Mashuhuda wasimulia, moto ukiua 16 Los Angeles

Los Angeles. Mamlaka jijini Los Angeles nchini Marekani zimethibitisha watu 16 kufariki dunia kutokana na janga la moto wa nyika ambao unaendelea kuteketekeza maeneo mbalimbali ya jiji hilo huku idadi ya vifo ikitarajiwa kuongezeka.

Kwa mujibu wa BBC, maofisa jijini humo wamesema leo Jumapili Januari 12, 2025, kuwa wanahofia huenda shughuli ya kutambua walioungua kutokana na moto huo ikachukua wiki kadhaa kwa kutumia vipimo vya vinasaba kwani vipimo vya alama za vidole na nyuso hazitambuliki kwa urahisi kutokana na kuungua vibaya.

BBC imeripoti kuwa miongoni mwa waliofariki dunia kwa kuunguzwa ma moto huo ni pamoja na Victor Shaw ambaye alifariki akipambana kuuzima moto huo ili kuinusuru nyumba yake iliyokuwa eneo la Altadena.

Taarifa ya kifo chake imethibitishwa na familia yake kuwa mwili wa mwanaume huyo (66) ulikutwa ukiwa katika barabara inayopita karibu na yalipokuwa makazi yake huku akiwa ameshikilia mashine ya kufanyia usafi kwenye bustani.

Victor aliyekuwaakiliki nyumba hiyo kwa miaka 50 iliyopita huku akiishi na dada yake Shari Shaw, ambaye alijaribu kumshawishi Jumanne Januari 7,2025, waondoke ndani ya nyumba hiyo hata hivyo aligoma kwa madai kuwa hatoweza kuiacha nyumba yake ikateketea.

Shari ameikieleza kituo cha televisheni cha CBS, kuwa kaka yake aligoma kutoka ndani ya nyumba hiyo kwa madai kuwa anataka kupambana kuikinga dhidi ya moto huo wa nyika huku yeye akiondoka na kumuacha baada ya kuona moto unazidi kusogea kwa kasi.

“Wakati bado nikiwa naye pale tuliona kama kimbunga cha moto kikija kwenye nyumba yetu, mimi niliogopa nikaondoka,” Shari ameieleza CBS News huku akidai kuwa atamkumbuka sana kaka yake.

“Nitakumbuka nilivyokuwa nikiongea naye, kutaniana naye, kusafiri naye, nitamkumbuka hadi siku ya kifo changu,” amesema Shari huku akidokeza kuwa jambo linalomchukiza ni uamuzi wake wa kugoma kuondoka naye kuupisha moto huo.

Mbali na Victor, raia mwingine aliyefariki katika moto huo na kutambulika ni Anthony Mitchell na mtoto wake, Justin, wote walifariki wakiwa ndani ya nyumba yao eneo la Altadena wakati wakipambana kuukimbia moto huo.

Kwa mujibu wa mke wa Antony, Hajime White alipozungumza na Gazeti la The Washington Post, amesema alipokea simu kutoka kwa mmewe (67), akimueleza kuwa moto huo umeyazingira makazi yao.

Mitchell, ambaye ni muuzaji wa bidhaa mstaafu, alikuwa akiishi na mtoto wake (Justin) ambaye alikuwa na umri unaodhaniwa kuwa miaka (20) na alikuwa alisumbuliwa na tatizo la Mtindio wa Ubongo.

Mtoto mwingine wa Antony anayeitwa Jordan, alinusurika kifo hicho kwa sababu alikuwa amelazwa hospitalini akisumbuliwa na maambukizi jambo ambalo lilimnusuru na kudhuriwa na moto ulioiteketeza familia yake.

White anasema baada ya muda flani kupita alipokea taarifa ya kifo cha mme wake na mtoto wake huku akidai anahisi kama amedondokewa na jiwe kubwa kichwani mwake.

Mitchell alikuwa ni baba wa watoto wanne na babu wa wajukuu 11, vitukuu 10, White aliieleza The Washington Post.

Mwingine aliyetambulika kufariki kutokana na moto huo ni Rodney Nickerson ambaye alimweleza mtoto wake kuwa angeweza kuwa hai siku inayofuata hata hivyo hakuweza kutimiza ahadi hiyo.

Rodney Nickerson (83) alifariki akiwa nyumbani kwake eneo la Altadena, kwa mujibu wa binti yake ambaye anasema baba yake aliamini kwamba moto huo wa nyika ungepita bila kuwaachia madhara.

Kimiko Nickerson, amesema kuwa baba yake alinunua nyumba hiyo mwaka 1968 na kwamba tangu wakati huo amekuwa akikumbana na majanga ya moto wa nyika kutokana na sehemu kubwa ya Los Angeles kuwa yenye jangwa kwa miongo kadhaa.

Kwa mujibu wa Nickerson, baba yake ambaye alikuwa alihudumu kama Mhandisi wa Miradi mbalimbali kwa miaka 45, anakumbuka kauli ya mwisho kutoka kwa baba yake alimwambia kuwa “ Kesho nitakuja kukupa.”

Mwathiriwa mwingine wa moto huo ambaye ametambulika ni raia wa Australia, Rory Callum Sykes (32) ambaye alifariki katika moto uliounguza makazi eneo la Palisades siku ya Jumanne na taarifa ya kifo chake imethibitishwa na mama yake mzazi, Shelley Sykes kupitia mtandao wa X.

Shelley anasema alikuwa na mtoto wake huyo ambaye alikuwa akisumbuliwa na tatizo la mtindio wa ubongo katika makazi yao yenye ukubwa wa Eka 17 eneo la Malibu jijini humo.

“Imeniuma sana,” amesema Shelley, ambaye ni mzaliwa wa Uingereza mwenye uraia wa Australia anayesumbuliwa na tatizo la uoni hafifu na asiye na uwezo wa kutembea kutokana na umri wake kuwa mkubwa.

Shelley alivieleza vyombo vya habari vya Australia kuwa alishindwa kumuokoa binti yake kwa sababu hana mkono mmoja kutokana na maradhi yanayomsumbua.

Miongoni wa marehemu waliotambulika kufariki katika moto huo ni kikongwe, Erliene Kelley (83) ambaye mwili wake ulipatikana Alhamisi ya wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa mjukuu wa Kelley, Briana Navarro, Bibi yake aligoma kuondoka kwa sababu moto ambao imekuwa ikiibuka katika eneo la Altadena haujawahi kuyafikia makazi yao hivyo aliamini hautoleta madhara kwao.

Amesema saa kadhaa baadae, mamlaka jijini humo, zilithibitisha kuwa kikongwe huyo alikuwa amefariki kwa kuungua na moto nyumbani kwake eneo la Altadena.

Wakati watu hao wakiripotiwa kufariki katika moto huo, vyombo vya habari nchini humo vimeripokiti kuwa kumeibuka wimbi jipya la urushaji wa ndege zisizo na rubani (droni) katika maeneo yaliyoathiriwa na moto huo.

Idara ya Zimamoto jijini Los Angeles imeonya kuwa droni hizo ni hatari na zinapunguza ufanisi wa shughuli ya kuzima moto huo na kuingiliana na ndege zinazomwaga maji maeneo mbalimbali yaliyofikiwa na moto huo.

Katika kipindi cha Saa 24, Droni 30 zilionekana zikiruka katika anga la Palisades, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Zimamoto ya Los Angeles, Sheila Kelliher.

Kelliher amesema moja ya ndege kubwa aina ya Super Scooper ‘Quebec 1’ iliyokopwa kutoka Canada kusaidia kupambana na moto huo ililazimika kushushwa ardhini baada ya kugongana na moja ya droni hizo.

Ofisa huyo amesema ndege hiyo ilipata mchubuko na imesitisha kuendelea na shughuli ya uzimaji wa moto japo hakuna majeraha yaliyotokana na ajali hiyo.

“Kama droni zitaonekana eneo lolote unapozimwa moto tafsiri yake shughuli hiyo itasitishwa kwa muda kwa sababu za kiusalama, huko ni kukwamisha na kuhatarisha usalama wa maisha na mali za watu ambazo ziko hatarini kuungua,” amesema Ofisa huyo.

Katika hatua nyingine, Mwandishi wa BBC aliyebobea kwenye masuala ya Utabiri wa Hali ya Hewa, amesema upepo mkubwa unatarajiwa kuongezeka leo Jumapili katika eneo la Los Angeles jambo linaloweza kuongeza kasi ya moto huo.

Upepo mkali unatarajiwa kuongezeka maradufu wakati ambao robo tatu ya eneo la Malibu limeshateketea kutokana na moto huo kwa mujibu wa Meya, Doug Stewart.

“Tutakuwa na kazi kubwa sana ya kuijenga upya Malibu lakini wakati tunawaza kuijenga upya bado tunakazi kubwa ya kufanya kuhakikisha moto huu tunaudhibiti,”  amesema Meta Stewart.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Related Posts