ALIYEKUWA kocha mkuu wa TMA, Maka Mwalwisi amesema sababu kubwa za kuamua kuachana na kikosi hicho cha jijini Arusha ni kutokana na baadhi ya viongozi wake kumuingilia katika majukumu yake uwanjani, ikiwamo kumpangia wachezaji wa kuwatumia.
Akizungumza na Mwanaspoti kocha huyo aliyezifundisha timu za Singida Black Stars zamani Ihefu na Mbeya City, alisema kwa sasa asingependa kuongelea mambo mengi zaidi baada ya kuachana na kikosi hicho, ingawa ameamua kuondoka kiroho safi tu.
“Jambo hilo la kupangiwa aina ya wachezaji wa kuwatumia limekuwa kwa muda mrefu sasa nikaona ifike mahali niheshimiwe na taaluma yangu, nilichukua uamuzi wa haraka kuwaandikia barua wa kujiuzulu na nashukuru wamekubali ombi langu,” alisema.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa TMA, Chris Salongo alipotafutwa na Mwanaspoti kuzungumzia juu ya sakata hilo, alisema yupo kwenye kikao hivyo, asingependa kuzungumza chochote hadi atakapokuwa na muda mzuri wa kuzungumzia.
Mwalwisi alijiunga na timu hiyo Januari Mosi mwaka jana akitokea Mbeya Kwanza, huku msimu huu akiiongoza katika michezo 15, ambapo ameshinda minane, sare mitatu na kupoteza minne, akiiacha katika nafasi ya tano kwa pointi 27.