Zaidi ya koo 45 za Waluguru zafanya tambiko kudumisha amani, kupinga ukatili wa kijinsia

Morogoro. Zaidi ya koo 45 za kabila la Waluguru zimefanya tambiko la tano la kudumisha amani na umoja katika jamii, kutoa elimu ya ulinzi na uhifadhi wa mazingira na kupambana na ukatili wa kijinsia kwa watoto, wanawake, na wazee kwa kushirikisha wadau mbalimbali mkoani hapa.

Akizungumza leo Jumapili Januari 12, 2025 mjini Morogoro, Chifu Mussa Lukwele (Mdimang’ombe) amesema tambiko hilo lililofanyika kwenye mti wa mtamba katika uwanja wa gofu, limehudhuriwa na viongozi wa jadi, wawakilishi wa Serikali na vitukuu wa machifu kutoka koo 52 za Waluguru.

Chifu Lukwele amesema tambiko hilo ni moja ya njia ya kuimarisha mshikamano wa kijamii, kutoa elimu kuhusu ulinzi wa mazingira na kuhamasisha juhudi za kukabiliana na ukatili wa kijinsia.

Shughuli hiyo imeenda sambamba na maandalizi ya vyakula vya asili, kucheza ngoma za kitamaduni na kuvaa mavazi ya asili ya Waluguru, huku zikihitimishwa kwa tambiko rasmi chini ya mti wa mtamba.

“Tambiko hufanyika katika miti mikubwa kama mng’ongo au mtamba, au misitu minene kwa lengo la kutafuta utulivu wa jamii. Vyakula vya asili kama magimbi, viazi vikuu, wali na kunde huandaliwa, huku majina ya wakuu wa koo na mizimu 12 ya kabila letu yakitajwa kwa heshima. Hata hivyo, Mwenyezi Mungu (Mlungu) ndiye anayepaswa kuombwa kwanza,” amesimulia  Chifu Lukwele.

Aidha, amesema kabla ya kuingiliwa kwa tamaduni za nje, jamii ya Waluguru haikuwahi kuchoma moto ovyo wala kuharibu miti ya matunda, bali walihifadhi mazingira kwa kushirikiana na wanasheria wa jadi.

Malkia wa wanawake Waluguru, Wamingila Shilingimbili amewahimiza Watanzania kuendeleza mila na tamaduni za makabila yao ambazo mara nyingi ndiyo huwa mwongozo wa maadili.

Amesema matamasha kama hayo, yanawasaidia hata watoto na vijana kufahamu historia ya kabila lao sambamba na mila na desturi za mababu na mabibi zao.

“Kupuuza tamaduni zetu ndiko kunakosababisha mmomonyoko wa maadili. Tunapofanya matambiko, watoto wanajifunza umuhimu wa vyakula vya asili na maisha ya mababu,” amesema Shilingimbili.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Michezo ya Jadi Tanzania, John Kuchinro akizungumza katika shughuli hiyo, amesema tambiko limekuwa urithi wa vizazi kwa karne nyingi.

Amesema kupitia matamasha ya matambiko,  wazee walimuomba Mwenyezi Mungu alete  mvua na kuondoa balaa.

“Pia, michezo ya jadi kama bao la Kiswahili, kulenga shabaha kwa kutumia pinde na manati, kukuna nazi na kukimbia na kijiko kichwani huchezwa wakati wa tambiko, hii inamaanisha kukuza mshikamano na furaha katika jamii,” amesema Kunchiro.

Related Posts