyo, pamoja na ugunduzi mkubwa, bado hatujanufaika vya kutosha zaidi ya uzalishaji wa umeme,” amesema Dk Mramba.

“Kwa sasa, tupo hatua za mwisho za majadiliano na tunatarajia mambo yatakwenda vizuri,” amesema Dk Mramba na kuongeza kwamba matarajio ya Serikali ni kuona ugunduzi huu unaleta manufaa makubwa ya kiuchumi, hususan kuleta fedha za kigeni nchini.

Aidha, katika ziara hiyo, naibu waziri huyo alitembelea miradi inayotekelezwa na Taasisi ya Norwegian Church Aid (NCA), ikiwemo ya uwezeshaji watu kiuchumi pamoja na ile ya vijana shuleni.

Related Posts