Tani zaidi ya 8400 za mahindi aina ya C105 kuzalishwa na vijana wa BBT awamu ya pili

Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma

 Imeelezwa kuwa vijana awamu ya pili wa mradi wa Jenga kesho iliibora (BBT),wanatarajia kuzalisha tani zaidi 8400 za mbegu bora ya mahindi aina ya C105 katika  ekari 4,200 za shamba la Ndogoye lililopo wilayani Chamwino mkoani Dodoma.

 Mkurugenzi Msaidizi Mipango na Bajeti wa Wizara ya Kilimo Mohamed Chikawe ameyabainisha hayo leo  jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokelewa kwa vijana wanufaika wa mradi kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.

Chikawe amesema katika shamba hilo wanatarajia kupokea vijana 420 ambapo kila kijana mmoja atakabidhiwa Ekari 10 kwa ajili ya uzalishaji wa aina hiyo ya mbegu itakayotumika katika msimu wa kilimo.

“Mpaka sasa tumeshapokea vijana 209 na bado wanaendelea kuwasili ili kufikia idadi hiyo ya vijana katika shamba hilo ambalo ni awamu ya pili ya vijana kuwasili,”alisema Chikawe.

Chikawe amesema zaidi ya kuwa vijana hao wanakwenda kuzalisha mbegu za mahindi aina hiyo ya C105 zitakuwa mbegu bora kwa sababu watazalisha chini ya usimimazi wa wataalam wa kilimo kutoka taasisi za uzalishaji mbegu bora.

Hata hivyo amesema maandalizi kwa ajili ya kiwapokea vijana hao yamekamilika ambapo alisema katika shamba hilo kila kitu ambacho kinahitajika kwa ajili ya kilimo kipo kwa ajili ya kuanza uzalishaji.

Alisema vijana wote wako katika hali ya usalama tayari kwa kuanza uzalishaji wa mbegu hizo

Kwa upande wa  vijana wawanufaika wa mradi huo,Fanuel Buu kutoka wilaya ya Babati mkoani Manyara amesema anaishkuru serikali kutokana na kutoa fursa za kilimo kwa ajili ya vijana mbalimbali hapa nchini.

Buu amesema fursa hizo zinachangia kupunguza uhaba wa ajira kwa vijana lakini pia zinasaidia kuwaweka vijana bize kwa ajili ya kujiandaa na maisha yao ya badae ikiwemo kujiinua kiuchumi.

“Vijana tunapopata fursa kama hizi tuzichangamkie ili zitusaidie kujiinua kiuchumi ikiwemo kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri ajira kutoka serikali na watu binafsi,”alisema Buu.

Naye Ilumbo Yohana kutoka wilayani Chamwino mkoani hapa alisema,wanakwenda kutumia fursa hiyo ya kilimo iliotolewa na serikali kwa vijana kwa sababu inakwenda kuwainua kiuchumi wao wenyewe na kukuza uchumi wa taifa kupitia sekta ya kilimo.

Aidha amesema kilimo hivi sasa ni fursa kubwa kwa vijana hasa ukizingatia serikali imewekeza kwenye sekta hiyo hivyo vijana wanapaswa kuchangamkia fursa zinazotolewa na serikali.

Kutokana na hilo aliwataka vijana kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kufanya maendeleo mbalimbali ambayo husaidia kukuza maendeo ya kiuchumi.

Related Posts